WANASIASA KILIMANJARO WAMLILIA PETER KISUMO.

No comments
Friday, August 7, 2015 By danielmjema.blogspot.com


Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro.
KUFUATIA kifo cha Kada wa siku nyingi wa chama cha mapinduzi (CCM) na mmoja wa waasisi wa TANU na baadae CCM, Mzee Peter Kisumo, aliyefariki dunia juzi majira ya saa moja usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, makada mbalimbali wa chama cha mapinduzi mkoani Kilimanjaro pamoja na viongozi waliowahi kufanya naye kazi wametaja msiba huo kuwa ni pigo kwa Taifa hili.

Taarifa zilizothibitishwa na Mtoto wake, Michael Kisumo, zinasema kuwa, hali ya ugonjwa wa Marehemu Peter Kisumo ilifikia katika kiwango cha juu na kulazimika kufanyiwa uchujaji wa figo mara tatu kwa wiki kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini ambaye aliwahi kushika nyadhifa kadhaa katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, alifariki Dunia Agosti 3, mwaka huu, akiwa katika Hospitali ya Muhimbili ambako alikopelekwa kwa ajili ya kufanyiwa dialysis (usafishaji damu katika figo) kabla ya kujitokeza kwa utata (complication) kulikopelekea kuharisha damu.

Wakizungumza na mtandao wa Kijiwe chetu Blog, viongozi hao walisema msiba huo umekuja kipindi ambacho Taifa bado linahitaji msaada wake hasa kipindi hiki muhimu ambacho nchi inajiandaa katika Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Nsilo Swai.

Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro, Mama Vicky Nsilo Swai, alisema msiba huo ni pigo kubwa kwa Taifa hili kwani alikuwa na mchango mkubwa katika siasa za vyama vingi.

Nsilo Swai alimtaja Marehemu Mzee Kisumo, kama mtu aliyependa sana kusaidia, mcheshi na kwamba Mzee Kimaro alikuwa msaada mkubwa kwake katika miaka yake 17 ya Siasa.
Alisema Chama cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro daima kitaendelea kuenzi yale yote mema ya Mzee Kisumo.

“Msiba huu ni pigo kubwa kwetu, ni pigo kubwa kwa Taifa la Tanzania, ni pigo kwa chama cha Mapinduzi, Mzee Kisumo alikuwa ni kiongozi wa mfano, alikuwa mcheshi, mpenda chama, mpambanaji, katika miaka yangu 17 ya Siasa, alinisaidia sana na hata katika miaka yangu 10 ya Uenyekiti alikuwa ni mtu muhimu sana kwangu” alisema Nsilo Swai.


Dkt. Augustino Mrema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha TLP Taifa, Dkt. Augustino Mrema alisema Daima wananchi wa Vunjo watamkumbuka sana Marehemu Peter kutokana na ukarimu wake kwao kwani miradi mingi ya maendeleo katika jimbo hilo ilianzishwa na Kisumo.

Akitolea mfano miradi ya maji katika eneo la Njia panda ambayo kwa sasa yako chini ya mamlaka ya maji safi na maji taka ya wilaya ya Moshi (MUWSA), Dkt. Mrema alisema miradi hiyo pamoja na mingine mengi jimboni humo yalifadhiliwa na Kiongozi huyo.

“Kisumo alikuwa mtu wa watu, wana Vunjo wanamkumbuka sana, amesaidia kuhakikisha tunapata maji, pale njia panda na jimbo zima alisambaza maji, Kisumo ni mzalendo wa kweli, mpiganaji na kiongozi makini sana”, alisema Dkt. Mrema.

Mbunge huyo wa Jimbo la Vunjo, anayemaliza muda wake, alimtaja Marehemu Peter Kisumo, kama kiongozi mvumilivu, mzalendo na mtu ambaye daima alitanguliza mbele maslahi ya wananchi wake bila kujali itikadi zao za kisiasa, dini wala kabila.

Michael Mwita.

Katibu wa Uenezi na Itikadi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani Kilimanjaro, Michael Mwita aliwataka wananchi wa Mkoa huo kuungana pamoja kuenzi yote mema aliyoyahubiri kiongozi huyo kuhakikisha mkoa huo unaendelea kupiga hatua katika maendeleo.

Mwita alisema alimfahamu Marehemu Peter Kisumo, kama Kiongozi mahiri aliyekuwa na Msimamo usioyumba na kwamba siku zote hata baada ya kung’atuka katika ulingo wa siasa aliendelea kutumia busara zake kuhakikisha chama hakiyumbi.

“Chama kimempoteza mtu muhimu sana, mtu mzoefu na kiongozi makini sana, Mzee Kisumo nilimfahamu tangu nikiwa mdogo, tunamzungumzia mtu aliyeshika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika taifa, alitumia busara zake kutatua vurugu ndani na nje ya chama, sina mengi ya kusema zaidi ya kuwataka wanaCCM kuenzi yote katika kipindi hiki ili itusaidie kuchukua dola”, alisema Mwita.

Kisumo aliwahi kuwa mmoja wa mameneja wa kampeni wa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 akisimamia kanda ya kaskazini iliyojumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga. Mbali ya kuwa waziri, Kisumo aliwahi pia kuwa Mbunge wa Jimbo la Mwanga, mkuu wa mkoa wa Mwanza (1975-1977) na mdhamini wa CCM.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .