MWAKA MMOJA YA KIFO CHA DAUDI MWANGOSI, WANAHABARI KILIMANJARO WAUNGANA NA WENZAO NCHI NZIMA KUMKUMBUKA; WATOA TAMKO KALI!!

Posted in
No comments
Monday, September 2, 2013 By danielmjema.blogspot.com


Ni mwaka mmoja tangu marehemu Mwangosi auawe kwa kupigwa bomu na mtu anayedhaniwa askari wa kikosi cha kutuliza ghasia( FFU),Sept 2,2012 katika kijiji cha Nyololo mkoani Iringa, marehemu alikufa akiwa analitumikia taifa kwa kutumia taaluma yake ya habari.

Tayari mtuhumiwa wa mauaji hayo amefikishwa mahakamani na kesi ipo katika hatua ya kutajwa,hatuna nafasi ya kuijadili zaidi bali kusubiri sheria ifuate mkondo wake.
Ikiwa ni mwaka mmoja leo tangu mwenzetu atangulie mbele ya haki, Klabu ya wanahabari mkoani Kilimanjaro(MECKI) inaungana na wanahabari wote nchini,kuendelea kutoa pole kwa familia ya Mwangosi na IPC iliyopoteza kiongozi shujaa,

pia tunalaani matukio yote yanayofanywa na baadhi ya vyombo vya dola na taasisi katika kunyima uhuru wa kupata habari na kudhoofisha kwa namna moja au nyingine juhudi za wanahabari katika kutekeleza majukumu yao.

Klabu inapenda kuwakumbusha wadau wa habari na taasisi za serikali kurejea kauli ya rais Jakaya kikwete ya kutaka taasisi za umma kutoa ushirikiano kwa wanahabari lakini pia kutangaza shughuli zao.

Kadhalika klabu inapongeza baadhi ya wadau ambao wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa wanahabari hususani mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Leonidas Gama ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono kazi ya wanahabari.

Pamoja na yale ya wadau, Klabu inatoa wito kwa vyombo vya habari kujali maslahi ya wanahabari,kwa kuhakikisha wanalipwa vizuri stahili zao lakini pia wanapata vitendea kazi ili kutekeleza wajibu wao kulingana na matakwa ya kitaaluma.

Ikumbukwe mwandishi dhaifu kitaaluma na vitendea kazi anakuwa mtumwa mbele ya mdau mwenye maslahi binafsi.

Tafiti za Umoja wa vilabu vya wanahabari nchini(UTPC) zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wanahabari nchini hawajaajiriwa na wanafanyakazi zao katika mazingira yasiyo ridhisha.

Mecki kwa kutambua changamoto zinazowakumba wanachama wake na wanahabari kwa ujumla, ipo katika hatua za mwisho za mchakato wa kuboresha utendaji kazi wa wanachama wake katika mpango ambao utatangazwa hivi karibuni.

Aidha Klabu inatoa wito kwa wanachama wake kutosita kutoa taarifa za kuzuiwa kutekeleza wajibu wao unofanywa na taasisi yoyote au kiongozi yeyote ama kudhalilishwa kwa mwanahabari pale anapokuwa akifanya kazi yake ya kitaaluma.Hata hivyo wanahabari nao wanapaswa kuzingatia maadili ya taaluma yao.

Ili kuendeleza mahusiano mazuri baina ya wanahabari na wadau na kuepuka kupelekana mahakamani,ambapo mara zote huendelea kujenga mpasuko kati ya aliyeshinda na aliyeshindwa, klabu imeunda kamati ya maadili na usuluhishi yenye wajumbe watano,chini ya uenyekiti wake, Japhary Ali ambaye ni wakili wa kujitegemea na afisa mtendaji utawala wa kiwanda cha sukari TPC. Wadau wanapaswa kuwasilisha malalamiko yao mara wanapobaini wanahabari wamekiuka maadili.

Naomba kuwasilisha.

Rodrick Makundi
Mwenyekiti MECKI.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .