RASIMU YA SERIKALI TATU ZENYE MARAIS WATATU NI MWISHO WA MUUNGANO
Posted in
No comments
Monday, August 26, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) ofisini kwake |
Ni kweli Muungano ni dhamira ya dhati ya wanaoungana na kwa Muungano wetu ni dhamira ya Watanzania wote, dhamira ya dhati ya kuudumisha muungano ni ile ambayo inakubalika na inaendana na Matakwa ya walio wengi.
Mwal.Leonidas Gama-Rc Kilimanjaro |
Kwa mazingira ya nchi yetu na mazingira ya kibinadamu, sio rahisi katika Taifa kama hili lenye watu zaidi ya milioni arobaini, tukawa na
dhamira moja, tutajiridhisha kinadharia tu kuwa Muungano utadumu kwa vile tuna
dhamira nao, huku ni kujidanganya. Ni
dhahiri kuwa ikitokea katika mfumo huu wa serikali tatu, tukapata kiongozi mkuu,
ama chama, ama chombo chenye mamlaka ya kutunga sheria, ama kundi la watu
ambalo dhamira yao
ni tofauti na dhamira ya wengi.
Ni
wazi kuwa pamoja na dhamira nzuri ya walio wengi wa kudumisha Muungano wa sasa,
Muungano utavunjika kwa matakwa ya mamlaka iliyopo. Kwa maoni yangu Dhamira ya Watanzania katika kudumisha Muungano ni sehemu tu ya kuimarisha na sio suluhisho la kudumu kwa Muungano.
Muundo madhubuti unaozuia fursa ya
kuvunja Muungano ndio suluhisho sahihi na la kudumu kwa Muungano. Ni vyema Watanzania tusisahau yale ya mwaka
1977, tulikuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, wote wana Afrika Mashariki
tuliipenda Jumuiya yetu, tulikuwa na dhamira ya dhati ya kuidumisha.
Lakini alitokea mtu mmoja tu kwa matakwa yake, na
akili zake alizoziona zinafaa alisababisha Jumuiya ya Afrika Mashariki
kuvunjika sembuse Muungano wa Serikali tatu?
Waasisi
wa Taifa letu, Hayati Abeid Amani wa Zanzibar na
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika,
karume walipoanzisha Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar
hawakukurupuka, walikuwa na sababu za msingi za kuunganisha nchi mbili hizi.
Miongoni
mwa sababu hizo ni pamoja na Undugu wa damu uliopo kati ya Wananchi wa Zanzibar na Tanganyika na pili ni sababu za kiulinzi na usalama kwa nchi hizi wa mali, rasilimali na watu wake, ninaamini kuwa, sababu hizi bado ni hai
hadi sasa na ni sababu muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.
Watanzania
hivi sasa kupitia mabaraza mbalimbali wanaendelea kutoa na kukusanya maoni juu ya katiba. wapo
wanaopita huku na huko na wale wanaotumia njia mbalimbali za kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba
na hasa eneo hili la muundo wa serikali tatu.
Ni
uhuru wa kila mtu kutoa maoni yake, lakini kuna haja ya Watanzania kuwa na
tahadhari sana, wapo wanaojua fika kuwa kuwepo kwa serikali tatu, zenye
Marais watatu katika nchi yenye mamlaka tatu, ni kuuvunja Muungano.
Hivyo wapo wanaoshabikia serikali tatu, si kwa kuimarisha
Muungano ila wanajua kuwa ni kuuvunja Muungano. Wanachelea kuonyesha dhamira yao ya kuuvunja
Muungano bali wanashabikia Serikali tatu kwa kujua dhamira yao itatimia.Watanzania tutafakari, tuchukue Hatua
Pamoja na Sababu nyingine nyingi unazoweza kuzichambua juu ya kudumu au kutokudumu kwa Muungano wa Serikali tatu, nimeona ni vyema nipitie maeneo ambayo binafsi nimeona yanaweza kuchochea kuunjwa kwa Muungano wa serikali tatu.
Wengine
wanajadili hoja ya gharama kubwa za kuendesha serikali tatu, kwangu hili si hoja,
naamini jambo lolote la kheri linahitaji gharama na kama gharama zinaweza kuhimilika,
hilo si tatizo.Maeneo yanayoweza kuvunja muungano ni pamoja na:
(i)Uwezo uliosawa ki-uwiano katika kuchangia uendeshaji wa Muungano
katika ibara ya 215 ya Rasimu, inazungumzia vyanzo vya mapato ya serikali ya Jamhuri ya Muungano,
na moja kati yake ni "mchango kutoka kwa washirika wa Muungano" maana yake ni
mchango toka serikali ya Zanzibar na kutoka ya Tanzania bara.
Ni
dhahiri muundo na mfumo wa uendeshaji wa serikali ya Muungano kiasi kikubwa utategemea
mchango huu ambao unategemea uchumi wa serikali mbili zinazounda Muungano,
katika mazingira halisi ya Tanzania
kwa kuzingatia rasilimali na mali
zilizopo katika maeneo ya Muungano yaani Tanzania Bara na Zanzibar ni dhahiri hayatawezesha mchango ulio sawa ki-uwiano katika kuendesha serikali ya Muungano, hii itaifanya Serikali yenye mazingira mazuri ya mali na rasilimali, kulazimika kuiendesha/kuichangia Serikali ya Jamhuri ya Muungano na nyingine kushindwa kuchangia katika hali yoyote ile, mgongano wa kiuchumi na kimaslahi hautaepukika.
Lakini pia katika mazingira ya umoja na mshikamano uliopo sasa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo ushirikiano katika uendeshaji wa shughuli za kiserikali ni ule usioepukika, (Gharama za uendeshaji na huduma katika serikali kwa mfano- Umeme , Mafuta n.k.)
Hali hiyo katika serikali tatu, haitapata nafasi, serikali itakayochangia zaidi tofauti na nyingine haitakubali hali hiyo. kwa maana ya kiuchumi, pia upo uwezekano wa serikali itakayoshindwa kujiendesha au hata kuchangia, kukopa nje katika mazingira ya kupoteza uhuru wake wa kiuchumi na kiusalama.
Tukumbuke kuwa hadi sasa bado waptu nje ya nchi wanaoitazama Zanzibar kisiwa chetu kizuri kama eneo lao, na bado wanandoto kuwa siku moja watarudi Zanzibar kiutawala.Jee iwapo Zanzibar itashindwa kuchangia katika serikali ya Muungano na kujiendesha kiuchumi ni nini kitatokea?
Ni
lazima tukubali Watanzania kuwa uchumi wa nchi hizi unatofautiana sana na
kuishi kwetu katika Muungano ni kule kwa kushirikiana kindugu kunakotokana pia
na mfumo uliopo wa Muungano, vinginevyo kwa muundo wa serikali tatu, zenye Marais
watatu, hili linalofanyika sasa halina nafasizi, ni wazi kuwa nafasi ya kudumu kwa Muungano itakuwa matatani.
(ii) Mgawanyo wa madaraka na mfumo wa kiutawala
Kwa
mujibu wa Rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutakuwa na Marais
watatu na serikali tatu na kwa mujibu wa madaraka na mamlaka, kila Rais atakuwa
na madaraka katika eneo lake la utawala.
Katika
mfumo wa miliki za mali na rasilimali na utawala wa mali na rasilimali za nchi,
kwa sehemu kubwa utakuwa katika mamlaka za serikali ya Zanzibar kwa eneo la Zanzibar
na Tanzania bara kwa yaliyo chini ya Tanzania bara.
Hii ni pamoja na utawala wa serikali, serikali za mitaa, tawala za mikoa na uteuzi wa mamlaka za utendaji, Ardhi, Maji, Barabara, Huduma za kijamii ikiwemo Elimu, Afya n.k.
Kiutawala
Rais wa Jamhuri ya Muungano hatakuwa na eneo la utawala kirasilimali hasa
rasilimali watu, Rais wa Muungano hatakuwa na mamlaka na madaraka za
kiutendaji, rasilimali na huduma za kijamii na za maendeleo, mamlaka za kuagiza
wala kukemea.
Katika
hali hii utendaji kazi wa Rais wa Muungano ambaye ndiye Kiongozi Mkuu,
hautakuwa wenye mamlaka na madaraka. Uwepo wa mgongano wa kimadaraka kati ya
Jamhuri ya Muungano na serikali ya Zanzibar na
ile ya Tanzania
bara hautazuilika. Na ni ukweli Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Boya, ataelea hewani.
(iii) Mfumo wa utawala na Vyama vingi vya siasa
Kwa
mujibu wa sura ya kwanza ya Ibara ya 1 (2) ya Rasimu ya Katiba, Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
ni shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Kwa mtazamo wangu; katika mfumo wa kidemokrasia unaozingatia vyama vingi vya siasa, ni dhahiri kuwa utawala na
mamlaka za utawala zinaweza kuwa katika matokeo ya mchanganyiko mkubwa wa Vyama
mbalimbali vya kisiasa, matokeo ya chaguzi za Rais, wabunge na Madiwani
zinaweza kutoa sura tofauti na katika maeneo tofauti.
Ni ukweli kuwa kila chama cha siasa, kina mfumo wake na malengo yake, kisiasa tunaamini nchi ni moja, na wote tunajenga nyumba moja kwa hiyo tofauti zetu za kisasa zisivuruge umoja na mshikamano wetu. Kwa nadharai ya kisiasa, hii ni sahihi, lakini kihalisia ni dhana isiyotakiwa kuiamini.
Upo uwezekano wa chaguzi katika serikali tatu, zikapata vyama vinavyoongoza serikali kwa tofauti kwa kila eneo la utawala: kwa mfano serikali ya Jamhuri ya Muungano ikaongozwa na chama kingine, Serikali ya Zanzibar ikaongozwa na chama kingine na ile ya Tanzanzia Bara inkaongozwa pia na chama kingine.
Kwa
vyovyote vile mamlaka na madaraka yatawataka Marais wa Bara na yule wa Zanzibar
kutii mamlaka ya Rais wa Muungano. Ni rahisi sana kusema hakuna tatizo
lolote, wataongozwa na Katiba lakini yeyote anayejua mwenendo wa siasa za Tanzania hivi
sasa na matarajio za siasa za baadae zinazoendelea hapa nchini, kwa tofauti ya sera, itikadi na mitazamo ya kimaslahi katika vyama vyetu na jamii kwa ujumla.
Kwa mtazamo wa yeyote yule ni kuwa Muungano huu wa serikali tatu, wenye Marais watatu ni ndoto kuamini kuwa utadumu katika mazingira ya utawala wa vyama tofauti katika serikali zilizopo.
Tukumbuke
Historia ya Muungano iliyoundwa kwa utaratibu unaofanana na huu ambao umeishia kusambaratika kama vile Muungano wa iliyokuwa Yugoslavia
na Usavieti. Katika
Yugoslavia, jimbo la Albania, ndilo lilikuwa la kwanza kutaka kujitenga
na hatimaye kulitumbukiza Taifa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe huku na
majimbo mengine kama Serbia
na Montenegro
yakidai kujitawala; hatima na matokeo ya Muungano huo ni Kuvunjika kwa Muungano wao.
Zipo nchi nyingi zimesambaratika kutokana na mifarakano midogo
midogo ya kijamii: kumbuka Ethiopia,
Eritrea, Somalia, Sudani na Sudani ya Kusini n.k
"Mimi bado naamini
kuwa suluhisho la kero la Muungano siyo kuwa na serikali tatu, bado tunao uwezo
na nafasi kubwa ya mjadala zaidi.Tujiulize
ni nchi gani duniani yenye Marais wa watatu, wenye serikali tatu na wakakaa
katika mfumo huu wa Muungano wakafanikiwa?
Marekani
haijagawa mamlaka, madaraka, usimazi, utawala na maamuzi kwa mtu zaidi ya mmoja
na ndio maana Taifa la Marekani linaendelea kuwa imara sio ndani tu bali hata
nje ya mipaka yake.
Watanzania
wa Bara na Visiwani, kama tunadhamiria kweli kujenga umoja wa kitaifa kwa mfumo
wa Serikali tatu tungekuwa na Serikali zenye muundo huu; Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania yenye Rais aliyechaguliwa na Watanzania wote.
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar
yenye Waziri Mkuu mtendaji aliyechaguliwa na Bunge la Jamhuri Serikali ya
Tanzania Bara aliyechaguliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Hili
ndilo suluhisho pekee kwa wale wanaotaka Serikali tatu, lakini nina hakika kwa
sababu za tulio wengi kutawaliwa na homa ya madaraka, wazo hili wengi
watalipuuzia bila kujali kuwa ndilo suluhisho.
Tujiulize
ni kweli tunautaka Muungano au tunasema tunaimarisha Muungano kumbe dhamira
zetu zinataka tuone Muungano unakufa kwa vile eti kwa nini Zanzibar
wana bendera yao, wana wimbo wao wa Taifa, wana
madai yao kila
kukicha.
Watanzania
wenzangu, Muungano unaondoka, chozi la Baba wa Taifa litatushukia. Kuna tafsiri
fulani nimesikia zikitolewa na wale wanaotetea muundo wa serikali tatu, Jaji
Warioba na kundi lake
katika tafsiri zao
nimesikia wakimnukuu Baba wa Taifa kupendekeza serikali tatu.
Tuache
kutafsiri na kupindisha maneno ya Baba wa Taifa kwa kile tunachokitaka sisi,
maana wapo wanaotumia maandishi mbalimbali ya Baba wa Taifa, kumpandikizia
tafsiri ya kutaka serikali tatu kwa matakwa yao.
Baba
wa Taifa amefariki akiamini na akiwa na msimamo mmoja tu “Muungano wa Serikali
mbili kuelekea serikali moja”. Mwanamapinduzi Mzee Abeid Amani Karume amefariki
akiamini juu ya Tanzania
yenye Muungano wa Serikali moja.
Mungu
Ibariki Muungano wetu. Mungu ibariki Tanzania.
Makala hii imeandaliwa na Mwalimu Leonidas T. Gama
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
haya ni Mawazo binafsi na Mapendekezo yangu!
Mwisho…
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :