LOWASA: UKWELI WA SAKATA LA RICHMOND NI HUU

Posted in
No comments
Wednesday, June 3, 2015 By danielmjema.blogspot.com

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Ngoyai Lowassa
Kwa mara ya kwanza Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa amefunguka na kueleza ukweli halisi wa sakata zima la Richmond lililomfanya achukue uamuzi wa kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mwaka 2008.
Katika maojiano maalumu na Rai, Toleo namba 1201, Mei 28 Mwaka Huu, Lowassa aliweka wazi kupitia  wazi kuwa anapata shida kujua kama tupo makini kusimamia ipasavyo mambo yanayohusu maisha yetu,kwani masihara ya kisiasa yaliyoratibiwa na baadhi ya wabunge ndiyo yaliyosababisha serikali kupitia Tanesco kushindwa katika kesi ya kuvunjwa kwa mkataba wa Richmond/Dowans katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa mizozo ya kiuwekezaji (ICC) iliyopo Paris nchini Ufaransa na kutakiwa kulipa mabilioni ya pesa. 

Pamoja na mambo mengine, Lowassa ambaye ametangaza nia ya kuwania nafasi ya Urais amezungumzia kwa kina urafiki wake na Rais Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na utajiri wake. 

Ukweli juu ya Sakata la Richmond 

Swali: Utakumbuka kwamba ulijiuzulu uwaziri mkuu kutokana na sakata la Richmond. Leo hii ni miaka saba imepita, unaweza kutueleza uhusika wako katika sakata hili? 

Jibu: Waswahili wanasema ukweli unajitetea wenyewe.Lakini nianze kulijibu hili kwa kueleza maana halisi ya dhana ya kuwajibika. Si kosa hata kidogo kujiuzulu wadhifa wa kisiasa kunapotokea mkanganyiko wa mambo kwa namna ile ilivyotokea. Uongozi ni dhamana. 

Mimi sio kiongozi wa kwanza hapa nchini na nje ya nchi kuwajibika yanapotokea mambo ya namna hiyo. Rais wetu mstaafu mzee Ali Hassan Mwinyi alipata kuwajibika kwa njia ya kujiuzulu uwaziri wa mambo ya ndani baada ya Raia kuuawa na polisi mkoani Shinyanga miaka ya 70. 

Naamini kwa dhati kabisa kwamba watanzania walio wengi sasa wanajua zaidi ukweli kuhusu sakata la Richmond ambalo lilisababisha nijiuzulu uwaziri mkuu. 

Pengine niseme tena leo, kwamba niliwajibika kisiasa kwa sababu kuu mbili: 

1:Kulinda heshima ya chama changu na serikali kama nilivyosema wakati ule. 
2: Nilijiuzulu ili ku 'register' masikitiko yangu kwa namna kamati teule ya bunge ilivyolitaja jina langu sana na tena kwa namna ya kunituhumu kwa mambo ambayo sikuyafanya, wakifanya hivyo pasipo kunipa haki ya msingi ya kusikilizwa (Natural Justice). 

Sakata la Richmond ni kielelezo kizuri au mfano mzuri wa kihistoria wa namna magomvi ya kisiasa yanavyoweza kuliingiza taifa katika gharama au hasara kubwa. Ni jambo la bahati mbaya, kwamba kasoro za kimaamuzi na kiutendaji zilizotokea wakati wa mchakato wa kutafuta suluhu ya dharura iliyokuwa ikikusudiwa kulinusuru taifa katika madhila kubwa iliyokuwa ikitokana na ukame mkali ulioikumba nchi yetu katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 na 2007, yaligeuzwa kwa sababu tu ya kuendekeza ugomvi wa kisiasa na kuwa kile kilichopewa jina la "Kashfa kubwa ya Ufisadi". 

Ni lini na wapi kulipata kuwa na rushwa katika mkataba ambao serikali ambayo mimi nilikuwa waziri mkuu wake, ilifikia uamuzi wa mkusudi kabisa wa kukataa kuilipa hata senti moja kampuni ambayo ilionyesha mwelekeo wa kusuasua baada ya kushinda zabuni ya kuleta mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura wa megawati 120. Nasema hakuna hata senti moja ya serikali ilitumika kuilipa Richmond. 

Ikumbukwe kwamba uamuzi wa kukataa kuilipa Richmond hata senti moja ulifikiwa serikalini baada ya jambo hilo kujadiliwa katika ngazi mbalimbali serikalini kabla ya bunge kuunda kamati teule. 

Si hivyo tu, ukweli kwamba mkataba uliopipa Richmond kuzalisha na kuiuzia Tanesco Umeme ulifuata taratibu zote za kiserikali na kwa kuzingatia misingi wa mikataba mingine ya mikataba ya dharura ya namna ile ambayo ishakuwepo, ni kielelezo kingine cha namna jambo hilo lilivyoshughulikwa kwa ushabiki mkubwa wa kisiasa. 

Leo hii ninapolazimika, tena kwa uchungu na masikitiko makubwa kulijibu swali hilo, huku nikitambua kwamba ugomvi wa kisiasa ulioratibiwa na baadhi ya wabunge ndio uliosababisha serikali kushindwa katika kesi ya kuvunjwa kwa mkataba wa Richmond/Dowans hata kutakiwa kulipa mabilioni ya pesa, napata shida kujua iwapo kweli tupo makini katika kusimamia ipasavyo mambo yanayohusu taifa letu. 

Nina imani watanzania ambao wamekuwa wakifuatilia mwenendo wa bunge tangu wakati wa sakata la Escrow ni mashahidi kwamba wabunge kadhaa kutoka CCM na upinzani kwa nyakati tofauti wameonekana kuanza kupata picha na kutambua kuwa kulikuwa na njama za makusudi za kutafutana na kuumizana kisiasa wakati wa sakata la Richmond. 

Kauli ambazo zimetolewa kwa nyakati tofauti na hivi majuzi na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe kuhusu kile ambacho kilitokea wakati wa mzozo wa Richmond ni ushahidi wa hicho ninachokisema. 
Kwamba leo hii mh. Mbowe anaposema,acha nimnukuu; 

"Kuendekeza makundi na vita vya kisiasa ndani ya CCM na serikali yake kwa gharama ya taifa hili sasa linadaiwa sh. bilioni 120 baada ya kushindwa kwenye kesi ya Richmond/Dowans katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi (ICC) huko Paris" 

Mh. Mbowe haishii hapo bali anakwenda bali zaidi na kusema iwapo ukweli hautawekwa bayana,"huko mbeleni jambo hilo litaligharimu taifa mabilioni haya ya fedha ambayo yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki vingetawala mchakato mzima wa kashfa ya Richmond."
 
Ni wazi kwamba anachokisema Mbowe hapa ni kwamba swala hili lilishughulikuwa katika misingi isiyo bayana na kwamba haki haikutendeka. 
Ukweli mchungu, leo hii mitambo ileile iliyoletwa na Richmond na Dowans ambayo ingeweza kununuliwa na Tanesco kama baadhi ya wataalamu walivyoshauri, badala yake inamilikiwa na kampuni ya kimarekani ya Symbion baada ya mkataba kuvunjwa kinyume cha sheria. 

Wakati tukiugulia maumivu ya makosa yetu,Rais wa Marekani Barack Obama na aliyekuwa Waziri wa mambo ya nje wa taifa hilo kuwa, Hillary Clinton,kwa nyakati tofauti wakati wa ziara zao hapa nchini walisifia ubora wa mitambo hiyo kuwa ni ya kisasa kabisa tofauti na kile kilichoelezwa wa wale wanaoendekeza siasa za makundi ambao walidai kuwa mitambo hiyo haiwezi kuwasha hata hata kibatari. 

Lakini kubwa na muhimu katika yote hayo ni hukumu ya Mahakama ya ICC ambayo ilisomwa na majaji watatu ambao weledi na uzoefu wao mkubwa kisheria si wa kutiliwa shaka, mmoja akitokea katika Supreme Court ya Marekani, mwingine wa mahakama ya Rufani ya Uingereza na watatu kutoka Mahakama ya Rufani ya Uganda. 

Majaji hao watatu katika hukumu yao walitamka bayana kuhusu kufuatwa kwa taratibu zote za kisheria katika kuipa ushindi Richmond/Dowans katika zabuni yake na kutokuwepo kwa wingu lolote la shaka juu ya vitendo vya Rushwa katika mchakato mzima wa zabuni hiyo. Vinginevyo tusingeshindwa kesi hii na kuligharimu taifa mabilioni haya. 

Ukisoma Ripoti ya kamati ya Dr Harrison Mwakyembe, kuna sehemu inaeleza bayana kwamba mwaka 2004,zaidi ya mwaka mmoja kabla serikali ya awamu ya nne ambayo mimi nilikuwa waziri mkuu wake haijaingia madarakani,kampuni hiyo hiyo ya Richmond ilishinda zabuni kubwa ya kujenga bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza. 

Huu ni ushahidi wa kwanza muhimu kwamba hii kampuni ilishakuwa miongoni mwa kampuni za kiukezaji miaka kadhaa kabla ya mimi sijawa waziri mkuu. 

Ukweli huu uliothibitishwa hadi katika kamati teule ya Mwakyembe ni ushahidi wa kwanza wa wazi kwamba eti mimi Lowassa ndiye niliyekuwa mmiliki wa kampuni hiyo ambayo hata wawekezaji wake sijapata kuwajua au hata kukutana nao hazikuwa sahihi. 

Lakini tukumbuke kwamba madai haya yalithibitika kuwa siyo sahihi baada ya mahakama ya kimataifa ya usuluhishi kutamka kwamba Richmond ilikuwa kampuni iliyosajiliwa Marekani kwa miaka mingi na kwamba ilishinda zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kihalali. 

Kwangu mimi jambo muhimu katika sakata hili lilikuwa ni uamuzi wa bodi ya tenda ya Tanesco na wizara ya Nishati ambayo katika rekodi zake ilikuwa ikiifahamu vizuri Richmond kutochukua tahadhari mapema, yaani kufanya due deligence ipasavyo, kwa kuangalia uwezo wa kifedha wa kampuni husika kabla ya kuipa ushindi. 

Sasa naingiaje Lowassa hapo au familia yangu? Hakika haya ni masihara, Mungu anajua. 

Uhusiano Wake na Rais Kikwete 

Swali:Jina lako limetajwa kwa muda mrefu pengine kuliko ilivyo kwa mwanasiasa mwingine yeyote ndani na nje ya CCM juu ya kuwa mgomea Urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Je,unafikiri ni kwa nini imekuwa hivyo?

Je,umejiandaa kukabiliana na mikiki ya Urais?

Iwapo jibu lako ni ndiyo,nini hasa ambacho wewe unadhani unastahili zaidi pengine kuliko kwa mgombea mwingine yeyote kubebeshwa dhamana hiyo kubwa na nzito?

Unaweza kutuambia ni mambo gani hasa umepanga kulifanyia taifa hili iwapo CCM itakuteua kuwa mgombea wake wa Urais na watanzania wakakuchagua kuwa kiongozi wao mkuu?

Kwa miaka mingi sasa jina lako limekuwa likitajwa sambamba na Rais Kikwete.Unaweza ukawaeleza watanzania wewe na Kikwete mlikutana lini na wapi?

Jibu: Ni kweli kwamba jina langu limehusishwa sana na Rais Kikwete kwa wema na kwa ubaya. Kwa wema kwamba tumefanya naye kazi ndani ya CCM,kabla sote wawili hatujapata fursa ya kuitumikia serikali
Katika hadhira na hususani nje ya CCM, uhusiano wangu na mh.Rais Kikwete ulianza kuonekana mwaka 1995,wakati yeye na mimi tulipokubaliana pamoja na tena baada ya kushauriana kwa kina na hatimaye tukafikia uamuzi wa kutangaza nia pamoja ya kuchukua fomu na kukiomba chama chetu,chama cha mapinduzi kiteue mmoja wetu kubeba bendera ya chama ya kugombea urais.

Tulipotangaza uamuzi wetu huo, tuliwaahidi watanzania mbele ya vyombo vya habari kwamba, yeyote ambaye angeshinda, yule mwenzake aliyeshindwa angemuunga mkono kwa nguvu zake zote.

Kimsingi kile ambacho siku zote nimekuwa nikiita safari ya matumaini kilianza na ndoto hiyo ambayo sote wawili tuliijenga katika misingi ya kutambua kuwa"Uongozi ni wajibu na kuwa kiongozi ni kuwa mtumishi wa watu",.

Tangu wakati huo, tumeendelea kuwa karibu kirafiki,kisiasa na kikazi na Rais Kikwete,tukishirikiana vyema katika kujadili, kuanisha na kutafuta majibu ya changamoto mbalimbali za kiungozi katika taifa letu.

Uamuzi huo ndiyo ambao ulisababisha wakati fulani nilipokuwa nikiongea na wanahabari miaka kadhaa baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu nitoe kauli ambayo ilipewa tafsiri tofauti na wanasiasa na wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kisiasa pale niliposema;" Mimi na Rais Kikwete hatukukutana barabarani".

Ni imani hiyo niliyoijenga katika misingi mama ya kufahamiana na kuaminiana ndiyo ambayo wakati wa mchakato wa kumtafuta Rais wa Nne wa Tanzania kwa moyo wa dhati kabisa nilimuunga mkono mwenzangu katika harakati hizo na wenzangu tuliokuwa na mawazo hayo wakaniteua mimi kuwa mwenyekiti wa kamati ya ushindi ambayo ilikuwa na kazi kubwa na ngumu ya kuratibu harakati za kumhakikishia mgomea wetu huyo ( Rais Kikwete) anateuliwa kubeba bendera ya kugombea kwa tiketi ya CCM. Jambo jema katika hili tulifanikiwa na tukashinda.

Kilichofuata baada ya hapo wengi wanakifahamu,mheshimiwa Rais alinipa heshima kwa ridhaa yake mwenyewe Disemba 2005 kuwa Waziri mkuu wake wa kwanza katika Serikali yake. Hili la kwamba ni rafiki yangu, ni swala ambalo hata yeye mwenyewe mheshimiwa Rais amepata kulielezea hadharani mara kadhaa tangu mwaka 1995 na baadaye akafanya hivyo mwaka 2005 alipokuwa akirejesha fomu yake ya kuomba ridhaa ya CCM alipotutaja mimi na Rostam Aziz kuwa ni marafiki zake.

Waliosoma maandiko yake watakuwa wanakumbuka kwamba yeye mwenyewe amepata kuandika kwa mkono wake kwamba, aliniteua kuwa waziri mkuu si kwa sababu ya urafiki wetu bali kwa kutambua uwezo na uchapakazi wangu.
Kwangu hilo ni jambo la faraja na kutia moyo sana.Naamini maelezo hayo yanajibu kwa sehemu kubwa kile ambacho kila mara kimekuwa kikirejewa kuhusu urafiki wangu na Rais Kikwete.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .