RAIS KIKWETE AVURUGA BUNGE LA KATIBA; APINGA SERIKALI TATU

Posted in
No comments
Saturday, March 22, 2014 By danielmjema.blogspot.com


Rais Jakaya Kikwete jana alibadili upepo wa mchakato mzima wa Katiba baada ya kutoa maoni yake binafsi, akitaka muundo wa Serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza katika ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Rais Kikwete alipangua hoja moja baada ya nyingine zilizotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba wakati akiwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni Machi 18, mwaka huu.
Katika hotuba yake hiyo ya saa 2:49 iliyokuwa na maneno ya ‘kuuma na kupuliza’ kuhusu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba, Rais Kikwete alisema  suala la muundo wa Muungano ndiyo ajenda mama katika Rasimu ya Katiba na kwamba iwapo wajumbe watatoa uamuzi usio sahihi, nchi inaweza kujaa migogoro ambayo haikuwapo.
Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo, Kikwete alisema kuwa wanaotaka Serikali tatu waangalie changamoto zake na kuzitafutia majibu, kwa maelezo kuwa muundo huo unaweza kuvunjika kirahisi.
Alisema ingawa Jaji Warioba aliwatoa hofu wananchi kuwa Serikali tatu hazitakuwa na gharama kubwa, ukweli ni kwamba muundo huo una gharama na utekelezaji wake ni mgumu na kusisitiza kuwa CCM inaweza kuzimaliza kero za Muungano bila kuhitaji uwapo wa Serikali ya tatu.
Huku akichambua kile kilichoelezwa na Jaji Warioba sambamba na kuwapiga vijembe wenyeviti wa vyama vya upinzani akiwamo Christopher Mtikila (DP) na Freeman Mbowe (Chadema), Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa sababu mbili kubwa  za kupendekeza muundo wa Serikali tatu;
“Sababu ya kwanza ni kwamba muundo huo ndiyo matakwa ya Watanzania wengi Bara na Zanzibar.  Sababu ya pili muundo huo unatoa majibu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazolalamikiwa na pande zote mbili.”
Aliongeza, “Wapo wanaokubaliana na tume na kwamba muundo wa Serikali tatu ni matakwa ya wengi na hauepukiki na kwa msemo wa Kiswahili wengi wape. Lakini wapo wanaopingana na takwimu za tume kwamba hazionyeshi ukweli huo. Mimi nasema maneno yanayosemwa na watu siyo yangu.”

Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo alisema, “Watu wanasema Watanzania waliotoa  maoni kwa tume ni 351,664, kati yao 47,820 sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano. Watu 303,844 sawa na asilimia 86.4 hawakuwa na tatizo na muundo wa Muungano na wala hawakuuzungumzia wakati wa kutoa maoni.”
Alisema hivi sasa watu wanahoji iweje asilimia 13.6 ndiyo wageuke Watanzania walio wengi ambao wametoa maoni ya kutaka Serikali tatu.
“Watu wanahoji mbona taarifa ya tume inayohusu takwimu (ukurasa 66,67), inaonyesha kati ya watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu muungano watu 17,280 ndiyo waliotaka Serikali tatu ambao ni sawa na asilimia 37.2 na waliotaka muundo wa Serikali mbili ni asilimia 29.8, Serikali ya mkataba asilimia 25.3 na Serikali moja asilimia 7.7” alisema. Alisema taarifa ya tume inaonyesha kuwa watu 772,211 waliotoa maoni ni asilimia 10.4 ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hawakuzungumzia Muungano, bali mambo mengine.
“Watu wanahoji kama Muungano ni jambo linalowakera sana Watanzania ingethibitika kwenye wingi wa wale waliotoa hoja. Usahihi wa hoja hii ni upi, nawaachie nyie (wajumbe) mjadili” alisema huku akishangiliwa kwa nguvu.
Akizungumzia sababu ya pili ya tume kwamba muundo wa Serikali tatu unajibu changamoto za muundo wa Serikali mbili, huku akifafanua kero zinazotolewa na kila upande wa Muungano alisema; “Nyinyi ndiyo waamuzi, sikilizeni vizuri hoja hizi mtafakari na kuamua. Tume yenyewe imekiri kuwa muundo wa Serikali wa Serikali tatu una changamoto zake ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma.”


APINGA SERIKALI TATU

Katika hotuba yake, Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, alionekana kufanya kampeni ya wazi kutetea mfumo wa serikali mbili unaopiganiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akitumia muda mrefu kujaribu kuonyesha ‘ubaya’ wa mfumo wa serikali tatu.

Akihutubia Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Rais Kikwete alitumia muda mrefu kutisha wasikilizaji wake kuwa serikali tatu zitavunja muungano, na kusema, “ni uamuzi ambao tutaujutia.” Alitumia mifano mingi kuonyesha kwamba mapendekezo ya Tume ya Warioba hayatekelezeki, huku akidai “mtu wa Mungu” alimshauri kukataa mfumo wa serikali tatu.

Huku akisingizia wajumbe kwamba wao ndio waamuzi, Rais Kikwete alitoa hotuba elekezi na kuweka msimamo wake huku akimtaja Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba mara kwa mara, na akishangiliwa na wajumbe wa CCM walio katika Bunge hilo.Tayari CCM imeweka msimamo kuwa inatetea serikali mbili, licha ya Tume kutoa uchambuzi unaoonyesha kuwa wananchi walio wengi wanataka mfumo wa serikali tatu.

Katika hotuba yake ya jana, ilionekana kwamba rais aliandaa hotuba hiyo baada ya kusikiliza hotuba ya Warioba, jambo linalothibitisha mkakati wa CCM waliofanya kwa kumtumia Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge la Maalumu la Katiba, kutengua kanuni ili Warioba aanze, Kikwete afuate. Msimamo wa JK unaweza kuleta utata kwa kuwa amesisitiza mfumo unaoungwa mkono na chache, huku akipuuza uchambuzi uliofanywa na Tume na kuungwa mkono na wananchi.
 
Iwapo hoja yake itaathiri maoni ya wajumbe na kuzua mtafaruku wa kijamii, Rais Kikwete atakuwa amepuuza ushauri uliotolewa jana na Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Kenya, Moses Wako, aliyeonya kuwa iwapo watachakachua mchakato wanaweza kuleta msukosuko wa kitaifa kama ilivyotokea Kenya mwaka 2007. Huku akisisitiza kwamba wajumbe wawe na kauli mbiu ya Tanzania Kwanza, yeye binafsi alitumia muda mefu kusisitiza msimamo wa chama chake.

Alianza kama vile aanauma na kupuliza, akiwaambia wajumbe kuwa wao ndio waamuzi, lakini kuelekea mwisho wa hotuba yake, alionekana kupambana na msimamo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba uliowasilishwa na Jaji Warioba wakati akiwasilisha Rasimu ya Pili ya Katika kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Wakati Jaji Joseph Warioba alihutubia Bunge Jumanne wiki hii akisisitiza kuwa “serikali tatu hazikwepeki,” jana Rais Kikwete aliliambia Bunge lile lile kuwa “serikali tatu haziwezekani.”

Wakati hotuba ya Warioba ilijikita katika kuchambua faida na hasara ya kila mfumo uliopendekezwa kwenye tume, Rais Kikwete alielekeza nguvu zote katika kuonyesha changamoto za serikali ya tatu, huku akionyesha kuwa changamoto za serikali mbili ni nyepesi.

“Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki hiyo Tanzania Bara.  Na wao vilevile wananung’unikia mkanganyiko kuhusu ugawaji wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.  Hizi ndizo baadhi ya changamoto ambazo Tume inaona jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa,” alisema.

Huku Warioba akisisitiza kuwa baada ya kukusanya maoni ya wananchi waliyafanyia uchambuzi wa kina ili kupata uhalali wake kabla ya kutoa uamuzi, rais Kikwete, kana kwamba anapotosha hoja ya Tume, alijielekeza tu katika idadi ya waliotoa maoni, akisema:

“Kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa.  Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote.  Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?”

Siku moja kabla ya Rais Kikwete kuhutubia Bunge, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alizungumza na vyombo vya habari kusisitiza msimamo wa chama chake wa serikali mbili. Kwa muda wa dakika 260, Rais Kikwete alijiegemeza katika madhara ya muundo wa serikali tatu unaopendekezwa katika Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Pamoja na kusifu kazi nzuri ya tume ya Warioba, Rais alisema kuwa mapendekezo yao kwa dhana mpya kama muundo wa serikali tatu yanatia hofu namna itakavyojiendesha.

“Sisi tunaotoka kwenye CCM, tunasema kuwa mambo haya yanaweza kumalizwa bila kuwa na serikali tatu,” alisema Kikwete na kushangiliwa na wajumbe wa chama chake. Alisema serikali tatu ina gharama na kwamba haitakuwa na mamlaka kwa serikali washirika kwa sababu haina rasilimali za kujiendesha kiuchumi.

“Rais wa dola hii hatakuwa na mamlaka, serikali hiyo haitakopesheka kwa sababu haina rasilimali, yawezekana ikawa hofu yangu lakini Napata shaka ya msingi wa serikali hiyo.Kana kwamba anawatia hofu wananchi, Rais Kikwete alidai kuwa baada ya kuundwa kwa serikali ya Tanganyika wananchi wa Zanzibar hawezi tena kuishi bara kwa amani.

“Hata tume ya Warioba katika maelezo yake haina majibu katika hili la uraia mmoja kwa nchi mbili, vinginevyo kila mtu aende zake muungano uvunjike. Lakini hilo mfanye nikiwa sipo tena madarakani,” alisema. Huku akiwasihi wajumbe kutumia maridhiano ili kumaliza kazi wakiwa wamepata katiba mpya, alisema kuwa lazima kuwe na fikra pana katika kuunda serikali ya washirika iwe na nguvu za kufanya kazi.

“Hii serikali mnajiridhisha ipo lakini haipo. Watakuja kuwafukuzeni nyote hapa. Wanajeshi wataingia na kutwaa madaraka, watafuta katiba na kisha wanavua kombati na kugombea urais,” alisema. “Jambo hili limekuwa likijirudia sana na sasa nafurahi linajadilika ili limalizike kwa kukubalika au kukataliwa ili tuweze kufanya shughuli nyingine.

Akigusia kauli ya Jaji Warioba kuwa mataizo ya serikali mbili yalianza mwaka 1984 kulipotokea mchafuko wa kisiasa Zanzibar, rais alisema kuwa Nyerere na Karume walichagua muundo wa serikali mbili ili kuzuia Zanzibar kumezwa, na Tanganyika isibebe gharama kubwa za muungano.
“Hivi karibuni alinitembelea kiongozi mmoja mkubwa wa dini fulani pale Ikulu. Akaniambia kuwa hivi kumaliza kero za muungano ni kuongeza serikali ya tatu au ni kuongeza kero nyingine ya gharama,” alisema Rais na kushangiliwa bila hata kumtaja kiongozi huyo.
Huku akitaja kasoro kadhaa alizodai zimo katika rasimu hiyo, Kikwete aliwataka wajumbe kujiridhisha kuhusu uandishi kwani vifungu vingine havijakaa sawa.
Alitolea mfano ibara ya pili inayozungumzia mipaka ya nchi akisema kuwa ina upungufu kwa kutotaja eneo la mipaka ya mito na maziwa kwa upande wa Tanganyika.

“Yako maziwa makubwa na mito katika mipaka yetu, sasa rasimu inataja eneo la bahari tu kwa upande wa bara. Hii lazima tuiweke sawa kwenye katiba ili baadaye majirani wasije kutusumbua. Pia aligusia ibara ya 128 (2)(d) inayohusu mbunge kupoteza ubunge wake kutokana na maradhi ya muda wa miezi sita au kuwa gerezani akisema inapaswa kurekebishwa.

Rais alikinzana na kipengele cha ukomo wa ubunge ambacho kwenye rasimu kinapendekezwa kuwa ni vipindi vitatu kisha mbunge anapumzika.Alisema kuwa mapendekezo hayo ni kuwanyima wanasiasa wachanga fursa na uzoefu wa uongozi na kwamba ukomo wa madaraka umewekwa kwa viongozi wakuu si ubunge.

Hotuba ya Rais Kikwete iliibua ukosoaji kutoka kwa baadhi ya wananchi waliomsikiliza, huku wengi wao wakisema kuwa aliyehutubia Bunge alikuwa mwenyekiti wa CCM, si rais wa nchi.Akizungumzia hotuba ya rais, mwandishi wa habari nguli, Ndimara Tegambawage, ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa mfumo wa vyama vingi vya siasa, na ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Muleba Kaskazini (1995-2000) alisema:

“Kwa suala la Muungano, Kikwete anatumia hoja dhaifu. Kwa ushahidi wote uliomo katika wasilisho la Warioba kuonyesha kuvunjika zamani kwa muungano, Kikwete atasikilizwa na watu wenye mawazo dhaifu. Warioba hajazungumzia kuvunja, bali kulinda muungano kwa mazingira ya sasa, kwa kutumia nyenzo zilizopo. Hoja ni kwamba muungano wa nchi mbili, serikali mbili hauwezekani.

“Hivi tunavyozungumza, Muungano haupo. Kama Zanzibar wameshaunda nchi yao, wamekataa muungano wa serikali mbili.  Kama yeye hawezi kuona hili, muache … Wananchi watamlazimisha.”Mmoja wa wasomaji wa gazeti hili aishiye Mwanza alijitambulisha kama Faustine Msekwa, alituma ujumbe mfupi wa simu uliosomeka hivi:

“Nasikitika kukuarifu kuwa Rais Kikwete hajahutubia Bunge Maalumu la Katiba, isipokuwa ametoa msimamo wa CCM juu ya katiba ya nchi. Nimekubali nia yake ni dhaifu kwa taifa. Kuna kazi kupatikana kwa Tanzania tunayoitaka.”

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .