Miaka mitatu tangu afariki, Muziki wake bado unaishi
Posted in
Burudani
No comments
Saturday, May 28, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
SIKU kama ya Leo, mwaka 2013, Tasnia ya Muziki Bongo ilipata pigo kubwa baada ya kuondokewa na Mwanamuziki wa Hip Hop, kipenzi cha watu Albert Magwea ‘Cowwizy’ aliyefariki huko Johannesburg, nchini Afrika Kusini katika Hospitali ya St. Helen akiwa na umri wa miaka 28.
Marehemu Ngwea tunammisi ile mbaya kwenye game la muziki Bongo kutokana na kipaji chake, ameusapoti sana Muziki wa Hip Hop hadi kufikia hapo ulipo leo. Ni kati ya wanamuziki waliofariki wakiwa na umri mdogo mno ukiachana na marehemu Complex, Steve 2K, Mtoto wa Dandu pamoja na Langa.
Hata hivyo, mwanamuziki huyu aliyekuwa mwingi wa swaga ni kati ya wanamuziki vijana waliokuwa wanatengeneza sana maneno mtaani, jina lake tu Ngwea linamaanisha ‘gheto’ kwa vijana lakini zaidi amewashawishi vijana wengi kufanya muziki.
Historia ya Maisha Yake
Albert Magwea alizaliwa jijini Mbeya Novemba 16, 1982, akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto 10 wa baba yake mzazi lakini kwa upande wa mama yake alikuwa ni mtoto wa 6. Akiwa na umri wa miaka 5 familia yake ilihamia Morogoro akasoma katika Shule ya Msingi Bungo, alipofika darasa la tano baba yake alihamishwa tena kikazi hadi mkoani Dodoma.
Akiwa Dodoma, Ngwea alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Mazengo kabla ya kujiunga Chuo cha Ufundi Mazengo baada ya kumaliza elimu yake hiyo ya sekondari. Hata hivyo, Ngwea hakuendelea zaidi kimasomo kutokana na ndoto zake kuwa kwenye muziki.
Kuhusu Muziki
Alianza harakati za muziki mwishoni mwa miaka ya 1990 ambapo mwaka 1999 yeye na washikaji zake Maloga na Moses Bushagama ‘Mez B’ (marehemu) waliokuwa wanaunda kundi lililojulikana kwa jina la CFG (Chamber Fleva Guys) waliachia albamu yao ya kwanza iliyojulikana kwa jina la Heshima Kwa Wote chini ya udhamini wa mwalimu mmoja wa Kikorea aliyekuwa anafundisha Mazengo.
Kumbuka CFG ni kabla ya CS (Chamber Squared), ambapo Chamber Squared ilianzishwa baada ya Maloga ambaye ni muasisi wa Chamber Fleva Guys kuwa ‘bussy’ na masomo Ngwea na Mez B wakaungana na akina Athuman Kabongo ‘Dark Master’ pamoja na Noorah kuunda Chamber Squared.
Baadaye Ngwea alihamia Dar kuendeleza ‘hustle’ za kimuziki ambapo alikutana na washikaji zake wa Chamber Squared ambao walikuwa pia wanaipaisha East Zoo, wakakutana na Prodyuza P Funk Majani aliyewapa shavu la kurekodi ngoma iitwayo Ahadi ya Bosi. Kutokana na uwezo aliouonesha Ngwea kwenye track hiyo, Majani alimchukua kwenye lebo yake ya Bongo Records.
Mwaka 2003, kipindi cha kihistoria kabisa kwenye Muziki wa Hip Hop Bongo kutokana na ushindani wa muziki uliokuwepo, Ngwea aliachia Wimbo Uitwao Geto Langu uliomtambulisha vizuri kwenye gemu la muziki na hiyo ilikuwa ni baada ya kumsindikiza Juma Nature katika ‘tour’ yake ya Albamu ya Ugali.
Baada ya hapo Ngwea alitoa ngoma nyingine zikiwemo Napokea Simu aliyomshirikisha Dully Sykes, Ndani ya Club na Mikasi nyimbo iliyopatikana pia kwenye albamu yake ya A.K.A Mimi iliyokuwa na ngoma nyingine kali ambazo ni Zawadi, Dakika 1, Weekend, She Got a Gwan, Geto Langu, Mademu Zangu, Sikiliza na Napokea Simu.
Hata hivyo, msanii huyu aliyejulikama pia kuwa mkali wa ‘frestyles’ mwaka 2010 aliachia albamu yake ya pili iitwayo Nge, pia alikuza jina lake kwa kushirikishwa kwenye ngoma za wasanii mbalimbali wakubwa nchini ambapo ngoma yake ya CNN ilimpaisha sana.
Alipenda pia hiki! Tofauti na muziki, Ngwea alikuwa anapenda mno kucheza basketball. Mwaka 2000 alifanikiwa kushiriki mpaka mashindano ya kitaifa ya UMMISETA kupitia mchezo huo huko jijini Mwanza.
Kifo
Jumanne ya Mei 28, 2013, taarifa zilisambaa Bongo kuwa Ngwea alifariki akiwa Johannesburg, Afrika Kusini huku madawa ya kulevya yakitajwa kuhusika katika kifo hicho. Hata hivyo, kwa mujibu wa watu wake wa karibu akiwemo M2 tha P, Bushoke walithibitisha juu ya hilo lakini pia ripoti ya madaktari ilieleza sampuli zilizochukuliwa kwenye mwili wake kwa ajili ya vipimo zilikutwa na dawa za kulevya aina ya Heroine, Cocaine chafu pamoja na sumu ya bangi ifikiayo gramu 0.08.
Pia msanii huyo alikutwa na tatizo la kutokula vizuri na kukosa muda wa kupumzika. Ukweli ni kwamba msiba wa Ngwea ulikuwa mkubwa sana nchini na alizikwa nyumbani kwao Kihonda, Morogoro baada ya wiki moja kupita tangu alipofariki dunia.
Msikilize Dark Master!
“Kila ninapomkumbuka mshikaji wangu Ngwea huwa nalia sana. Sitamsahau katika maisha yangu, ninakumbuka ‘goodtime’ yetu wakati Chambe Squared iko ‘hot’. Yeye ameondoka lakini utaona bado nyimbo zake zinaishi, pia namkumbuka Mez B ambaye hatunaye kwa sasa. Chamber inaishilia hivyo,” anasema Dark Master.
GPL
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :