MIGOGORO YA ARDHI YASHIKA KASI HANDENI;WANANCHI WALAOLAMIKA KUPORWA ARDHI HANDENI
Posted in
Mazingira
No comments
Saturday, March 29, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
Na Mwandishi wetu, Aliyekuwa Handeni
WANANCHI wa Kijiji cha Komsala,
wilayani Handeni, mkoani Tanga, wamemlalamikia mwekezaji anayejulikana kwa jina
la Amina Singa, kuwa anapora ardhi zao, huku serikali ya Kata Kwamatuku,
ikishindwa kuwatetea wakulima wadogo na kuelemea upande wa mwekezaji.
Katibu wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, Nassib Bakari, pichani.
Mwandishi wa habari hizi alitembelea katika kijiji
hicho na kufanya mazungumzo na wananchi sambamba na Baraza la Kata juu ya mgogoro
huo unaosababisha malalamiko mengi kutoka kwa wakulima hao.
Mjumbe wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, Mwanahamisi Nyata, pichani.
Akizungumza kwa huzuni kubwa,
mkulima aliyejitambulisha kwa jina la Hausi Zuberi, alisema kuwa mwekezaji huyo
amechota eneo lake, kama alivyofanya hivyo kwa wananchi wengine waliopakana na
shamba lake.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu pichani.
Alisema hali hiyo imewafanya waishi
kwa mashaka wakiamini kuwa ataendelea na tabia yake hiyo, licha ya kumiliki
eneo zaidi ya heka 120 hali ya kuwa anashindwa kulilima.
Hausi Zuberi, mmoja wa walalamikaji wa migogoro ya ardhi katika Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga.
“Mwekezaji huyu ni kero kubwa kwetu
kwasababu amechota maeneo yetu wakulima tusiopungua 6 baada ya kuvuka mbele ya
mpaka wake, hali inayotufanya tuishi kwa hofu tukiamini kuwa ataendelea
kutupora,” alisema.
Naye Paulina Athon Simbaulanga,
alisema kuwa uporaji huo umebarikiwa na Baraza la Kata, baada ya kutembelea
eneo hilo, jambo linalowafanya waamini kuwa kuna njia ya mkato iliyopitwa
katika kufanikisha uporaji huo.
“Amina alikuja kijijini kwetu na
kuomba heka 60, lakini sasa ana heka 120 na bado anapora sisi tusiokuwa na hata
heka 5, licha ya yeye kumiliki eneo kubwa.
“Hatujui hizo heka nyingine
amezipata vipi na sheria za ardhi zinasemaje katika hilo, ingawa serikali ya
kijiji inajua na mgogoro huu umebarikiwa na viongozi wetu,” alisema.
Alipotafutwa Amina, alisema hawezi
kuzungumzia suala hilo kwakuwa wananchi hao ndio waliovamia shamba lake, licha
ya kushindwa kusema ni kiasi gani cha shamba analomiliki kijijini hapo kutoka
heka 50 zinazotakiwa kisheria.
“Kwanza mtakuwa umefanya makosa kama
mmeamua kufanya mazungumzo na wananchi hao kabla yangu, hivyo siwezi kusema
lolote,” alisema Amina.
Katibu wa Baraza la Kata ya
Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga, Nassibu Bakari Bigo, alikiri
kuupokea mgogoro huo wa Amina na wakulima wa kijiji cha Komsala, huku akisema
kesi za aina hiyo zimeendelea kushamiri katika maeneo mengi katika Kata hiyo.
“Tuliupokea mgogoro huo, lakini kwa
kiasi kikubwa umechangiwa na serikali ya kijiji husika kwa kushindwa kutatua
kesi hizo na watu kusaka haki yao Baraza la Kata,” alisema Bakari.
Kwa mujibu wa Bakari, kesi za
migogoro ya ardhi zimeshamiri katika eneo lao, hivyo viongozi wa vijiji
wanapaswa kusimamia vyema sheria za ardhi, huku wakitoa elimu kwa wakulima na
wananchi wao, wakiwamo walalamikaji wa kesi inayomhusisha Amina, kutokana na
mashahidi wao kushindwa kufika walipoitwa na Baraza la Kata.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :