PROFESA JAY ALIPOKABIDHIWA KADI YA CHADEMA NA SUGU

Posted in
No comments
Wednesday, May 22, 2013 By danielmjema.blogspot.com


MSANII wa Muziki wa Kizazi kipya, Joseph Haule (Profesa Jay), amejiunga na Chama Cha Demokrasia na Mendeleo (Chadema).
Profesa Jay alikabidhiwa kadi ya Chadema jana mjini Dodoma katika hafla iliyomhusisha pia msanii mwingine wa Hip Hop, Kulwa Kinega, maarufu kama K wa Mapacha.
Profesa Jay alikabidhiwa kadi yake na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, wakati Kinega alikabidhiwa kadi yake na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu alipongeza hatua ya wasanii hao kujiunga na chama chake na kusema kuwa kitendo hicho ni cha historia.

“Joseph Haule baada ya kuwa nasi kwa siku nyingi, leo ameamua rasmi kuvaa gwanda. Profesa Jay Niger like me, Karibu nikukabidhi rasmi kadi yako kama waziri kivuli wa vijana,” alisema.
Kwa upande wake profesa Jay alisema hatua yake ya kujiunga na Chadema ni hitimisho la ndoto yake ya siku nyingi.
“Nimekuwa mfuasi wa Chadema kwa siku nyingi sana, lakini leo niona nijiunge rasmi. Nimefikia uamuzi huo bila kushawishiwa na mtu, nikitumia akili na uwezo wangu baada ya kuona Chadema wanataka kulitumikia taifa.
“Najivunia hii kadi na mtu yeyote akiiba, hata adandie ndege namkimbiza,” alisema huku akipigiwa makofi na baadhi ya wabunge wa Chadema.
Kwa upande wake Kinega alisema kwa muda mrefu amekuwa na wazo la kujiunga na Chadema, lakini alikuwa bado anafanya uchunguzi ili kujiridhisha.
“ Hiki ni kitu ambacho nimekuwa kikifikiria sana kwa muda mrefu, nimekuja kubaini kuwa Chadema ni mkombozi wa wasanii. Niko bega kwa bega kuona vijana wetu wanaenda mbele,” alisema.
Kwa upande wake, Sugu aliwataka wasanii hao kuelewa kuwa hakuna watakachopoteza kwa kujiunga na siasa, kwani hata yeye ni msanii ambaye uwepo wake bungeni hajaujutia.
“Huku utakuja na bado ni sehemu ya jukwaa linaloweza kukufanya uendelee kufanya unachotaka. Kama ningeambiwa nikushauri, ningesema urudi Mikumi ukawatumikie watu wako,” alisema Sugu.
Akizungumza kwa niaba ya chama, Mnyika aliwakaribisha rasmi wasanii hao katika siasa na kuwadokeza kuwa, mbele ya safari watatakiwa kutumika kuendesha jahazi la chama.
“Tukio la leo ni kubwa na linaloweza kuandika historia kwa taifa letu. Kwa yeyote aliyekuwa anafuatilia nyimbo za Profesa Jay na Anti Virus, atagundua kuwa Jay ni mtu wa mabadiliko,” alisema Mnyika.
Aliongeza: “Tunawashukuru wasanii hao kwa kujiunga nasi. Sisi wakati wote tunaamini katika kazi na kugawana majukumu, hivyo tunaamini kwamba mtakuja kupokea majukumu katika harakati za chama chetu,” alisema.
Mnyika alibainisha kuwa hatua ya wasanii hao kujiunga na Chadema ni safari ndefu iliyoanza mwaka 2005. 
Mnyika alisema yeye akiwa kiongozi wa Chadema, alikutana na Sugu ofisini kwake na baadaye Profesa Jay hotelini na kuwashawishi wote kwa pamoja waingie katika siasa.
Mnyika alisema imemchukua Sugu miaka mitano kufanya maamuzi na leo hii ni Mbunge wa Mbeya Mjini, wakati Profesa Jay imemchukua miaka saba kufikia uwamuzi wa kujiunga na chama hicho,” alisema.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .