RAIS KIKWETE KUZINDUA SHUGHULI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA LEO

Posted in
No comments
Friday, March 21, 2014 By danielmjema.blogspot.com

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kuzindua rasmi shughuli za bunge la kitaifa kuhusu marekebisho ya katiba mjini Dodoma katika hatua itakayoanzisha rasmi mjadala wa kitaifa kuhusu marekebisho hayo.

Bunge hilo maalum la katiba limepewa kati ya siku 70 hadi 90 kujadili rasimu ya katiba na kisha kuifanyia marekebisho kabla ya kura ya maamuzi.
Kuna ripoti kwamba baadhi ya wajumbe kutoka upinzani na mashirika ya kiraia yanapanga kuvuruga shughuli hiyo ya uzinduzi.
Suala la hotuba ya Rais Kikwete limekuwa sehemu ya mjadala katika Bunge hilo kutokana na baadhi ya wajumbe kuhoji sababu za Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu kabla ya Rais kuzindua Bunge kwa mujibu wa kanuni.

Mjadala huo uliwafanya baadhi ya wajumbe kumzuia Jaji Warioba Jumatatu iliyopita kuwasilisha rasimu hiyo kama ilivyokuwa imepangwa.

Kikao cha maridhiano kilifanyika siku hiyohiyo usiku na kufikia mwafaka kwamba Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba awasilishe Rasimu ndiposa Rais aweze kuzindua shughuli ya kujadili rasimu hiyo kabla ya kura ya maoni.
 
 Kikwete na ujumbe mzito 
 
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana na Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad,   Rais Kikwete atahutubia Bunge hilo kwa mujibu wa Kanuni ya 75 (1) ambapo ataambatana na ujumbe mzito wa marais wastaafu wa pande zote za Muungano, wake wa waasisi wa taifa na mawaziri wakuu wastaafu atakapokwenda kuzindua Bunge Maalumu la Katiba.
 
Hatua ya Rais kuambatana na ujumbe huo imepongezwa na viongozi wa vyama vikuu vya upinzani nchini, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na mwenzake wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mbali na viongozi hao, Rais Kikwete pia ataambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad.
Wanaotarajiwa kuwamo katika msafara huo ni Rais wa pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa tatu, Benjamin Mkapa na marais wastaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour na Amani Abeid Karume, Mama Maria Nyerere na Mama Fatma Karume.
Mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba-Samwel Sitta
Miongoni mwa mawaziri wakuu wastaafu wanaotarajiwa kuwamo ni pamoja na Jaji Joseph Warioba, ambaye juzi aliwasilisha bungeni hapo Rasimu ya Katiba kwa kutoa hotuba iliyoliteka Bunge kwa jinsi alivyofafanua mambo mengi yenye utata kuhusu muundo wa Muungano.
Mawaziri wakuu wengine ni Cleopa Msuya, John Malecela, Dk Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye pamoja na Edward Lowassa na Mizengo Pinda ambao ni wajumbe wa bunge hilo.
Wengine walioalikwa ni mabalozi wa nchi mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa dini, vyama vya wafanyakazi, vyama vya siasa, wafugaji, wakulima, wavuvi na wawakilishi wa sekta binafsi.

Rais Kikwete atapokewa katika Viwanja vya Bunge na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na baadaye kukagua gwaride maalumu kabla ya kuhutubia Bunge kuanzia saa 10:00 jioni.
Baadhi ya wajumbe wa bunge hilo
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana, baada ya Rais kuhutubia saa 11:35 jioni, aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa bunge hilo, Pandu Ameir Kificho atatoa neno la shukurani kabla ya Rais kupiga picha za kumbukumbu na wajumbe wa Bunge hilo.

Suala la hotuba ya Rais Kikwete limekuwa sehemu ya mjadala katika Bunge hilo kutokana na baadhi ya wajumbe kuhoji sababu za Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu kabla ya Rais kuzindua Bunge kwa mujibu wa kanuni.
Mjadala huo uliwafanya baadhi ya wajumbe kumzuia Jaji Warioba Jumatatu iliyopita kuwasilisha rasimu hiyo kama ilivyokuwa imepangwa hadi kilipofanyika kikao cha maridhiano siku hiyohiyo usiku na kufikia mwafaka kwamba Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba awasilishe Rasimu Jumanne, Machi 18 mwaka huu, na Rais ahutubie leo.
 

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .