KUTOKA KIJIWENI: ILI UFANIKIWE ACHA KUFANYA HAYA
1. Acha tabia ya kuahirisha mambo.
Kama kuna jambo au kitu unachotakiwa kukifanya leoleo ni vizuri ukafanya
kuliko kukiacha na kutegemea utafanya kesho. Wakati wa kubadili maisha
yako upo sasa na wala si kesho kama unavyofikiri. Hiyo kesho
unayoisubiri haitafika na wala hakuna kesho kama unavyofikiri. Ni mara
ngapi umesema utafanya kitu hiki kesho na hukufanya? Hii ni moja ya
tabia inayokuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa unayoyataka. Unataka
kuwa tajiri achana na tabia hii kwanza.
2. Acha tabia ya kufikiria sana makosa uliyoyafanya.
Wengi wanakuwa wanashindwa kusonga mbele kutokana na kufikiria sana
makosa waliyoyafanya siku za nyuma. Kama kuna sehemu ulikosea, hiyo
imeshapita chukua hatua sasa za kusonga mbele. Acha kuumia na
kung’ang’ania kufikiri pale ulipokosea, hiyo haitakusaidia sana zaidi ya
kukurudisha nyuma. Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara kukosea
ni sehemu ya maisha ya binadamu, kitu cha msingi jifunze kutokana na
hayo makosa.
3. Acha tabia ya kuongelea sana ndoto zako.
Watu wengi sana ni waongeaji juu ya ndoto zao lakini sio watendaji. Kama
ni kuongea umeongea sana juu ya ndoto zako, umefika sasa wakati wa
kufanya mambo yako kwa vitendo. Jifunze kuchukua hatua dhidi ya ndoto
zako kila siku, hata kama ni kwa kidogo kidogo utasogea, mwisho
utajikuta unafanikisha kile unachokitaka. Hii ni tabia ambayo imekuwa
ikiwakwamisha wengi kutokana na kuongea sana. Unataka mabadiliko achana
na tabia hii.
4. Acha tabia ya kutokujiwekea akiba.
Hii ni tabia ambayo ukiiendeleza katika maisha yako kutojiwekea kipato
itakuwa ni ngumu sana kwako kufanikiwa. Unaposhindwa kujiwekea kipato
katika pesa unayoipata kitakachokutokea katika maisha yako, utashindwa
kumudu kupata pesa ya kuendeshea miradi yako na mwisho wa siku utakuwa
ni mtu wa kulalamika tu. Kama unataka kuwa tajiri na kuwa huru kifedha
anza kujifunza kujiwekea akiba, hii itakusaidia sana kusonga mbele
katika mambo yako mengi.
5. Acha kutumia pesa zako hovyo.
Watu wengi huwa ni watumiaji vibaya wa pesa zao hasa pale wanapozipata.
Unapotumia pesa zako hovyo hiyo hupelekea kuweza kukosa pesa ambayo
ungeweza kuipata kama akiba yako ya baadae. Mtumizi mabaya ya pesa, ni
moja ya tabia kama tabia zingine, lakini ambayo inakukwamisha kwa kiasi
kikubwa kufikia ndoto na malengo yako makubwa uliyojiwekea. Ili uweze
kusonga mbele na kuachana na majuto uliyonayo jifunze kutunza pesa zako
vizuri, utafanikiwa.
6. Acha tabia ya kuwa na madeni mengi.
Unapokuwa na madeni mengi hiyo itakusababishia badala ya kuendelea mbele
utakuwa unarudi nyuma. Acha kulimbikiza madeni ambayo kwako yanakuwa
mzigo kwako. Kabla hujakopa chukua hatua muhimu ya kujiuliza je, kuna
ulazima wa kukopa hiyo pesa? Madeni ni kitu ambacho kimekuwa
kinawarudisha wengi nyuma bila kujua, kutokana na kuwa na elimu ndogo
inayohusiana na madeni. Unataka kuwa na mafanikio, iache tabia hii mara
moja.
7. Acha tabia ya kusubiri sana kutekeleza ndoto zako.
Hakuna muda sahihi ambao upo wa kuanza kutekeleza ndoto zako kama
unavyofikiri. Muda wa mafanikio na kufanya ndoto zako kuwa za kweli ni
sasa na wala si kesho. Acha kuwa na tabia au fikra za kufikiri kuwa
mipango yako mingi utaiyafanya siku nyingine, hakuna kitu kama hicho.
Hii ni tabia ambayo umekuwa nayo na inakukwamisha. Unataka kutoka hapo
ulipo anza kutekeleza mipango na malengo yako iliyojiwekea mara moja.
Kama una nia ya kweli kutaka kuleta mabadiliko makubwa katika maisha
yako, anza kujiandaa kubadilika wewe kwanza ikiwa ni pamoja na kubadili
hizo tabia ulizonazo zinakukwamisha sana. Kwa kadiri, utakavyoweza
kumudu kubadili tabia zako kwa kiasi kikubwa, ndivyo utakavyo jikuta
maisha yako yanakuwa na mafanikio makubwa kuliko unavyofikiri. Kumbuka
hili, mafanikio yanajengwa na tabia tulizonazo. (Ahsante JF)
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :