KENYA: ALFRED MUTUA, KALONZO MUSYOKA SASA NI PAKA NA PANYA

No comments
Monday, March 14, 2016 By danielmjema.blogspot.com

Sasa ni dhahiri kuwa Gavana wa Machakos, Alfred Mutua na Kiongozi wa chama cha kidemokrasia cha Wiper, Wiper Democratic Movement, ambaye pia ni mmoja wa vinara wa muungano wa CORD, Kalonzo Musyoka hawapiki chungu kimoja. 

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na vita vya chini kwa chini, kati ya viongozi hawa wenye ushawishi mkubwa katika siasa za eneo la ukambani huku kila mmoja akidaiwa kujaribu kupata sapoti ya wananchi wa Ukambani kuelekea uchaguzi mkuu ambapo inadaiwa kuwa Alfred Mutua ameanza kuonesha dalili za kujitokeza kama mpinzani mkuu wa Musyoka katika 'ufalme' wa siasa za Ukambani.

Akizungumza katik amahojiano Rasmi na Mwanahabari Anne Kiguta wa Kituo cha Runinga ya Citizen, hapo jana, Gavana Mutua bila kupepesa macho, alimtuhuma Musyoka kuwa amekuwa akitumia mbinu chafu ikiwemo kuwahonga MCAs kwa lengo la 'kummaliza' kisiasa na kuongeza kwamba hana imani n auongozi wa chama cha Wiper.

“Kalonzo amekuwa akijaribu kunikwaza tangu nichaguliwe kuwa Gavana. amekuwa akiwapigia baadhi ya wajumbe baraza la Kaunti (MCAs) kwa lengo la kunichafua na wako tayari kuthibitisha hilo, sina imani tena na uongozi wa Wiper na simuamini kiongozi wa chama (Kalonzo), kwa sababu kuna muda hunialika tunywe Kahawa, lakini muda huo huo anawapigia MCAs akisuka njama za anguko langu,” alisema Mutua.

Gavana huyo wa Machakos amebainisha kwamba, hafikiri kugombea kiti cha Ugavana kwenye uchaguzi mkuu ujao (mwaka 2017) kwa tiketi ya chama cha Wiper, CORD au Jubilee, huku akifuchua uwezekano wa kusajili vuguvugu alilolianzisha kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo ya Ukambani, hasa watu wa Machakos, Maendeleo Chap Chap Movement, kuwa chama cha siasa na kukitumia kutetea kiti chake.

Alisema licha ya upinzani mkali kutoka kwa Kalonzo na kundi lake (baadhi ya maseneta), idadi sehemu kubwa ya wajumbe wa baraza hilo (MCAs), wanamuunga mkono kwa sababu wanaimani na ajenda yake ya kuleta maendeleo katika eneo la Machakos na eneo lote la Ukambani.
“Katika kambi yangu, niko sambamba na Mbunge wa Mwala, Vincent Musyoka na baadhi ya Wabunge kutoka Makueni, Kitui na Machakos, wengine wanaogopa kuungana nasi kwa sababu ya kuhofia mashambulizi ya Viongozi wa Wiper.”

Mutua pia alifafanua, kitendo cha kutoonekana katika eneo la kazi, Kaunti ya Machakos, kwa muda mrefu ambapo alisema kuwa kutokuwepo kwake kunatokana na safari ya matumaini, aliyoifanya kwa ajili ya kutafuta wawekezaji kwa ajili ya watu wake.
“Nilienda Tanzania, ambayo ni moja ya wabia wetu wakubwa katika maswala ya kibiashara, na lengo la kwenda huko ni kutafuta uwezekano wa kuwa ushirikiano wa kilimo, nikaenda Dubai na Abu Dhabi kutafuta fusra za ajira kwa ajili ya vijana wetu, nilifanikiwa kupata fursa 2,000 za ajira kwa vijana wetu wenye elimu ya Diploma na Uzoefu wa kazi wa miaka mitatu,

“Ashok Leyland nao wamevutiwa na Machakos, ambapo wanampango wa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza magari, hii ni fursa kubwa ya ajira kwa vijana wote kote nchini, viwanda vitatu tofauti vya matunda vina mpango wa kuweka kambi katika kaunti yetu, yote haya ni fursa nzuri za maendeleo."

Mutua alisema ana mpango wa kuleta mabadiliko ya kimaendeleo kwa watu Machakos, na kuongeza kuwa siku za hivi karibuni kutakuwa na vuguvugu la mabadiliko lakini vuguvugu hilo halitatokana na Wiper ya Kalonzo Musyoka. Moto wa mvutano wa kisiasa kati ya Viongozi hawa wawili, ulianza mara baada ya Kalonzo Musyoka kuripotiwa kumshambulia Alfred Mutua akihoji kitendo cha Gavana huyo kutotulia katika Kaunti yake.

Akizungumza kwa mara ya kwanza, kuhusu swala hilo, Kalonzo alisema kitendo cha kutoonekana kwa Mutua kazini kwa muda mrefu kumesababisha Ombwe la uongozi (Leadership vacuum) na kuongeza kwamba majukumu ambayo yalikuwa chini ya Mutua, yametelekezwa. Kwa mujibu wa Naibu Gavana, Bernard Kiala, Mutua amekuwa nje ya Ofisi kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja huku akiacha baadhi ya majukumu ya bila mtu wa kuyahudumia

Chanzo: Citizen TV.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .