JARIBIO LA KUTEKA NYARA MTOTO WA MWANAHABARI LASHINDIKANA

Posted in
No comments
Friday, May 2, 2014 By danielmjema.blogspot.com

Rehema Matowo-mwandishi wa Mwananchi Kilimanjaro

Na Mwandishi Wetu, Moshi

Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz amewatahadharisha wazazi wenye watoto wadogo, kuwaelimisha wafanyakazi wa ndani kutowakabidhi watoto wao kwa watu wasiowajua.

Tahadhari hiyo inafuatia tukio la jana saa 7:00 mchana ambapo watu watatu wakiwa na pikipiki mbili, walifanya jaribio la kutaka kumteka mtoto wa mwandishi wa gazeti hili mkoa Kilimanjaro, Rehema Matowo.

Watu hao walifika nyumbani kwa mwandishi huyo saa 7:00 mchana na kumweleza mfanyakazi wa ndani kuwa wametumwa na baba mzazi wa mtoto huyo ili wamchukue kutoka Soweto na kumpelekea katikati ya mji.

 “Aliwauliza mbona baba wala mama hajapiga simu?… hao watu wakasisitiza wametumwa kumchukua mtoto huyo tena wakimtaja kwa jina mtoto na jina la baba”alisema Rehema. Mtoto huyo ana umri wa miaka miwili na miezi nane.

Hata hivyo mfanyakazi huyo aliwatilia mashaka watu hao na kurudi ndani kisha kufunga geti la nyumba hiyo lakini watu hao wakagonga geti hilo mara kadhaa wakisisitiza kupewa mtoto.

Wakati watu hao wakiendelea kugonga geti hilo, mfanyakazi huyo alimpigia simu mwandishi huyo na kumweleza ambapo alimtahadharisha kutofungua geti hilo kwa vile ni jambo la ajabu.

“Tumeondoka na mume wangu asubuhi kwenda ofisini na kila mmoja anafanya kazi ofisi tofauti na isingewezekana kumhitaji mtoto bila mimi kunijulisha na nilipomweleza naye alishtuka sana”alisema.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Boaz aliwatahadharisha wazazi kuwa makini ikiwamo kuwapa elimu wafanyakazi wao ili kuchukua tahadhari pindi wanapokutana na matukio yasiyo ya kawaida.

“Huwezi kujua dhamira yao hasa ilikuwa ni nini, inawezekana walitaka kumteka nyara mtoto au kwa madhumuni mengine maana hivi sasa kuna matukio ya ajabu ajabu huwa yanaibuka,”alisema.

Kamanda Boaz, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari pale wanapowaona watu wakiwa katika harakati zinazotilia shaka hasa katika maeneo yao na watoe taarifa polisi mara moja.
 
Vitendo vya utekaji nyara watoto mkoani kilimanjaro viliwahi kutikisa mkoa huo miaka miwili iliyopita ambapo watoto walikuwa wakitekwa nyara na kupelekwa katika mji wa Busia nchini Uganda na baadae kurudishwa baada ya wazazi kulipa fedha kwa watekaji kupitia Benki ya Stanbic

Source:Mwananchi

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .