MWENYEKITI WA HAI ATOA KAULI MGOGORO WA MADIWANI NA HALMASHAURI YA HAI
Posted in
No comments
Thursday, September 6, 2012
By
danielmjema.blogspot.com
![]() |
| MWENYEKITI KWAYU KATIKA MOJA YA SHUGHULI ZA BUMACO INSURANCE |
PRESS RELEASE
KUTOKA KWA
MWENYEKITI, HALMASHAURI YA HAI
5,SEPTEMBA,2012
MSIMAMO WA
MWENYEKITI KUHUSU KUAHIRISHWA KWA KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI 30,AGOSTI,2012.
Habari
zimeenezwa kuwa baadhi ya madiwani, hususan wale wa CHADEMA walisusia kikao cha
Baraza la Halmashauri cha tarehe 30.8.2012 na hivyo kusababisha kikao
kuahirishwa. Ukweli ni kuwa mimi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai nilikifuta
kikao hicho na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai awaarifu madiwani wote
juu ya jambo hili. Aidha Mkurugenzi alishauriwa aandae kikao kingine kwa tarehe
5 au 6 Septemba 2012 kwa barua mbili za tarehe 27 na 29 Agosti 2012. Mkurugenzi
aliendelea kukaidi agizo na ushauri huo.
Nilisikitishwa
sana na barua ya Mkurugenzi ya 29/8/2012 iliyosisitiza kuwa tarehe ya kikao ibaki tarehe 30/8/2012. Hatima yake ni kikao kilichovunjika baada ya
Halmashauri kuingia gharama zisizo za lazima.
Mapema
mwezi Agosti Mkurugenzi alikataa kwa nguvu zote kushiriki nami kuandaa kikao
cha Baraza. Baada ya kushindwa kumpata
ofsini au kwa simu yake, nilimwaandikia SMS tarehe 13 August 2012 kumtaka awasiliane na mimi ili kati ya mambo mengine
tupange kikao cha Baraza ambacho kingeliwajummuisha madiwani wote. Hakuniona.
Badala yake tarehe 14/8/2012 alisambaza barua ya kuitisha kikao cha pre-baraza
tarehe 22.8.2012 na kikao cha Baraza tarehe 23.8.2012. Vikao hivi viliahirishwa kwa simu na
Mkurugenzi masaa machache kabla ya kikao. Baadhi ya wajumbe walihudhuria
wakaambulia patupu. Sababu kubwa ya kuahirisha ilikuwa ni ili kuruhusu baadhi
ya madiwani wetu washiriki katika chaguzi za CCM (jumuiya ya wazazi na UWT).
Pamoja na udhaifu wa taarifa hizi niliona ni vema wenzetu kushiriki katika chaguzi hizo.
Mnamo
tarehe 22.8.2012 Mkurugenzi alisambaza barua za Wito wa Mkutano wa Mwaka wa Baraza
la Halmashauri wa tarehe 30/8/2012. Mapema 23.8.2012 nilimwendea Mkurugenzi
kumshauri asitishe kikao hicho kwa sababu kuu mbili.
- Unyeti wa zoezi la kitaifa la Sensa na majukumu waliyokabidhiwa madiwani ya kuhamasisha na kufanikisha sensa ya watu na makazi. Hata wakati wa kusambaza barua hizo madiwani wakishiriki na Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine walikuwa katika kazi nzito ya kuhamasisha na kufundisha wananchi maana na umuhimu wa sensa na kuwasihi washiriki kikamilifu. Barua ya tarehe 14.8.2012 iliwataka madiwani wawe na ratiba ya zoezi hilo. Tarehe ya mkutano iliangukia wiki ya sensa. Kwa mtu mwenye akili na uzalendo wa nchi ataelewa uzito wa zoezi hili kwa taifa zima.
- Mbunge wa Jimbo hangeliweza kushiriki katika kikao hicho cha mwaka. Kwangu mimi Mkutano wa Baraza wa Halmashauri ni jambo muhimu sana. Unajumuisha shughuli zote zilizofanyika tangu Halmashauri iingie madarakani na unaweka malengo ya vipindi vinavyofuata. Mbunge akiwa mwakilishi wa wananchi wote wa Hai bungeni anastahili aelewe hali ya wilaya kwa ujumla wake na hakuna mahali pengine popote atakapoweza kupata undani huo zaidi ya kwenye Baraza la mwaka la madiwani.
Mkurugenzi
alipuuza mambo haya yote mawili. Mimi niliona umuhimu wa mambo haya, na kama
Mwenyekiti nilimuagiza Mkurugenzi asitishe
kikao hicho na kukihamishia wiki ifuatayo baada ya wiki ya sensa kwa tarehe 5
au 6 Septemba.
Baada
ya kikao cha tarehe 30/8/2012 kushindwa kufanyika, nilitazamia Mkuregenzi aitishe
kikao hicho kwa tarehe nilizomshauri, yaani tarehe 5 au 6 septemba. Hakufanya
hivyo. Nilirudia agizo langu mara mbili, moja kwa barua na lingine kwa SMS.
Yeye amejibu kwa SMS kuwa ameshamwaandikia mkuu wa mkoa na hivyo anasubiri
maelekezo yake.
Shauri la kupanga na kuairisha mikutano ya
baraza na mikutano mingine katika
Halmashauri ni jambo la kawaida. Ikiwa mkutano wa tarehe 30 ulishindikana,
ushauriano kati ya Mwenyekiti na Mkurugenzi ungeliweza kupanga kikao kingine
bila malumbano yeyote. Mkurugenzi analifanya hili jambo dogo kuwa mgogoro
katika Halmashauri. Kwake kichuguu ni
mlima. Isitoshe yeye anapenda kupanga na kupangua mikutano ya Halmashauri mwenyewe
na kumwarifu mwenyekiti kwa simu dakika za mwisho. Huu sio utaratibu,
wala kanuni wala busara za kuendesha Halmashauri. Kamwe Mkurugenzi hawezi kuwa mwamuzi wa
mwisho wa vikao vya Halmashauri.
Kwa
kifupi hakuna mgogoro Hai.
Mkurugenzi Mtendaji wa BUMACO INSURANCE NA MWENYEKITI WA HAI
CLEMENCE KWAYO
mwisho............
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako



0 MAOINI :