KUMBUKUMBU: HARAKATI ZA KUNDI LA G55 NA UASI WA WAZI KWA MUUNGANO MWAKA 1993

No comments
Monday, April 11, 2016 By danielmjema.blogspot.com

KWA muhtasari, nimezungumza na Mzee Njelu Kasaka kuhusu kilichojiri kati ya kundi la wabunge maarufu kama G55 na Mwalimu Julius Nyerere. Kasaka (akiwa Mbunge wa Lupa-Mbeya) ndiye aliyeibua hoja iliyobebwa na G55, kuhusu kuidai Tanganyika.


Ingawa nimepata fursa ya mahojiano naye siku zijazo, lakini ni muhimu kujiuliza ni kwa nini Mwalimu Julius Nyerere, hakuwa mkali kwa wana-G55, tofauti na alivyokuwa ndani ya vikao vya juu vya Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikalini; hasa kwa Waziri Mkuu, John Malecela?

Ndiyo, Mwalimu hakuwa mkali kwa G55 na hata Kasaka amegusia hili kwamba kati ya vikao vyote vinne walivyofanya na Nyerere wakati akihangaika kuizima hoja hiyo, mazungumzo yalifanyika kwa kuongozwa kwa nguvu ya hoja na si ukali wala kufokeana.

Lakini pia Nyerere hakuwa mkali sana kwa Rais (wakati huo), Ali Hassan Mwinyi, kama alivyokuwa kwa Waziri Mkuu, John Malecela. Hii inathibitishwa na kauli yake kwamba, Malecela alishindwa kumshauri vizuri Rais, akikwepa kugeuza hoja hiyo upande wa pili, Rais naye alipokea ushauri usio mzuri. Kwa nini haya yote?

Bahati mbaya, sikumuuliza Kasaka kwa nini Nyerere hakuwa mkali kwao (wachokoza mada) kwa sababu hili ni swali alilopaswa kujibu Nyerere mwenyewe, ingawa pia Kasaka na wenzake wanaweza wakabaini sababu. Kwa upande wake na kwa kuzingatia maelezo ya Kasaka, niliridhika kuwa Nyerere hakuwa mkali sana kwa G55.

Swali hili kwamba kwa nini Nyerere hakuwa mkali kwa kiwango sawa kwa G55, kama ilivyokuwa kwa Waziri Mkuu Malecela na viongozi wengine, ni endelevu; maana linajadilika na mwenye mawazo zaidi ashiriki mjadala huu lakini kwa manufaa ya nchi yetu.

Binafsi, kama nilivyoeleza, nimebaini Nyerere hakuwa mkali na hii inatokana na maelezo ya Kasaka kwangu ambayo alimnukuu Mwalimu Nyerere akiwaeleza G55 katika moja ya vikao kati yake na wabunge hao.

“Kama kijiji kizima wangeungana na kunieleza kuwa mama yangu mzazi ni mchawi, ningekubali.” Haya ni maneno ya Kasaka, akimnukuu Mwalimu Nyerere alichowaeleza wana-G55 nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam.

Hakuishia hapo katika mfano wake huo, Nyerere akawaeleza akina Njelu Kasaka, Jenerali Ulimwengu, Arcado Ntagazwa, Mussa Nkangaa na Sebastian Kinyondo: “Lakini kama wangenieleza kuwa nimuue kwa sababu ni mchawi, ningekataa.”

Bila shaka, Mwalimu Nyerere kwa kuzingatia mantiki ya maelezo yake hayo katika mfano wa mama mzazi, aliamini wabunge wa G55 wanayo hoja kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unazo kero zake zinazoonekana kwa wananchi.

Ni kama vile Muungano ndiye mama, wananchi (wanakijiji) wanafichua kasoro hizo na hapa Mwalimu Nyerere akaamini ni jambo zuri, lakini hakubaliani na wale wanaosema suluhisho ni kuua Muungano (kumuua mama mzazi).

Hii inaweza kuwa sababu ya kwanza kwamba, Mwalimu Nyerere hakuamini katika kuwarejesha Watanzania katika utengano; bali alimini katika Uhuru na Umoja kama inavyoeleza nembo ya Taifa.

Kwa hiyo, hakukubaliana na yeyote anayeamini kuua msingi wa umoja wa wananchi (Muungano) ni suluhusho. Lakini sababu ya pili inawezekana (nasema inawezekana kwa sababu ni Mwalimu pekee angetueleza kwa uhakika kwa nini hakuwa mkali kwa G55) ni kwamba; hoja iliyobebwa na G55 ilikuwa hatari lakini ikitetewa kwa umahiri mkubwa na wahusika.

Ilikuwa ni hoja inayohusu kuidai Tanganyika kutoka katika Muungano lakini sababu zake kama zingepotosha katika utetezi wa hoja, zingeingiza nchi kwenye matatizo ya kidini.
Hoja hii ilitokana na uamuzi wa Zanzibar, ikiongozwa na Dk. Salmin Amour, kukubali Zanzibar ijiunge na Umoja wa nchi za Kiislamu (OIC).

Ikumbukwe, kati ya masharti ya OIC ni wanachama wake kuwa si tu nchi, bali nchi za kiislamu. Kwa wakati huo na hata sasa, Zanzibar haikuwa nchi yenye mamlaka kimataifa. Nchi inayotambulika kimataifa ni Tanzania. Kwa hiyo, haikuwa halali Zanzibar kujiunga kwa sababu hiyo lakini pia kwa sababu nchi (Tanzania) si ya kidini.

Pengine hapa, Mwalimu Nyerere aliona kuna hoja za msingi katika tukio la Muungano kutikiswa na wabunge wa G55 kupinga mtikisiko huo ingawa namna ya kupinga (kuvunja Muungano) hakukubaliana nayo.

Lakini pia inawezekana Mwalimu hakuwa mkali kwa G55 kwa sababu hoja yao ilitetewa kwa kuzingatia msingi wa nchi, ambayo ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ingawa hoja hii kwa namna fulani iligusa maslahi ya dini ya kiislamu, lakini hoja zilizojengwa hazikuwa na mweleko wa kuathiri, kudharau au kupuuza dini hiyo.

Ndani ya G55 kulikuwapo na wabunge waislamu, ambao walitambua kutokana na uwezo wao katika kuchambua na kupima mambo kwamba; mustakabali wa nchi usiachwe utanguliwe na maslahi ya dini moja moja.

Kwa hiyo, mjadala huu uliendeshwa kwa udhibiti mkubwa na pengine hili lilimfanya Mwalimu kutokuwa mkali sana kwa G55, akitambua Katiba inavyosema....nchi yetu haina dini.

Lakini jambo jingine nadhani Mwalimu Nyerere hakuwa mkali zaidi kwa G55 kwa sababu, aliamini kuzima hoja hiyo (Zanzibar kujiunga OIC) hakuhitaji gharama kubwa katika ustawi wa nchi ikilinganishwa na gharama inayohitajika baada ya kuvunja Muungano.

Hali hii ni tofauti na ilivyo sasa ambapo hata mjadala wa Mahakama ya Kadhi ulishindwa kujadiliwa kwa staha, busara, hekima na maarifa ya kutosha miongoni mwa wabunge au viongozi wengine ambao hawakuona kwamba Serikali kutumbukia katika kuanzisha Mahakama hiyo kwa gharama zake ni kosa kikatiba.

Wakati umefika sasa baadhi ya viongozi wajifunze kujadili masuala mazito hata ya kiimani kwa lengo la kuboresha ustawi wa nchi. Tunapokumbuka miaka 12 ya kifo cha Mwalimu Nyerere lazima tutambue, mustakabali wa nchi yetu Tanzania unapaswa kujengwa bila kuingilia imani za watu na hivyo hivyo, imani za watu zisiachwe kuathiri mustakabali wa nchi.

Mpaka uliowekwa kikatiba kati ya maslahi ya dini na maslahi ya nchi, haupaswi kutumika kuchonganisha maeneo hayo mawili bali utumike kuimarisha umoja, mshikamano na hatimaye kujenga nchi inayoheshimu imani za watu na watu wanaoheshimu misingi ya taifa.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .