TANZANIA: WIZI MKUBWA BODI YA MIKOPO-HELSB
Posted in
Elimu
No comments
Wednesday, February 17, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
![]() |
WAZIRI WA ELIMU, dKT. JOYCE NDALICHAKO |
Wakati
migomo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu mbalimbali nchini
ikiendelea ulitikisa Taifa, uongozi wa Bodi ya Mikopo nchini (HESLB),
umefuja Sh. bilioni 3.23 za mikopo ya wanafunzi kwa kutoa mikopo hewa,
kulipa waliomaliza vyuo, ambao hawajaomba mikopo huku wengine wakilipwa
mara mbili mbili.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema
ubadhirifu wa fedha hizo ulibainishwa na Mkaguzi wa Ndani alipokagua
hesabu za bodi hiyo mwaka 2013, lakini mpaka sasa ripoti hiyo ilikuwa
imefungiwa kabatini bila kufanyiwa kazi.
Alisema
baada ya kuingia ofisini, bodi hiyo waliandikiwa barua ili kujibu hoja
zilizobainishwa na mkaguzi huyo, badala ya kujibu hoja walijikita
kulalamika kuwa Mkaguzi wa Ndani aliingia kazi ambayo ingetakiwa
kufanywa na Mkaguzi wa Bodi.
Kufuatia
kutoridhishwa na majibu hayo, alisema ofisi yake imeamua kumfuta kazi
Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, George Nyatenga.
Mbali na
Mkurugenzi huyo, Profesa Ndalichako alisema ofisi yake imewasimamisha
kazi Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusuf Kisare, Mkurugenzi wa
Urejeshaji Mikopo, Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji
Mikopo, Onesmo Laizer.
Alisema kwa
kuwa Nyatenga alishastaafu na alikuwa akifanya kazi kwa mkataba ambao
ungeisha Agosti, mwaka huu, baada ya kuuvunja kwa notisi ya siku moja,
Mkurugenzi huyo atalipwa mshahara wa mwezi mmoja kwa mujibu wa sheria ya
utumishi wa umma.
Kwa
Wakurugenzi wengine watatu waliosimamishwa, Profesa Ndalichako alisema
watakaa nje ya ofisi na wizara yake itateua maofisa wa kwenda kushika
nyadhifa zao kwa muda ambao Mkaguzi wa Ndani atarudi tena kukagua hesabu
za tangu mwaka 2013 mpaka sasa.
FEDHA ZILIVYOTAFUNWA
Profesa
Ndalichako alisema katika ukaguzi huo, ilibainika kuwa wanafunzi 23
walilipwa mikopo kupitia vyuo viwili tofauti kwa kipindi cha miaka
mitatu mfululizo.
Alisema katika chuo cha kwanza, wanafunzi hao walilipwa Sh. milioni 153.9 na kwenye chuo cha pili Sh. milioni 147.54.
Katika eneo
lingine, alisema wanafunzi 169 walipata mikopo kupitia vyuo viwili
tofauti kwa miaka miwili mfululizo ambapo kwenye chuo cha kwanza Sh.
milioni 658.04 zilitolewa huku kwenye chuo cha pili zikitolewa Sh.
milioni 665.13.
Profesa
Ndalichako alisema bodi hiyo pia ilitoa Sh. milioni 342.46 kwa wanafunzi
343 ambao usaili wao haupo kwenye vyuo ambavyo fedha hizo zimepelekwa.
Profesa Ndalichako alisema bodi hiyo pia ililipa Sh. milioni 136.23 kwa wanafunzi 55 ambao wameacha masomo.
“Sh. milioni 159.66 zililipwa kwa wanafunzi 306 zaidi ya kiwango kinachokubalika kisheria,” aliongeza Profesa Ndalichako.
Alitaja kundi lingine kuwa ni lile la wanafunzi ambao walilipwa fedha kwenye vyuo vya ndani na nje ya nchi kwa wakati mmoja.
Katika kundi
hilo, alisema wanafunzi 77 wawalilipwa Sh. 467.62 kwenye vyuo vya nje
ya nchi na wakati huo huo wakilipwa Sh. milioni 123.04 kwenye vyuo vya
ndani ambavyo walikuwa hawasomi.
Alisema pia
kuwa Sh. milioni 207.05 zilipelelekwa kwenye vyuo sita na
hazikuchukuliwa na wanafunzi na kiutaratibu zingepaswa kurudishwa Bodi,
lakini ziliyeyuka.
Alisema pia kwamba, wanafunzi 143 walilipwa Sh. milioni 173.64 katika muda ambao walikuwa hawajasajiliwa kwenye vyuo husika.
Bila kutaja
kiasi cha fedha kilicholipwa, alisema ripoti hiyo ya Mkaguzi wa Ndani
iliainisha kuwa wanafunzi 19,348 walipewa mikopo ambayo haijapitishwa na
Bodi ya Kamati ya Mikopo, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.
Pia alisema wanafunzi 54,299 walipangiwa mikopo wakati walikuwa hawajaomba.
“Wakati
kukiwa na watoto wa maskini wanaomba mikopo na hawapewi, wengine bila
hata kuomba wanapewa, hili halikubaliki,” alisisitiza Profesa
Ndalichako.
Kutokana na
hali hiyo, Profesa Ndalichako alisema utendaji mbovu na ubadhirifu
umesababisha kuwe na malalamiko kutoka kwa wanafunzi kila wakati.
Alisema
wakati mwingine, wanafunzi wanavyolalamika na wizara kuingilia kati,
hulipwa fedha zao ndani ya siku moja ama mbili, jambo linaloonyesha kuwa
siyo kweli kwamba kuna tatizo la fedha.
Alisema
kutokana na usumbufu huo usio wa lazima, wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya St.
Joseph Songea, St. Joseph Arusha, Chuo Kukuu cha Dodoma (Udom) na
wanafunzi wengine mmoja mmoja kutoka kwenye vyuo vingine, waliwasili
vyuoni mwao Novemba, 2015, lakini walipewa mikopo Januari, mwaka huu.
“Wanafunzi
wanaosoma nje ya nchi kama Ujerumani na Algeria, wamekuwa wakiendelea
kulipwa fedha wakati muda wa mkataba wao wa mikopo umeisha,” alifafanua.
Alisema
baadhi yao wameendelea kulipwa huku wakiwa wamemaliza masomo na
kuendelea na kazi kwenye nchi walizokuwa wakisoma na wengine wakiendelea
na masomo ya juu tofauti na mikataba yao ya awali ilivyokuwa inataka.
“Licha ya
udhaifu uliobainishwa na Bodi kutakiwa kujibu hoja hizo, haikutoa majibu
kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali hadi Januari, 2016 ilipoagizwa na
Wizara kufanya hivyo.
Majibu
yaliyowasilishwa na Bodi Februari mosi, mwaka huu, yanadai Mkaguzi Mkuu
wa Ndani wa Serikali, hakukidhi viwango na alijikita kwenye mambo ya
uendeshaji wakati kazi hiyo hufanywa na Mkaguzi wao wa Ndani,” alisema
Profesa Ndalichako.
ZINGESOMESHA WANAFUNZI 808
Fedha hizo ambazo zimelipwa kinyume cha taratibu, zingesomesha wanafunzi 808 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wanafunzi
hao ni wale ambao wakilipiwa asilimia 100 ya mkopo kwenye ada, fedha za
kujikimu, za vifaa vya kujifunzia na zile za mazoezi kwa vitendo na
nyingine zote ambazo zingehitajika, kila mmoja angepata Sh. milioni nne
na akasoma kwa mwaka mzima bila kudaiwa chochote.
Baadhi ya
fani ambazo wastani wa gharama yake unaakisi kiasi hicho cha fedha
kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni pamoja na ile ya Mawasiliano kwa
Umma, Uhusiano kwa Umma na Uandishi wa Habari.
Wanafunzi
hawa ambao hulipwa Sh. 8,500 kwa siku kwa ajili ya chakula na malazi,
kwa muhula hulipwa wastani wa Sh. milioni 1.2 ada ya mwaka Sh. milioni
1.3, huku kiasi kingine kikienda kwenye mafunzo kwa vitendo na mahitaji
mengine.
NA FREDY AZZAH
CHANZO: NIPASHE
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :