KLABU YA WANAHABARI MKOANI KILIMANJARO (MECKI), WALAANI UKATILI ALIOFANYIWA MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI, ABSALOM KIBANDA.

Posted in
No comments
Saturday, March 16, 2013 By danielmjema.blogspot.com




KLABU ya waandishi wa habari mkoa wa Kilimanjaro(MECKI) imeungana na taasisi,wanaharakati na watu wengine, kulaani tukio la kuvamiwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda.


Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006, alijeruhiwa usiku wa kuamkia Machi 9,  mwaka huu na watu ambao hadi sasa hakuna taarifa ya kufahamika kwao.

Klabu  inalaani kwa nguvu zote mashambulizi  yote, ambayo yamefanywa kwa wanahabari katika kipindi cha takribani miaka miwili mfululizo  ambayo, baadhi yake yamesababisha vifo kwa wanahabari hao na wengine kupata  ulemavu maishani mwao.

Akitoa tamko hilo la wanahabari wote mkoani Kilimanjaro, Mwenyekiti wa MECKI, Rodrick Makundi alikumbusha kwamba ni Jukumu la wanahabari na vyombo vya habari  wanavyoviwakilisha, kuelemisha jamii na kuwasaidia wananchi katika kutiririsha mawazo katika nyanja mbalimbali, kulenga  kuleta uhuru wa kweli  na kujenga demokrasia hata pale inapotokea kukawa na kutofautiana kwa hoja ili mradi sheria za nchi hazivunjwi.

"
Ikumbukwe kwamba ni Jukumu letu sisi kama wanahabari na vyombo vya habari  tunavyoviwakilisha, kuelemisha jamii na kuwasaidia wananchi katika kutiririsha mawazo katika Nyanja mbalimbali, sote tukilenga  kuleta uhuru wa kweli  na kujenga demokrasia  hata pale tunapotofautiana kwa hoja ili mradi sheria za nchi hazivunjwi,"

"Wanahabari mkoani Kilimanjaro, tunaungana na wengine nchini,kulaani lakini kutokatishwa tamaa  na tukio hilo na kuahidi kuendelea kutangaza, kufichua maovu  na kuelimisha jamii kwa kadri maadili ya taaluma yanavyoelekeza,  lengo likiwa ni kuisadia jamii ambayo kwa namna moja ama nyingine sisi ndio wasemaji kwa niaba yao hususani wale wasio na sauti, alisema Makundi".

Aidha aliwataka Waandishi wa Habari, kutumia tukio hilo kama chachu katika kupigania maslahi ya wananchi na rasilimali za nchi ili ziweze kuwanufaisha  wote kwa ujumla na si wachache ambao kwa bahati mbaya wamesahau maadili ya utumishi wa umma.

Klabu inatoa rai kwa serikali kupitia vyombo vyake vya dola, kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo na yale yaliyopita na  wahusika watakaokamatwa wachukuliwe hatua kali za kisheria,kwani  mashambulizi dhidi ya wanahabari ni tishio kwa demokrasia.

Naye Katibu wa MECKI, James Nakajumo, aliitaka jamii isaidie kufichua hujuma dhidi ya wanahabari  kwani tukio la kutekwa na kuteswa kwa Kibanda ni miongoni mwa matukio zaidi ya matano yaliyotokea katika kipindi kifupi kilichopita.

Alisema Klabu inatoa pole kwa Kibanda, familia yake na tasnia ya habari kwa ujumla, lakini kubwa zaidi ni kuomba watanzania kumuombea kwa MUNGU ili aweze kupona haraka na arejee salama katika shughuli za ujenzi wa taifa.

MWISHO





Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .