LOWASSA ATOA DARASA KWA SERIKALI:AWAPONGEZA MAGUFULI NA MWAKYEMBE

Posted in
No comments
Tuesday, November 5, 2013 By danielmjema.blogspot.com


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kwa mara nyingine ameibuka na kukosoa mipango ya Serikali, ambayo alisema mingi imelala kutokana na taifa kukosa viongozi wasiokuwa na ujasiri wa kuamua. Hata hivyo, alisema kuzorota kwa maendeleo nchini kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na uswahili wa baadhi ya viongozi, ambao wamekuwa wakipanga mambo mengi bila utekelezaji.
Lowassa alitoa kauli hiyo bungeni jana mjini hapa, wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2014/2015, huku akipongeza Kamati ya Bunge ya Bajeti kwamba imefanya kazi nzuri ambayo hajawahi kuiona katika kipindi cha miaka 20 aliyokaa bungeni.

Mbali ya kuipongeza kamati hiyo, ambayo inaongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, alisema Serikali inapaswa kuchagua vipaumbele muhimu ambavyo vinatekelezeka, badala ya kuwa na vipaumbele vingi visivyotekelezeka.

“Ningekuwa mimi ningeanza na kipaumbele cha ajira, huwezi kuzungumza mipango bila kuzungumza ajira, huwezi kupanga bila kuzungumza ajira.

“Tukiri kwamba kuna Watanzania wengi waliomaliza kidato cha nne, cha sita na darasa la saba, ambao hawana ajira. Tusipowaangalia watakuja kula sahani moja na sisi msipowashughulikia sasa,” alisema Lowassa.

Alitoa mfano kwa nchi ya Hispania na kusema kuwa nchi hiyo katika miaka mitatu imeweza kutoka katika matatizo ya ajira kwa sababu iliweka kipaumbele katika sekta ya ajira.

Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Mwasa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu, akisema wameweza kuchukua vijana waliomaliza chuo kikuu na kuwatafutia mashamba na trekta na kufanya kazi.

Mbali ya viongozi hao, Lowassa pia alimpongeza Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, kwa namna wanavyosimamia vizuri sekta wanazoziongoza.

Kipaumbele cha pili elimu

Akizungumzia elimu, Lowassa alitaka pawepo na mjadala wa kitaifa kuhusu suala hilo na kusema kuwa mjadala wa elimu usipuuzwe, kwani lipo tatizo la msingi katika elimu.

Lowassa alisema alitegemea kamati hiyo ingepata taarifa ya waziri mkuu iliyotolewa kuhusu elimu, ili kuangalia matatizo yaliyojitokeza, ndipo mipango ya kuondoa changamoto hizo iweze kufanywa.

Alisema kelele zinazopigwa na wananchi juu ya elimu zinapaswa kufanyiwa mjadala nchini kujua tatizo lililopo, vinginevyo Tanzania itaachwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), SADC na kubaki kuwa wababaishaji.

Kipaumbele cha tatu reli ya kati
“Namsifu sana Dk. Magufuli kwa kazi nzuri aliyoifanya, ni kazi nzuri ya ujenzi wa barabara, lakini barabara zile zimeanza kuharibika kwa kasi ya hali ya juu sana.

“Nimetoka Singida juzi zimeharibika vibaya sana, ile ya Shinyanga imeharibika vibaya kwa sababu mizigo inayopaswa kupita kwenye treni inapitishwa kwenye barabara kwa malori kuziharibu, sasa naomba muiangalie reli ya kati kwa haraka sana.

Suala la foleni Dar es Salaam
Kuhusu tatizo la msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, Lowassa alisema: “Nakupongeza sana Dk. Harrison Mwakyembe (Waziri wa Uchukuzi) kwa kazi nzuri unayoifanya, keep it up, lakini haitoshi jamani haitoshi, muda wa saa tunaoupoteza kwa foleni pale Dar es Salaam ukizipanga kwa ajili ya uzalishaji ni muda mrefu sana.

“Serikali haiwezi kukaa hivi hivi, hii ni disaster (haya ni maafa) jamani, Serikali itafute njia ya kutatua sasa, si kungoja, nasema sasa vinginevyo tunaharibu sana uchumi wa nchi.”

Hata hivyo ameipongeza Serikali kwa kuanzisha Presidential Delivery Unit, lakini akaonyesha wasiwasi wake katika utendaji kazi wa chombo hicho.“Nataka mjiulize maswali machache, je, wana meno? Tatizo la nchi hii mnazungumza mambo mengi, mnazungumza tu hakuna utekelezaji.

“Tunazungumza, lakini nidhamu ya Malaysia ni tofauti na hapa, hapa kwetu kuna uswahili mwingi wa kukaa bila kutekeleza mambo, jamani tukiamua mambo lazima yatekelezwe.

“Lazima kuwe na watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi magumu kupanga mambo yanayoweza kutekelezeka, bila kujivisha joho la kufanya uamuzi kwa utekelezaji, itakuwa ni kazi bure, ni lazima wawe na meno ya kuuma ili mkikubaliana mambo yafanyike.

“Haiwezekani katika nchi kila mtu alalamike, kiongozi analalamika, wananchi nao wanalalamika, haiwezekani tuwe sisi ni jamii ya kulalamika tu,” alisema.

Lowassa alisema ni lazima awepo mtu mmoja anayefanya maamuzi na kuchukua hatua, bila kuchukua hatua tutaendelea kulalamikiana kila siku.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
Kuhusu mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Lowassa alisema hakuna sababu ya kugombana na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda.

“Kama wao wameona kukimbilia Sudani Kusini ni jambo la msingi, sisi (Tanzania) twende East Congo (kuungana na nchi za DR Congo na Burundi) kwa sababu nako ni kuzuri zaidi, hivyo kinachohitajika ni kufufua reli ya kati,” alisema.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .