GAMA ASISITIZA POLISI JAMII
Posted in
No comments
Sunday, January 20, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
Na Fadhili Athumani, Moshi
20, Januari
IMEFAHAMIKA kuwa, moja ya mambo ambayo kama
hayatadhibitiwa mapema yanaweza kuhatarisha usalama na amani ya taifa, ni kuwepo kwa uadui wa
aina yoyote kati ya wananchi na Jeshi la polisi.
Tahadhari hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Leonidas Gama katika hafla ya iliyoandaliwa na Jeshi la polisi mkoa wa
Kilimanjaro, katika ukumbi wa chuo cha mafunzo ya Polisi (CCP), mjini hapa
kuadhimisha siku ya wanafamilia wa jeshi la polisi (police family day).
Gama alisema kuwa moja ya mambo yanayoweza kutishia
usalama wa mkoa wa Kilimanjaro na nchi kwa ujumla ni maaskari katika Jeshi hilo
kujijengea uadui na wananchi kwa kutumia nafasi yao vibaya katika kazi za
ulinzi wa usalama na amani ya nchi.
“Ifahamike kuwa usalama wa nchi unahitaji ushiriki
wa wananchi kwa asilimia kubwa, ushiriki huu ndio sababu iliyotukusanisha
mahali hapa na kutufanya tupongezane kwa kazi nzuri ya mwaka jana, kama polisi
itajenga uadui wa aina yoyote ile na wananchi, kuna hatari ya nchi kukumbwa na
balaa,” alisema Gama.
Alisema kuwa, katika siku za hivi karibuni, kumekuwa
na tabia ya baadhi ya maaskari kutumia nafasi zao kazini kuwakandamiza wananchi
na kuongeza kuwa hali hiyo ni hatari maana wananchi wakianza kuonesha hasira
zao kwa jeshi hilo panaweza kutokea maafa makubwa sana.
“Wapo maaskari ambao wanatumia nyota zao,
kulitukanisha jeshi la polisi, wapo maaskari ambao wanatumia vyeo vyao, iwe
mahakamani au hata uraiani kuwakandamiza raia, hali hii ni hatari sana ndugu
zangu katika jeshi la polisi, maana wananchi wakianza kuonesha hasira zao,
kinachoendelea Syria ni maigizo tu,” alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Kilimajaro alisema kuwa pamoja
na kupongezana kwa kufanikiwa kushusha kiwango cha uhalifu ndani ya mkoa, jeshi
la polisi lisijisahau na kuongeza kuwa safari bado ni ndefu hujku akimea tabia
ya maaskari kujiona kama miungu watu katika jamii.
Kuhusu swala la Rushwa katika Jeshi la Polisi Gama
aliwataka Maaskari wa Jeshi hilo kuchangamkia Fursa za mikopo zinazotolewa na
mashirika ya kifedha pamoja na mabenki
kujipatia mikopo na kufanya biashara kujiongezea kipato badala ya kuomba rushwa
kwa wananchi na wahalifu.
Aidha Leonidas Gama alilitaka Jeshi la polisi
kuhakikisha linazuia matukio na Tabia ya Ukahaba pamoja na unywaji Pombe haramu
ulioanza kuota mizizi katika maeneo mengi ya Mkoa huo, hasa katika manispaa ya
Moshi na Wilaya ya Rombo.
Gama alisema kuwa vijana sasa hivi wamejiingiza
katika tabia ya ukahaba na kujiuza miili kama sehemu ya kujipatia kipato huku
akisisitiza umuhimu wa ushiriki wa kila mtu katika nafasi yake kutokomeza
vitendo hivyo vinavyochafua na kushusha heshimu ya mkoa wa Kilimanjaro.
“kuna badhi ya vijana ambao waamua kujiingiza katika
biashara ya kuuza miili ili kujipatia kipato pampja na unywaji pombe, ni
marufuku biashara hii kuendelea hapa mkoani na RPC naomba ulisimamie hilo
kuhakikisha vitendo hivi vinatokomezwa hapa mkoani,” alisema Gama.
Awali, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa,
Robart Boaz, alisema kuwa pamoja na Mafanikio waliyoyapata mwaka jana, jeshi
hilo bado linakabiliwa na changamoto nyingi katika utendaji, ambapo alisema
kuwa kwa mwaka jana changamoto walilokumbana nalo ni upungufu wa rasilimali kwa
maana ya Vifaa vya kufanyia kazi ya ulinzi na usalama.
Boaz alisema, changamoto nyingine lililotishia
mafanikio ya jeshi hilo ni utovu wa nidhamu miongoni wa baadhi ya vijana wake
pamoja na kuongezeka kwa tabia ya kutozingatia maadli ya kazi miongoni mwa maaskari
huku akitahadharisha kuwa mwaka huu ni mwaka wa kujirekebisha hivyo yeyote
mwenye tabia yake mbaya aanze mapema kujirekebisha kabla ya kurekebishwa.
MWISHO.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :