RWANDA: KAGAME KAMA MAGUFULI
Posted in
afrika mashariki
No comments
Monday, March 14, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
Rais wa Rwanda Paul Kagame amelaumu
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutumia pesa ‘kiholela’ kutokana na
mawaziri kufanya ziara za mara kwa mara kuhudhuria mikutano. Amesema
mawaziri wa nchi yake wanatumia chombo hicho kama njia ya kujinufaisha
kwa kufanya ziara na kuhudhuria mikutano ya jumuiya hiyo isiyo muhimu.
Ameahidi
kuiga mfano wa Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kutokomeza ufisadi
huo wa kusitisha ziara za mawaziri alizotaja kuwa za kufuja mali ya
taifa. Akiongea katika mkutano wa faragha wa viongozi wa taasisi
zote za serikali nchini Rwanda, Rais Kagame amesema suala la ufisadi
nchini humo linachukua mwelekeo mpya na kasi ya ajabu na kwamba hawezi
kuendelea kuvumilia.
Rais Kagame aidha amesema Jumuiya ya Afrika
Mashariki imeanza kuwa ghali na mzigo kwa taifa lake akisema mawaziri
katika mataifa wanachama wanatumia jumuiya hiyo kama chombo cha kuchota
pesa kwa kubuni mikutano ya kila siku baadhi akiitaja kuwa haina umuhimu
wowote.
Amesema mawaziri wake wasiopungua watano wanasafiri kama mara
tatu kwa wiki kushiriki mikutano ya EAC popote inapotokea katika nchi
wanachama na kwamba ziara hizo zinaigharimu serikali kitita kikubwa cha
pesa.
“Ni kama mawaziri wa nchi hizi walikubaliana kushinikiza
serikali zao kuwa lazima wahudhurie kila aina ya vikao vya jumuia hii
kwa kisingizio kuwa waziri anayeshindwa kuhudhuria nchi yake
inachukuliwa hatua ama inaonekana kupinga juhudi na mikakati ya
jumuiya,” amesema Rais Kagame.
Moja ya njia alizosema anaweza
kutumia ni kumpa waziri wake wa masuala ya EAC Valentine Rugwabiza
jukumu la kushughulikia masuala yote yanayohusu jumuiya hiyo.
Amepongeza juhudi za Rais wa Tanzania John Magufuli za kukomesha
ufisadi uliokuwa umekithiri katika taasisi za serikali, akisema lazima
na yeye afuate nyayo za Rais Magufuli katika suala zima la kukomesha
ufisadi na ufujaji wa mali ya serikali.
Rwanda
inaorodheshwa ya kwanza katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kupambana na rushwa na ufisadi. Mwandishi
wa BBC Yves Bucyana anasema miaka ya nyuma viongozi kadhaa wa wilaya na
taasisi nyingine za serikali walipoteza kazi zao na kutupwa jela kwa
makosa ya kuhusika na rushwa na ufisadi.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :