HALI YA DKT. MVUNGI MHH!!!

Posted in
No comments
Tuesday, November 5, 2013 By danielmjema.blogspot.com

Waandishi wetu, Dar es salaam
HALI ya Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UB), Dk. Emmanuel Mvungi ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imeanza kuimarika taratibu japokuwa bado hajitambui.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana katika Hospitali ya Taasisi ya Mifupa na Ubongo (MOI), Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia alisema, Dk. Mvungi ambaye amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), bado anaendelea kupatiwa matibabu na madaktari bingwa wa taasisi ya MOI.

 “Hadi leo hii (jana), Dk. Mvungi bado hajaweza kujitambua, lakini ukilinganisha na hali aliyokuwa nayo siku ya kwanza anaendelea vyema na tuna imani Mungu atazidi kuimarisha afya yake japokuwa amepata majeraha mengi kichwani,” alisema Mbatia.

Aliongeza kuwa anawashukuru wasamaria wema wakiwemo masheikh, wanazuoni, mapadri ambao walifika kwa nyakati tofauti na kufanya ibada ya kumuombea Dk. Mvungi hospitalini hapo.

Mbatia alisema hata hivyo ibada maalumu ya kumuombea Dk. Mvungi itafanyika leo saa 10 jioni katika Kanisa Katoliki la Mt. Joseph lililopo Posta ya zamani jijini Dar es Salaam na amewaomba wananchi wenye mapenzi mema wajumuike pamoja katika ibada hiyo maalumu.

Alisema hata hivyo ana imani na Jeshi la Polisi chini ya IGP, Said Mwema watafanya uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika wa tukio hilo na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

“Tushirikiane pamoja katika kipindi hiki kigumu cha changamoto inayotukabili ya kuvamiwa na kujeruhiwa Dk. Mvungi, kwani hatuna shaka katika hili ukweli utapatikana,” alisema Mbatia.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa MOI, Almas Jumaa alisema hali ya Dk. Mvungi inaendelea vyema tofauti na awali.

Alisema madaktari wanaomuhudumia wameshauri Dk. Mvungi aendelee kupumzika kwa muda mrefu na wanaoruhusiwa ni ndugu wa karibu kutokana na hali yake.

Gazeti la RAI lilishuhudia viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali wakimiminika katika hospitali hiyo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, Prof. Mwesiga Baregu, Dk. Salim Mohamed Salim kwa lengo la kumjulia hali Dk. Mvungi.

Naye, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alisema jeshi lake linawashikilia watuhumiwa sita ambao wanadhaniwa kuhusika na tukio la kumvamia na kumjeruhi kwa mapanga, Dk. Mvungi.

Dk. Mvungi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sheria katika chama cha NCCR-Mageuzi, alivamiwa juzi saa 7:30 usiku, nyumbani kwake katika eneo la Mpiji mpakani mwa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam na watu wasiojulikana.

Watuhumiwa baada ya kufanya uvamizi huo, walimjeruhi kisha kumpora kompyuta yake ndogo aina ya HP, simu mbili na fedha taslimu Sh milioni moja.

Kamanda Kova alisema baada ya tukio hilo, polisi walifanya doria kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo, ambapo waliwatilia shaka baadhi ya wananchi ambao wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Aliongeza kuwa msako mkali unaendelea wa kuwasaka watuhumiwa wote ambao walihusika kwa namna moja ama nyingine kufanya kitendo hicho cha kinyama.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .