TANAPA KWA KUSHIRIKIANA NA MWEKA WILDLIFE WANAFIKIRIA KUBALISHA MTAALA WA KUFUNDISHA WAONGOZA WATALII KATIKA MLIMA KILIMANJARO

Posted in
No comments
Sunday, November 17, 2013 By danielmjema.blogspot.com

ALLAN KIJAZI
SHIRIKA la hifadhi za Taifa(TANAPA) kwa kushirikiana na chuo cha uhifadhi na usimamizi wa wanyapori Mweka,wanafanya utafiti ili kupata  mitaala ya kufundishia waongozaji watalii katika mlima Kilimanjaro ili taaluma hiyo kutambulika kitaifa na kimataifa.


Lengo la utafiti huo ni kuifanya taaluma ya waongoza na utoaji huduma kwa watalii kuwa rasmi,lakini pia kufanywa kwa ubora unaokubalika,kwani kazi hiyo ikiboreshwa ni moja wapo ya sifa nzuri zitakazolitangaza taifa,kulingana na ubora wa huduma wanazopata watalii.

Mkurugenzi mkuu wa TANAPA, Allan Kijazi alisema hayo wakati akifungua mkutano mkuu wa pili wa mwaka wa chama cha waongoza watali mkoani Kilimanjaro (KGA) uliofanyika jana mjini Moshi ambapo pia walieleza changamoto inayowakabili ikiwamo kutokuwa na mfumo rasmi wa malipo.

“Hii ni biashara ya ushindani baina ya kampuni moja na nyingine, lakini nchi moja na nyingine,watalii wakibaini kwamba wakija nchini mwetu watapata huduma bora zinazokubalika kimataifa, itakuwa ni sehemu ya kukuza Zaidi sekta ya utalii”alisema.

Alisema kwa sasa taaluma hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo kila chuo kuwa na mtaala wake ambao haufanani na mahali pengine jambo linalotia shaka kuhusu kiwango kinachotolewa na ubora wa waongoza watalii watakaofanya kazi hiyo.

Kuhusu suala la mfumo wa malipo kwa waongoza watalii, Kijazi alisema sharia inazuia kwa mamlaka kuingilia mikataba binafsi ya kampuni za utalii ingawa jambo hilo linafahamika na kwamba tayari liliwasilishwa idara ya kazi ili kutazama namna sahihi ya kusaidia kutendeka kwa haki.

Akizungumzia suala la kukabiliana na ujangili,mkurugenzi huyo alisema TANAPA imejipanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kudhibiti vitendo hivyo lakini akataka waongoza watalii kwa ujumla nao kusaidia kukomesha vitendo hivyo.

Naye Mwenyekiti wa KGA,  Respius Baitwa, alisema wanakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kulipwa malipo duni yanayosababisha ugumu wa maisha lakini pia kushindwa kujiendeleza kitaaluma kutokana na ukosefu wa fedha.

Kutokana na hilo waliomba serikali kutoa mwongozo wa malipo hayo ili kudhibiti tabia ya baadhi ya kampuni za utalii kujineemesha huku wakisababisha waongoza watalii kutumia mbinu zisizokubalika ili kujipatia kipato.

Aidha mwenyekiti huyo aliomba  TANAPA kuwapa elimu ili kuwawezesha kufahamu sharia za uhifadhi jambo ambalo litasaidia kukabiliana na vitendo vya ujangili.

Mwisho.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .