SERIKALI IMERUDISHA ZERO SEKONDARI

Posted in
No comments
Tuesday, November 5, 2013 By danielmjema.blogspot.com

SERIKALI imetangaza kurudisha daraja ziro katika elimu ya sekondari, huku
zikiwa zimepita Siku tatu, tangu uamuzi wa kufuta daraja hilo utangazwe. 

Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kelele nyingi za wadau mbalimbali wa elimu, wakipinga hatua ya kufuta ziro na badala yake lisomeke kama daraja la tano. Uamuzi wa kurudisha ziro ulitangazwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, huku mtihani wa kidato cha nne ukiwa umeanza jana.

Tamko la Mulugo limepingana wazi wazi na tamko jingine lililotolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wake, Profesa Sifueni Mchome akitangaza uamuzi wa Serikali wa kufuta ziro. Kutokana na mkanganyiko huo, Bunge limeitaka Serikali kuwasilisha kauli moja kuhusu mabadiliko ya alama za ufaulu kwa shule za sekondari, ili kuondoa utata huo.

Mulugo alitoa tamko hilo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM), ambaye alitaka kujua kama uamuzi huo wa Serikali ulilenga kuwasaidia wanafunzi wanaofeli.

Akijibu swali hilo, Mulugo alisema taarifa zilizoenea kuwa divisheni ziro imefutwa si za kweli.

“Serikali haijafuta divisheni ziro na wala hakuna divisheni V (daraja la tano), ipo divisheni I, II, III, IV na divisheni ziro kama kawaida,” alisema.

Alisema uamuzi wa kushusha madaraja uliofanywa haukuwa na lengo la kuwaokoa wanafunzi wanaofeli, bali ni kuondoa mrundikano wa alama katika daraja moja.

Alisema Serikali imeweka madaraja mapya kwa kutofautisha alama kumi kumi kutoka daraja moja kwenda jingine na kwamba hata hivyo alama za ufaulu bado ni 40 ambazo ni daraja la C.

Baada ya majibu hayo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliingilia kati na kuitaka Serikali kuwasilisha bungeni kauli moja inayoeleweka, ili kuondoa utata unaowachanganya wananchi.

“Hii taarifa unayosema waziri ni tofauti kabisa na tamko la awali lililotolewa. Haiwezekani kuwe na taarifa mbili tofauti katika Serikali moja, nendeni mkakae mje na kauli moja inayoeleweka tusiwachanganye wananchi,” alisema Makinda.

Wakati Mulugo akitoa tamko hilo, zilikuwa zimepita saa tatu tangu kiongozi huyo anukuliwe katika vyombo vya habari akitetea uamuzi wa Serikali wa kufuta ziro na kuanzisha daraja la tano.

Mulugo alifanya hivyo jana saa 1:40 asubuhi wakati akihojiwa katika kipindi cha kumepambazuka kinachorushwa na kituo cha Redio One, kinachoruka kila siku kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 4 asubuhi.

Katika kipindi hicho ambacho mada ilikuwa ni mfumo wa madaraja mapya, Mulugo aliutetea uamuzi wa Serikali wa kufuta ziro na kudai kuwa hatua ya kupunguza viwango vya ufaulu imefanyika ili kupambanua madaraja hayo.

“Elimu zaidi inahitajika kwenye suala hili la mgawanyo wa madaraja, ukweli ni kwamba kilichofanyika katika kufuta alama ya ziro ni kupambanua madaraja ya ufaulu, ni suala ambalo litasaidia elimu yetu huko mbele ya safari,” alisema Mulugo.

Awali akijibu swali la msingi la Magige, Mulugo alisema Serikali haina mpango wa kuanzisha programu maalumu hasa za ufundi kwa wanafunzi waliofeli katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.

“Kwa mwaka 2013, jumla ya wanafunzi 60,507 wa kujitegemea, wamejisajili kufanya mtihani huo, watahiniwa 3,578 wakiwemo wasichana 2,020 na wavulana 1,558 waliofeli katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana wamejisajili kurudia mtihani huo,” alisema.

Mulugo alisema Serikali imekuwa ikiongeza na kuboresha vyuo vya ufundi na kuweka mazingira rahisi kwa wanafunzi ili waweze kupata stadi mbalimbali.

“Kati ya mwaka 2010 hadi 2012, Serikali kupitia VETA imesajili jumla ya Vyuo vya Ufundi Stadi 75 sawa na asilimia 75 na asilimia 10.8 ya vyuo 618 vilivyokuwepo.

“Aidha, katika kipindi hicho, jumla ya vyuo 8 sawa na asilimia 3.2 ya vyuo 248 vilivyokuwepo vilisajiliwa na NACTE,” alisema Mulugo.

Mabadiliko hayo yameibua mjadala mkubwa, ambapo wasomi na wadau mbalimbali waliyaponda mabadiliko hayo na kudai kuwa yanaua elimu nchini.

Kwa mujibu wa wadau hao, uamuzi wa kufuta ziro sekondari ulikuwa umefanywa kisiasa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kisiasa na si kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

Walisema uamuzi wa awali ulilenga kutimiza lengo la Mpango wa Maendeleo Makubwa Sasa (BRN), ambao ni kuongeza ufaulu kwa mtihani wa kidato cha nne mwaka huu kutoka asilimia 33 mwaka jana na kufikia asilimia 60.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .