WAKUTANA KUJADILI MKAKATI WA MRADI WA KIJIJI CHA DIGITALI
Posted in
Matukio
No comments
Friday, February 27, 2015
By
danielmjema.blogspot.com
Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph, akiwasilisha mada ya mchanganuo wa ufumbi wa changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa mradi wa kijiji cha kidigitali.
Na Mwandishi wetu, Bagamoyo
WADAU mbalimbali wa elimu, afya, Tehama na masuala ya utamaduni na uchumi ambao wamo katika mradi wa kijiji cha dijiti cha Ololosokwan kilichopo wilayani Monduli Arusha wanakutana kwa warsha ya wiki moja ikiwa ni sehemu ya mandalizi ya uwapo wa kijiji hicho nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini Al Amin Yusuph warsha hiyo imelenga kuangalia changamoto na namna ya kuzitatua ili mradi kuwa na tija kwa wananchi wake.
Yusuph alisema kwamba wadau hao wanapanga mkakati kuangalia vipaumbele na changamoto katika utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitatu. Alisisitiza kwamba kwa kuwa mradi huo utakuwa na mawasiliano ya kisasa, masomo kwa njia ya Tehama, tiba kwa kutumia mtandao wadau wamekusanyika mjini Bagamoyo kuangalia namna bora ya kuufanya mradi huo uwe endelevu hata kama UNESCO na mbia wake Samsung watajiondoa huko mbeleni.
Aliwataja baadhi ya wadau kuwa ni kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Afya na ustawi wa jamii, Samsung, Unesco, wanakijiji wa Ololosokwan, waganga wa jadi wakunga, Taasisi ya elimu na Chuo cha Ufundi cha DIT.
Alisema changamoto ambazo zinaonekana ni lazima ziangaliwe ni pamoja na matumizi ya lugha hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa wengi wa wananchi wa Kimasai hawazungumzi Kiswahili fasaha.
“tunategemea sana Tehama kufanikisha mradi huu, na lugha inayoweza kutumiwa ni Kiswahili, sasa hili ni changamoto ni lazima kuangalia mawasiliano” alisema Yusuph na kuongeza kuwa kuwapo kwa radio ya jamii kutachangia kwa kiasi kikubwa kutoa nafasi ya wananchi wengi kujifunza Kiswahili.
Aidha alisema kwamba mambo mengine ambayo yanaangaliwa katika warsha hiyo ni matumizi ya Tehama (intaneti) na kutoa mafunzo ya namna ya kuhudumia na kufanyia matengenezo mitambo mbalimbali iliyomo katika mradi huo.
Mwenyekiti wa kikundi cha elimu kutoka UNESCO, Jennifer Kotta akishiriki kutoa maoni wakati wa warsha hiyo inayoendelea wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani. Aliyesimama ni Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph.
Alisema nia kubwa ya kukusanya wadau mbalimbali ni kuangalia utekelezaji wa nia ya mradi ya kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kwa jamii ya kimasaii ambayo kwa sasa utamaduni na uchumi wake unatishiwa na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tunataka maendeleo haya yasaidiwe na mawasiliano. Tunaangalia jinsi ya kutumia mawasiliano kuleta maendeleo” alisema Yusuph. Alisema ni matumaini yao kwamba wabia wengine wa mradi huu ambao ni kampuni ya simu ya Airtel watatumia uwezo wao kuhakikisha kwamba kijiji hicho kinakuwa hewani muda wote kwa lengo la kurahisisha huduma zinazopatikana kwa njia ya mtandao hasa tiba.
Aidha alisema kwamba pamoja na kuleta maendeleo mradi huo unakusudiwa kuhamasisha amani kati ya koo na makabila mbalimbali yaliyopo wilayani Ngorongoro.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Dkt. Peter Kitenyi (wa kwanza kulia) akichangia maoni kwenye kikundi cha sekta ya Afya wakati wa kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili jamii ya wafugaji wa kijiji cha Ololosokwan katika utekelezaji wa mradi wa kijiji cha kidigitali huku Mwenyekiti wa kikundi hicho kutoka UNESCO, Bw. Mathias Herman(katikati kulia) akiorodhesha maboresho ya changamoto hizo.
Katika warsha hiyo ambapo wadau wamegawanyika makundi mbalimbali ili kutengeneza hoja za kufanyia kazi kwa ajili ya kufanikisha masuala ya elimu na afya. Katika elimu wameangalia vikwazo ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni na watoto kuacha shule kwenda kuchunga mifugo.
Ili kukabiliana na kiwango kikubwa cha kutojua kusoma na kuandika kipaumbele kinachofikiriwa ni kuwafikia vijana hao wakiwa machungani kwa kuwapelekea mafunzo kwa njia ya mtandao.
Afisa Mipango wa Elimu wa Unesco, Jennifer Kotta alisema changamoto ya elimu katika kijiji hicho na majirani ni kubwa na kwamba wanachofikiria ni kutumia Tehama ambapo sasa watawafikia vijana kule waliko.
Wadau mbalimbali wa Elimu, Afya, Tehama na masuala ya utamaduni na uchumi wanaoshiriki warsha ya wiki moja inayofanyika wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani ikiwa ni sehemu ya mandalizi ya uwapo wa kijiji cha dijiti cha Samsung cha Ololosokwan kilichopo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.
Aidha wamepanga kufunza lugha ya Kiswahili na Kiingereza ili kutanua wigo wa majadiliano wa wakazi wa eneo hilo na watalii wanaofika na kupenda kununua kazi zao. Warsha hiyo iliyofunguliwa na Mkurugenzi Mkazi wa Unesco nchini inafanyika wakati vifaa vya kutengeneza kijiji hicho vikiwa vimeshaondoka katika bandari ya Dar es salaam.
Katika masuala ya Afya wadau wameangalia vipaumbele vinavyostahili sasa ikiwa ni pamoja na utunzaji wa mimba na mtoto. Wamesema wanawake wa kimasai wanafanya shughuli nyingi kuanzia ujenzi wa makazi na ukamuaji wa maziwa hadi ulezi wa watoto na kusema katika mazingira hayo wanahitaji sana elimu ya uzazi salama.
Mwenyekiti wa kikundi cha Sanaa na ubunifu kutoka UNESCO, Courtney Ivins (wa pili kushoto) wakijadiliana na wanakikundu wenzake kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya utamaduni hususani kwa wakimama wa kimasai wanaotengeneza bidhaa za shanga jinsi ya kuziboresha na kuvutia watalii wanaotembelea hifadhi ya Ngorongoro mpaka kijiji cha Ololosokwan pamoja na jinsi ya kutatua migogoro ya ardhi iliyopo kwenye jamii za wafugaji.
Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph (wa kwanza kulia) wakiwa kwenye majadiliano na kikundi chake huku wakiangalia changamoto mbalimbali za masuala ya Tehama zinazoikabili kijiji cha Ololosokwan kwa ajili ya kuziboresha ikiwa ni maandalizi ya kupokea mradi wa kijiji cha kidigitali.
Mwenyekiti wa kikundi cha elimu kutoka UNESCO, Jennifer Kotta (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa elimu ya msingi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Sarah Mlaki (wa kwanza kushoto) na wadau kutoka Ololosokwan wakianisha changamoto na utatuzi wa changamoto kwenye sekta ya elimu katika kuboresha utekelezaji wa mradi wa kijiji cha kidigiti cha Samsung cha Ololosokwan wakati wa warsha ya wiki moja iliyoandaliwa na UNESCO wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :