MAMA ALIYEJIFUNGUA "MAPACHA WANNE" KCMC AOMBA MSAADA
Posted in
No comments
Monday, September 23, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
MWANAMKE aliyejifungua mapacha wanne katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ameiomba Jamii ya Watanzania kumsaidia fedha za kugharamia malezi ya watoto hao kutokana na hali yake kiuchumi kumuwia vigumu kuwapa watoto hao malezi stahili.
Mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Nipa Mrutu (36), mkazi wa kijiji cha Kavambugu, Kata ya Same mjini, wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, alilazwa katika hospitali hiyo, Agosti 3 na kujifungua watoto wanne kwa njia ya Upasuaji Septemba 10 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika wodi ya kina Mama hospitalini hapo, Mrutu ambaye ni Mkulima na mama wa Watoto saba pamoja na uzao huo, alisema kuwa kutokana na hali yake kiuchumi kuwa duni hatoweza kugharamia mahitaji ya malezi ya wanae.
Alisema kwa hivi sasa, ukiacha gharama za kuwalea watoto hao pia anadaiwa Hospitalini hapo fedha ambazo ni nyingi sana na hivyo anatoa wito kwa yeyote yule atakayeguswa na hali yake kumsaidia chochote kitakacho mwezesha kukidhi mahitaji ya watoto hao.
“Namshukuru Mungu nimejifungua salama, lakini kwa kweli sijui hawa wanangu nitawaleaje, mimi ni mkulima, kipato changu pamoja na mume wangu hakituwezeshi kuwalea watoto wetu, tangu Tarehe 3 mwezi wa nane niko hapa, bili ni kubwa mno,” alisema Mrutu.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya akina Mama katika Hospitali ya KCMC, Dkt. Gileard Masenga alisema kuwa baada ya kumfanyia mwanamke huyo uchunguzi wa Kitabibu, walilazimika kumzalisha Septemba 10 ikiwa ni wiki 34 tu za ujauzito wake.
Dkt. Masenga alisema kitaalam, inatakiwa mwanamke abebe mimba kwa muda wa wiki 40 lakini kutokana na Mgonjwa wao kuonekana kuwa na shinikizo la Damu Uongozi wa Hospitali iliamua
afanyiwe upasuaji kuokoa maisha ya viumbe vilivyoko tumboni.
Alisema katika taarifa za madaktari, afya ya mwanamke huyo ilionekana kuzorota kutokana na shinikizo la damu lililokuwa likimsumbua kuongezeka mara kwa mara hali ambayo iliwalazimu kumpa dawa maalum kwa ajili ya kuboresha afya ya Mama na watoto.
“Kitaalam inatakiwa Mama mjamzito ajifungue baada ya wiki 37 kwani hapo mapafu ya mtoto yanakuwa yamekomaa, hali ilikuwa tofauti kwa mgonjwa wetu, Presha yake ilikuwa inapanda kila kukicha hivyo tukaamua kumpa dawa maalum ambayo itasaidia kukomaza mapafu ya watoto”, alisema Dkt. Masenga.
Kuhusu hali ya Watoto hao kiafya Dkt. Masenga alisema watoto hao ambao watatu ni wa kiume na mmoja ni wa kike, walizaliwa na uzito wa kilogramu 1.5, wa pili 1.6 watatu ambaye ni wa kike ana 1.8 huku wanne akiwa na uzito wa kilogramu 1.6 wana afya nzuri japo kwa sasa wako
katika uangalizi wa madaktari.
Alisema kutokana na uzito wao kutofikia uzito unaotakiwa wa kilogramu angalau 2.5 au zaidi, wameamua kuwaweka katika wodi maalum na kuwatenga na Mama yao hadi hapo uzito wao utakapoimarika huku akibainisha kuwa hiyo ni salama kwao kutokana na magonjwa ya
maambukizi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi, aliyefika Hopitalini hapo Juzi kumjulia hali Mama huyo na wanaye wanne, alisema tayari serikali ya Wilaya ya Same imeshaanza kufanya utaratibu wa kuhakikisha Mama huyo anapata msaada.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :