SUDAN KUSINI: HALI INAZIDI KUWA MBAYA
Posted in
afrika mashariki
No comments
Friday, March 11, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
Hali ya kibinadamu Sudan Kusini ni mojawapo iliyo mbaya zaidi duniani
huku mauaji ya kiholela katika taifa hilo changa, yakisemekana
kuangamiza maelfu ya maisha ya watu.
Wanaume wanawake na watoto wameuwawa kwa kupigwa risasi, kuchomwa
mishale, kuchomwa moto, kunyongwa, kukanyagwa kwa magari, kuzamishwa
majini, kuachwa bila chakula hadi kufa, kuripuliwa na miili yao kuachwa
mahali itakapoangukia au kufukiwa katika kaburi la pamoja.
Mwaka mmoja wakati wa vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Novemba
mwaka 2014, shirika la kimataifa la kushughulikia mizozo ICG,
linaloangalia hali ilivyo kwa karibu nchini humo, limeliambia shirika la
habari la AFP kwamba watu takriban 50,000 waliuwawa. Mwaka huu Umoja wa
Mataifa nao ukatoa idadi yake sawa na hiyo lakini baada ya muda wa
miaka miwili.
Hata hivyo mtaalamu wa masuala ya Sudan Eric Reeves, ambaye ni
Profesa katika chuo kimoja nchini Marekani, amesema kushindwa kuhesabiwa
vifo vilivyotokea ni ukosefu mkubwa wa maadili na kwamba hiyo huenda
ikamaanisha maisha ya watu wa eneo hilo hayatiliwi maanani au
hayaonekani kuwa na umuhimu.
Kwa upande wao wafanyakazi wa kutoa misadaa ya kiutu ambao hawakutaka
kujulikana wanasema idadi ya waliyofariki huenda ikawa juu zaidi na
kufikia watu laki tatu, idadi ambayo inafanananishwa na watu
waliyofariki nchini Syria katika vita vinavyoingia mwaka wake wa tano.
Wachambuzi watoa maoni yao juu ya mauaji yanayosahaulika Sudan Kusin.
Vifo hivyo vya Sudan Kusini vinajumuisha mauaji yaliyotokana na njaa
kufuatia misaada ya kibinaadamu kuzuwiwa kufika maeneo ya waathirika,
kama vile watu 40,000 ambao Umoja wa Mataifa ulionya kuwa wapo katika
hali mbaya kufuatia maeneo yao kuwa hatari kufikia ili kuangazia pia
hali ilivyo ikiwemo visa vya kikatili kama watu kufungiwa katika mapipa
hadi kufa.
Vile vile vifo hivyo pia vinajumuisha wale waliyoangamia kutokana na
ukosefu wa huduma za matibabu kufuatia kushambuliwa hospitali kadhaa
katika eneo hilo. Madaktari wasio na mipaka MSF wameonya kuwa huenda
kukatokea madhara mengine mengine zaidi kufuatia hospitali zake sita
pamoja na Kliniki kushambuliwa kuvamiwa na kuchomwa moto mara kwa mara.
Aidha wachambuzi wanasema kushindwa kudhibitisha vifo vilivyotokana na
mapigano ya wenyewe kwa wenyewe inachangia mateso ya Sudan Kusini kukaa
nje ya ramani ya kimataifa na kusababisha wanaotenda makosa hayo kukosa
kuadhibiwa.
Lakini huku mapigano yakiendelea licha ya makubaliano ya kusitisha
mapigano yaliyofanyika mwezi Agosti ushahidi wa wale waliyouwawa
unaendelea kupotea. Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights
Watch, lililorekodi makaburi ya halaiki katika mji wa mashariki wa Bor
mwezi wa Januari mwaka 2014 limeonya kuwa ushahidi unaendelea pole pole
kupotea kutokana na makaburi yaliyofichika.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :