Rais Kenyatta: Wahamiaji Haramu warudi makwao
Posted in
afrika mashariki
No comments
Saturday, May 21, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
Wahamiaji haramu walioko nchini Kenya, kwa takribani miaka 23 sasa, ni sharti warudishwe makwao. Hii ni kwa mujibu wa Rais Uhuru Kenyatta.

“Kama tungekuwa ni watu wakatili na watu wabaya kama baadhi ya watu wanavyotuita, je tungeweza kuwavumilia na kuwakirimu wageni hawa kwa muda wote huu? Bado tunawachukulia majirani zetu Wasomali kama ndugu na marafiki zetu, tunawachukulia kama wabia wetu katika biashara, lakini imefika muda sasa kila mtu arudi nyumbani kwake," alisema Kenyatta.
Rais Uhuru Kenyatta, alisema raia wa Kenya ambao alama zao za vidole vinaonekana katika orodha ya vitabu vya kumbu kumbu ya wahamiaji haramu, hivi karibuni watafanyia utaratibu wa kuwatenganisha na wahamiaji na kisha kupewa vitambulisho vya uraia.
Katika utekelezaji wa utaratibu huo, Rais Kenyatta amewaagiza Machifu na viongozi wa kijadi pamoja na serikali za kaunti kushirikiana katika kuwatambua Wakenya hao ambao majina yao yako kwenye orodha hiyo, ambao majina yao yaliingia huko kwa ajili ya misaada wakati wa kiangazi.
Aidha kutokana na malalamiko ya muda mrefu ya viongozi wa siasa kutoka katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya kuwa vijana wengi hawana vitambulisho vya taifa, Rais Kenyatta alimuagiza Waziri wa mambo ya ndani, Joseph Nkaissery kurudi Garissa kwa lengo la kulipatia tatizo hilo suluhisho la kudumu kwa sababu zoezi hilo ni haki ya kila Mkenya.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais, William Ruto aliwataka wenyeji wa Ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa Kenya kuhakikisha wanadumisha amani kwa kufanya kazi kwa ukaribu na vyombo vya dola kama njia ya kufikia maendeleo ya haraka.
Katika ziara hiyo, Rais Kenyatta na Naibu wake, waliambatana na Waziri wa mambo ya Ndani, Joseph Nkaissery, Waziri wa Maji, Eugene Wamalwa, Adan Mohammed (Viwanda) pamoja na wabunge Aden Duale (Garissa mjini), Gavana wa Garissa Nathif Juma, Elias Bare Shill (Fafi), Shukran Gure (mwakilishi wa wanawake, Garissa), Ibrahim Ahmed Bass (Ijara) na Ferdinand Waititu (Kabete).
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :