Hotuba ya upinzani yalikoroga Bunge

Posted in
No comments
Wednesday, July 18, 2012 By danielmjema.blogspot.com



HOTUBA ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imelivuruga Bunge.

Hali hiyo ilitokea jana wakati Msemaji wa kambi hiyo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Vincent Nyerere aliposoma hotuba ya kambi yake kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.

Hotuba hiyo ilitanguliwa na hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi aliyewasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka huo wa fedha.


Utata alianza baada Vincent Nyerere kufika ukurasa wa Pili wa hotuba yake ambako Mnadhimu Mkuu wa Serikani Bungeni, William Lukuvi alisimama na kuomba Mwongozo wa Spika.

Wakati akiomba mwongozo huo, Lukuvi alitumia Kanuni ya 64 (1) A hadi C inayozuia wabunge kujadili mambo yaliyo mahakamani.

Katika maelezo yake, Lukuvi alisema ukurasa wa tatu ambao Vincent alikuwa hajausoma, ulikuwa na mambo yanayohusu kesi zilizoko mahakamani na kwamba haukupaswa kusomwa kwa kuwa ulikuwa na maneno yanayokiuka Kanuni za Bunge.

“Mheshimiwa Spika, maelezo ambayo yapo kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani yanayoelezea mauaji ya viongozi wa Chadema Igunga, Usa River, vitisho kwa wabunge wao na kutekwa kwa Dk. Stephen Ulimboka, hayapaswi kusomwa kwani kesi za mambo hayo ziko mahakamani.

“Pia baadhi ya watuhumiwa wa matukio hayo wameshafikishwa mahakamani kwani hata tukio la kuuawa kwa Mwenyekiti wa UVCCM Iramba Singida lipo katika upelelezi mkali wa polisi.

“Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, naomba kiti chako kitumie busara katika kuamua jambo hili kwani maelezo hayo yakisomwa yanaweza kuvuruga uchunguzi ingawa kambi ya upinzani inaweza kuyapeleka polisi maelezo haya kuwasaidia katika upepelezi wao,” alisema Lukuvi.

Lukuvi alipomaliza kusema hayo, maneno yake yalionekana kutomfurahisha Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA).

Lissu alisimama na kulalamika kuwa Spika hatakiwi kumsikiliza Lukuvi kwa kuwa akikubali alichokiomba, atakuwa hawatendei haki wapinzani ambao idadi yao ni ndogo ikilinganishwa na wabunge wa CCM.

“Mheshimiwa Spika, naomba ututendee haki ingawa sisi ni wachache kwani ni jana tu wabunge wa CCM walizungumzia masuala haya bila kuzuiwa.

“Baadhi ya wabunge wa CCM jana waliwashutumu wabunge wa Chadema kuwa walihusika katika mauaji hayo huku Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema akisema baadhi yao wataitwa polisi kutoa maelezo.

“Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, nasikitika hotuba yetu kukatishwa na tukio hili sijawahi kuliona tangu niingie hapa bungeni…sijawahi kuona msomaji wa hotuba iwe kwa upande wa Serikali wala Kambi Rasmi ya Upinzani inakatishwa na kuzuiwa kusoma kile alichotakiwa kusoma," alilalamika Lissu.

Kutokana na maelezo hayo, alimtaka Spika Anne Makinda atumie Kanuni ya tano kuwatendea haki.

Lissu alipomaliza kusema hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, alisimama na kusema kuwa kutenda haki ni kufuata kanuni zinazoendesha Bunge wala si vinginevyo.

Hata hivyo, alikana baadhi ya wabunge wa CCM kuwashutumu wabunge wa Chadema kwamba wanahusika na mauaji ya kijana huko Singida jambo ambalo lilisababisha wabunge wagune.

“Kama ni kukosa nidhamu hilo ni tatizo lake kwani hata kiti alichokaa Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani kimevunjika.

“Jana (juzi) jioni, nilisema wabunge ambao wataombwa kwenda kutoa maelezo polisi wafanye hivyo kutoa ushirikiano lakini maelezo yaliyoko katika Kambi ya Upinzani yaondolewe.

"Mheshimiwa Spika, jana jioni kwa kutumia kanuni ya 48 nina imani kuwa waheshimiwa wabunge watakiri kuwa haya si jambo la kuingia kwenye hotuba, hivyo naunga mkono hoja ya Mnadhimu Mkuu wa Serikali ya kutaka maneno hayo yasisomwe hapa bungeni," alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kutokana na maelezo hayo, Spika alilazimika kuingilia kati na kupinga kauli kwamba wapinzani wanaonewa kutokana na uchache wao bungeni.

“Hapa hakuna anayeonewa, inapaswa kila mtu kutambua kuwa mtu yeyote awe wa Serikali au upinzani anaposoma hotuba inayokwenda kinyume na kanuni anaweza kuzuiwa kuendelea hata kama akiwa mmoja au kambi.

"Yeyote atakayesema kitu ambacho ni kinyume na utaratibu na kanuni lazima atakuwa interrupted (ataingiliwa), awe waziri au mbunge wa chama chochote, huo ndiyo utaratibu wetu.

“Unaweza kuzungumza au kujadili masuala yoyote isipokuwa yale yaliyopo mahakamani, yale yaliyo katika upelelezi unaweza kuyazungumza kwani utakuwa unawasaidia polisi kupata ukweli.

“Kwa hiyo, kama hayo mambo yako mahakamani, naomba yasisomwe hapa, naomba mnieleze ni yapi yaliyo mahakamani maana mimi siyajui, naomba mnieleze ili yaachwe kwa mujibu wa Kanuni ya 64.

“Nayasema haya kwa sababu kumekuwa na lawama nyingi zinazotupiwa Bunge kuwa limekuwa linaingilia na kutoa uamuzi katika masuala ambayo yapo nje yake hususan yaliyo mahakamani,” alisema Spika.

Baada ya maneno hayo, Waziri Lukuvi alisimama na kuyataja mambo hayo kuwa ni suala la kupigwa linalomhusu Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), suala la kutekwa Mweyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka na tukio la kifo cha mfuasi wa CCM kilichotokea Singida mwishoni mwa wiki.

"Kuhusu suala la Mwanza nalo lilifikishwa mahakamani na tayari mbunge mmoja aliyetajwa kuhusika naye akamtaja mwingine na aliyetendewa yupo humu na anaendelea vizuri," alisema Lukuvi.

Hata hivyo, Lukuvi aliposema kuna mtu amekamatwa kuhusiana na kutekwa kwa Dk. Ulimboka, wabunge wa Chadema walilipuka kwa pamoja na kusema huyo ni kichaa lakini Lukuvi aliwapinga na kusema kichaa kinatofautiana.

Alipomaliza kusema hayo, Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (CHADEMA) alisimama na kuomba Mwongozo wa Spika akisema kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, maneno yanayolalamikiwa hayapaswi kuondolewa kwa kuwa hayaingilii mahakama.

“Hotuba yetu inatoa maelezo ya awali tu kuhusu matukio ya vitisho na mauaji ya wanasiasa na kuwashutumu baadhi ya wabunge wa CCM wanaosema Chadema walihusika na mauaji ya Iramba Magharibi huko Singida,” alisema Wenje.

Baada ya mvutano kushika kasi, Lissu alisimama tena na kusema kama kweli masuala hayo yako mahakamani, Lukuvi alitakiwa kutoa ushahidi wa kutosha kwa kutaja namba ya kesi, walalamikiwa ni akina nani na kesi hizo ziko katika mahakama zipi.

Alipomaliza kusema hayo, Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Abwao (CHADEMA), naye alisimama na kuomba Mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni ya 68 akitaka kujua ni kanuni ipi iliyotumika kumkatisha Vincent wakati kinacholalamikiwa alikuwa hajakisoma.

Akijibu hoja hiyo, Spika Makinda alisema Lukuvi alikuwa sahihi kumkatisha Vincent kwani yanayolalamikiwa yako kwenye kitabu ambacho wabunge walikuwa wameshagawiwa mapema.

Mvutano ulipoendelea, Mbunge wa Bariadi Magharibi, John Cheyo (UDP), naye alisimama na kutumia Kanuni ya 76 (1) kinachoeleza jinsi Spika anavyotakiwa kuahirisha Bunge kutatua vurugu zilizotokea bungeni.

Kwa mujibu wa Cheyo, hali ya utulivu ilikuwa imetoweka bungeni na kwamba ili kunusuru hali hiyo, ni Spika kuahirisha Bunge suala hilo likajadiliwe kwenye Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Hata hivyo, Spika Makinda alikataa kwa kile alichosema kuwa hakuna sababu ya kuahirisha Bunge kwa kuwa hakukuwa na hali mbaya badala yake akamtaka Vincent aendelee kusoma hotuba yake ila asisome ukurasa wa tatu hadi wa sita uliokuwa ukilalamikiwa.

Akitoa taarifa ya Kamati ya Bunge Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge jana jioni, Spika alisema kamati hiyo ilikubali wapinzani wasome kipengele kinachohusu kada wa Chadema aliyeuawa Igunga wakati wa uchaguzi mdogo kwa kuwa suala hilo haliko mahakamani.

Pamoja na hayo, alisema mauaji ya Usa River Arusha, kuvamiwa kwa wabunge wa Chadema mkoani Mwanza, kuvamiwa kwa Mchungaji Msigwa, Kutekwa kwa Dk. Ulimboka na tukio la kifo cha kijana wa CCM huko Singida yasizungumzwe bungeni kwa kuwa masuala hayo yako mahakamani.
Na Maregesi Paul, Dodoma

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .