Showing posts with label Utamaduni. Show all posts
Showing posts with label Utamaduni. Show all posts

Tamasha la Handeni Kwetu lasogezwa mbele, sasa kufanyika Desemba 20

Tamasha la Handeni Kwetu lasogezwa mbele, sasa kufanyika Desemba 20

Posted in
No comments
By danielmjema.blogspot.com
Na Mwandishi Wetu, Handeni

TAMASHA la Utamaduni la NSSF Handeni Kwetu, sasa litafanyika Desemba 20, badala ya Desemba 13, kama ilivyotangazwa hapo awali, huku sababu kubwa ikiwa ni kuwaachia Watanzania washiriki katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika Jumapili ya Desemba 14 nchini kote.

Mratibu Mkuu wa Tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014, pichani akizungumza jambo katika tamasha la mwaka jana lililofanyika kwa mafanikio makubwa wilayani Handeni, mkoani Tanga.
 
Akizungumzia hilo leo mjini Handeni, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kwamba hatua ya kusogeza mbele kwa wiki moja, ni kutokana na mguso wa tukio lenyewe na nia ya kuwashirikisha Watanzania wote ili kuliweka tamasha lao katika kiwango cha juu.
 
Alisema kuwa Desemba 13 ni siku ya mwisho kwa kampeni za ugombea uenyekiti wa serikali za mitaa, vitongoji na mitaa, hivyo kwa kushauriana na jeshi la Polisi wilayani Handeni, wamekubaliana kulifanya Desemba 20.
 
“Tumeangalia mambo mengi sana hadi kukubaliana lifanyike Desemba 20, ikiwa ni kukosekana kwa wengi, wakiwamo Wakurugenzi ambao kimsingi wao ndio wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo mengi.
 
“Tunaamini kwa kufanyika Desemba 20, tamasha litakuwa kwenye mvuto pamoja na kukwepa malalamiko kwa baadhi ya wanasiasa ambao huenda wangelalamika endapo lolote lingetokea huku wao kushindwa uchaguzi wao,” alisema Mbwana.
 
Mbwana alitumia muda huo kuwaomba radhi wadau wote, wakiwamo wasanii, wadhamini na wale waliokuwa wamepanga kutembelea Handeni Desemba 13, huku akiwataka safari yao ifanyike kwa ajili ya Desemba 20, ukizingatia kuwa wote wanaweza kushiriki chaguzi zao na kupata muda mkubwa wa kutembelea wilayani Handeni na mkoa mzima wa Tanga kumaliza mwaka wao vizuri.
 

 Wadhamini tamasha hilo ni Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.

Machenja ajifua kutoa burudani Tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014

Machenja ajifua kutoa burudani Tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014

No comments
By danielmjema.blogspot.com


NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MSANII wa muziki wa mashairi, Said Machenje, amesema ameanza mazoezi rasmi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa anakuwa mmoja wa wasanii watakaotoa burudani kali katika tamasha la NSSF Handeni Kwetu, linalotarajiwa kufanyika katika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio, mjini Handeni, mkoani Tanga.

Machenje anayeshindana vilivyo na mkali wa muziki huo, Mrisho Mpoto alisema kuwa maandalizi yake yanakwenda sambamba na shauku ya kutembelea kwa mara ya pili wilayani Handeni.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Machenje alisema kwamba mwaka jana alipanda jukwaani kuimba kwa kushirikiana na kikundi cha Naukala Ndima, ila msimu huu amefanikiwa kupata mwaliko wake binafsi.

Mwimbaji huyo wa 'Kajenge kwa Mumeo' na 'Mila', alisema kwa kualikwa binafsi, kunamfanya apate hamu ya kujiandaa kwa ajili ya kufanya mambo makubwa zaidi ili kuonyesha umahiri wake katika tasnia ya muziki wa mashairi.


“Nashukuru Mungu kwa kupangwa kuwa mmoja wa wasanii watakaotoa burudani katika tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014, wilayani Handeni mkoani Tanga kwakuwa ni mwelekeo mzuri katika maisha yangu ya sanaa.

“Nafanya mazoezi makali kwa ajili ya kujiweka sawa ili nifanye shoo nzuri Desemba 13, katika Uwanja wa Azimio, ukizingatia kuwa nina uzoefu sasa na jukwaa la tamasha hili la aina yake,” alisema.

Wadhamini tamasha hilo ni Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.
 
Mwisho
 

Tamasha la Handeni Kwetu lawapigia magoti wadhamini

Tamasha la Handeni Kwetu lawapigia magoti wadhamini

Posted in
No comments
By danielmjema.blogspot.com
 
Na Mwandishi Wetu, Handeni

WADAU wa mambo ya utamaduni yakiwamo mashirika, makampuni na watu mbalimbali wameombwa kujitokeza kuliwezesha tamasha la Handeni Kwetu 2014, lililopangwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Tamasha hilo linafanyika huku mwaka jana likiwezeshwa kwa kiasi kikubwa na Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ushirikiano na wadau mbalimbali walioliwezesha tamasha hilo kwa mara ya kwanza katika Historia ya Mkoa wa Tanga.

Akizungumza mjini hapa, Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kuwa wadhamini wakijitokeza kwa wingi kutaongeza chachu ya maendeleo ya nchi, sanjari na sanaa ya utamaduni inayotakiwa kuungwa mkono na watu wengi.

Alisema kuwa kitendo cha wadhamini kuendelea kuliunga mkono Tamasha hilo kutachangia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa nchi pamoja na kutangaza utamaduni wa Mtanzania.

“Mwaka jana wadau wengi walijitokeza kuliwezesha tamasha la Handeni, wakiwamo NSSF, hivyo tunaomba msimu huu pia tuendelee kushirikiana kuliwezesha Tamasha la Handeni Kwetu litakalofanyika Desemba 13 mwaka huu, Handeni Mjini.

“Hadi wakati huu, walioonyesha nia ya kulisaidia tamasha la Handeni Kwetu 2014 ni pamoja na SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu chao cha Ni Wakati wako wa Kung’aa, Phed Trans, chini ya Yusuphed Mhandeni, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd,” alisema Mbwana.
 
Tamasha la Handeni Kwetu ni miongoni mwa matukio makubwa ya kiburudani mkoani Tanga, ambako zaidi ya watu 500 walihudhuria tamasha hilo ambalo kwa mwaka huu mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa linafanyika kwa mafanikio.
Mwisho
 

KWEINGOMA WAAHIDI UHONDO WA NGOMA YA SELO TAMASHA LA HANDENI KWETU 2014

KWEINGOMA WAAHIDI UHONDO WA NGOMA YA SELO TAMASHA LA HANDENI KWETU 2014

No comments
By danielmjema.blogspot.com

Na Mwandishi Wetu, HANDENI
KIKUNDI cha ngoma cha selo kilichopo katika kijiji cha Kweingoma, wilayani Handeni, mkoani Tanga, kimesema kimepania vikali Desemba 13 mwaka huu kufanya balaa katika tamasha la Handeni Kwetu 2014, litakalofanyika wilayani hapa.

Shauku ya kikundi hicho imetolewa na Kiongozi wao Zaina Selemani, alipozungumzia umuhimu wa tamasha hilo, ambalo mwaka jana walishindwa kushiriki kutokana na wasanii wake wengi kukabiliwa na mambo ya kifamilia, ikiwamo kuugua na kuuguliwa.
Akizungumza kwa furaha kubwa, Zaina alisema ngoma ya selo ni nzuri inayoshawishi kuangalia wasanii wanapokuwa jukwaani, hivyo mashabiki na wadau wote watapata burudani nzuri.

“Mwaka huu tutashiriki kwa nguvu zote kwasababu ni tamasha lililoanza vizuri kwa mkoa huu wa Tanga, maana vikundi vingi kutoka sehemu mbalimbali za Handeni na mkoa wa Tanga vinashiriki,” alisema.

Naye Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kuwa kwa siku kadhaa walikuwa wakifanya ziara kadhaa katika vijiji ambavyo vina vikundi vya ngoma za asili ili vishiriki, hususan vile ambavyo mwaka jana havikushiriki.

“Tunataka kuongeza wigo wa vikundi kutoka ndani ya Tanga na nje pia, ukizingatia kuwa tunahitaji tamasha lenye nguvu na mguso pia ili kukuza sekta ya utamaduni na uchumi wa nchi yetu,” alisema Mbwana.

Tamasha la Handeni Kwetu lililopangwa kufanyika Desemba 13 katika Uwanja wa Azimio (Kigoda Stadium), ni moja ya matukio makubwa mkoani Tanga yanayokutanisha mamia ya watu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania.

TAMASHA LA 'HANDENI KWETU LAPANIA KUVUNJA REKODI YA 2013

TAMASHA LA 'HANDENI KWETU LAPANIA KUVUNJA REKODI YA 2013

No comments
By danielmjema.blogspot.com
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MRATIBU Mkuu wa Tamasha la Utamaduni Handeni, maarufu kama ‘Handeni Kwetu’, Kambi Mbwana, ameapa kuhakikisha kuwa tamasha lao msimu wa 2014 linakuwa la aina yake na kuvunja rekodi ya mwaka jana lilipofanyika kwa mara ya kwanza wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mbwana alisema kuwa hiyo ni kutokana na kutamani kushirikisha wasanii wengi kutoka Tanga na Tanzania kwa ujumla.

Alisema kwamba mwaka jana wasanii zaidi ya 200 walionyesha uwezo wao kutoka kwa vikundi mbalimbali vya wilayani Handeni na jijini Dar es Salaam.

“Mwaka jana vikundi zaidi ya 10 vyenye wasanii wasiopungua 15 walipata nafasi ya kupanda jukwaani kuonyesha vipaji vyao, ukiacha wasanii wanaotoka kwenye Kambi ya jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa Mgambo waliozidi 80.

“Wakati tunajivunia mafanikio haya, tunaamini msimu huu utakuwa mzuri zaidi tukiamini kuwa tutavunja rekodi ya mwaka jana, ambapo tulishuhudia burudani mbalimbali, ikiwamo hadithi zilizohusu watu wa Handeni, bila kusahau vyakula vya asili pamoja na michezo waliyokuwa wakicheza wazee wetu enzi hizo,” alisema Mbwana.

Kwa mujibu wa Mbwana, mipango ya kuboresha tamasha hilo imepamba moto ambapo kwa sasa utafiti wa ubora wa vikundi nje ya wilaya ya Handeni inafanywa ili kuhakikisha kuwa wasanii watakaopanda jukwaani wanakuwa na uwezo wa juu na kufanikisha kwa dhati kukuza sekta ya utamaduni pamoja na uchumi wa Tanzania.

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .