TANZANIA: RAIS DKT. JOHN MAGUFULI AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA BENKI KUU (BOT)

No comments
Thursday, March 10, 2016 By danielmjema.blogspot.com

fdf133f1-117d-4631-8f60-160f6d60b301
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara ya kushitukiza katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ambapo pamoja na mambo mengine ameiagiza Benki hiyo kusitisha mara moja ulipaji wa malimbikizo ya malipo ambayo tayari yalishaidhinishwa (Ex-Checker) na badala yake yarejeshwe Wizara ya fedha na Mipango kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki.

Mpaka Rais Magufuli anatoa agizo hilo, Benki Kuu ya Tanzania ilikuwa katika mchakato wa kufanya malipo ya shilingi Bilioni 925.6, ambazo Wizara ya Fedha ilitoa idhini ya kufanyika malipo.

Akizungumza na watendaji wakuu wa Benki Kuu ya Tanzania waliojumuisha Gavana, Naibu Magavana, Wakurugenzi na Mameneja, Rais Magufuli ametaka Wizara ya Fedha ifanye upya uhakiki wa malipo hayo, ili kubaini kama walengwa walioidhinishwa kulipwa wanastahili kulipwa ama vinginevyo.

Aidha, Dkt. Magufuli ameagiza Kitengo cha madeni ya nje ambacho awali kilikuwa chini ya Benki Kuu na baadaye kikahamishiwa Wizara ya Fedha, kirejeshwe Benki Kuu mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni.

Wakati huo huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Beno Ndulu kupitia upya orodha ya wafanyakazi wa Benki hiyo, na kuwaondoa mara moja wale wote ambao hawana ulazima wa kuwa wafanyakazi katika benki hiyo.

"Haiwezekani tukawa na kundi kubwa la wafanyakazi, wanalipwa mishahara wakati hata kazi wanazofanya hazijulikani" Amesema Dkt. Magufuli. Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati ambapo Benki Kuu ya Tanzania ina wafanyakazi 1391.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
10 Machi, 2016.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .