HIVI NDIVYO MAHAKAMA ILIVYOENDESHA KESI ILIYOMPA USHINDA PROF. MAHALU NA GRACE

Posted in
No comments
Saturday, August 11, 2012 By danielmjema.blogspot.com

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, akiteta jambo na waandishi wa habari
Prof. Mahalu akifuatilia hukumu iliyomweka huru
Grace akiingia Mahakamani Juzi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwachia huru aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martine, baada ya kuonekana hawana hatia. Hukumu hiyo, ilisomwa jana na Hakimu Mkuu Mkazi, Illivin Mugeta, kwa saa moja na nusu, huku umati uliofurika katika mahakama hiyo ukisikiliza kwa makini, akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (CHADEMA).

“Namtegemea Mungu zaidi, yeye ndiye wa mwisho kuhukumu, siwezi kuwa na wasiwasi kwa sababu namwamini Mungu,” maneno ya Mahalu aliyozungumza muda mfupi kabla ya hakimu kuingia mahakamani.


Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mugeta alisema washitakiwa walikuwa wakikabiliwa na mashitaka sita, yakiwemo ya kula njama, kutumia nyaraka mbalimbali kuidanganya Serikali, kuiba Euro 2,065,827.60 na kuisababishia hasara Serikali.

Alisema upande wa mashitaka katika kesi hiyo, ulipeleka mashahidi saba kwa ajili ya kuthibitisha mashitaka dhidi ya washitakiwa.

“Kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani, hakuna ushahidi wa kuonyesha kwamba Euro 2,065,827.60 zilichukuliwa na washitakiwa,” alisema.

Alisema aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Jakaya Kikwete (sasa Rais) na Profesa Mahalu, walishiriki katika utaratibu wa kununua jengo la ubalozi nchini Italia.

“Waziri alikwenda Italia kwa shughuli zake, lakini alipata nafasi ya kulitembelea jengo na suala la mikataba miwili alilijua na alielekeza malipo ya awali yafanyike haraka,” alisema.

Alisema kuna mkanganyiko, kwani upande wa mashitaka unadai taratibu hazikufuatwa katika ununuzi, lakini ushahidi unaonyesha taratibu zilifuatwa kwa sababu wataalamu walitumwa kufanyia tathmini jengo hilo lililonunuliwa.

Alisema mikataba miwili ya mauziano, ilifanyika kutokana na mazingira yaliyokuwepo, hakuna ushahidi unaoonyesha kama kuna fedha ziliibwa.

“Hakuna ushahidi wa kweli kwamba washitakiwa waliiba, upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kosa hili,” alisema.

Alisema katika makosa ya kutumia nyaraka mbalimbali kudanganya Serikali ili kujipatia fedha si kweli, nyaraka zilizotumika zilikuwa halali kwa ajili ya ununuzi wa jengo hilo, lililogharimu Euro 3,098,741.40.

“Nyaraka hizi hazikuwa na maelezo yoyote ya kupotosha ukweli na zilisainiwa na Profesa Mahalu,” alisema.

Alisema Jamhuri, imeshindwa pia kuthibitisha mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara na kula njama.

Alisema kwa mashitaka yote sita, washitakiwa wanaachiwa huru kwa sababu upande wa mashitaka, umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

Inadaiwa mwaka 2002, washitakiwa wote walikula njama ya kuiba Euro 2,085,827.60, kwa madai kwamba walinunua jengo la ubalozi mjini Rome, Italia kwa Euro 3,098,741.40, wakati jengo hilo lilinunuliwa Euro 1,032.913.80.

Ilidaiwa mikataba miwili, iliandaliwa kwa ajili ya kuhalalisha tofauti ya fedha ambazo washitakiwa waliiba.

Washitakiwa, baada ya kuachiwa huru walitoka kwa furaha katika kizimba cha mahakama hiyo, huku wakiwa wamezingirwa na watu wengi waliofika kushuhudia hukumu hiyo ikisomwa.

Akizungumza baada ya hukumu, Profesa Mahalu alisema anarudi kuendelea kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anashukuru Mungu kwa kumpigania.

“Mungu amenipigania, ninashukuru sana na mahakama imefanya kazi yake, naelekea kanisani kufanya ibada ya kumshukuru Mungu kwa aliyonitendea,”alisema Mahalu, huku akielekea kwenye gari na kumalizia kwa kuuambia umma uliokuwa ukimzunguka kwamba anawapenda.

Mawakili waliokuwa wakimtetea Mahalu, Alex Mgongolwa na Mabere Marando, kwa nyakati tofauti walishukuru uamuzi uliotolewa na mahakama, kwa sababu mteja wao hakustahili kushitakiwa.

Katika kesi hiyo, upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi watatu, akiwemo Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye katika ushahidi wake, alimtetea Profesa Mahalu, kuwa alifuata taratibu zote.

Mkapa aliithibitishia mahakama kwamba anamfahamu Mahalu ni mtu safi, hawezi kutenda makosa yanayomkabili, kwani hata yeye alikuwa akifahamu taratibu za ununuzi wa jengo hilo.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .