THE RISE AND FALL OF ABOUD JUMBE MWINYI (sehemu ya pili)

No comments
Sunday, April 10, 2016 By danielmjema.blogspot.com


KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya, tuliona jinsi Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, alivyopaa kutoka nafasi ya Waziri wa Nchi (Mambo ya Mungano) kabla ya mwaka 1972, hadi kuwa Rais wa Zanzibar mwaka huo, katikati ya upinzani mkali kutoka kwa watetezi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, na namna alivyojitengenezea kitanzi mwenyewe baadaye kuelekea anguko kuu.



Tuliona pia jinsi alivyoanzisha mapambano kati yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika harakati za kutaka kujiponya na anguko hilo, kwa kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuwa chukizo kwa Mwalimu ambaye naye aliandaa kipigo kizito cha kumnyamazisha.  Kipigo hicho kilikujaje? Fuatana nami kupata jibu katika sehemu hii ya pili na ya mwisho ya makala haya.

Jumbe aandaa mashitaka dhidi ya Muungano

Kwa kumtumia Alhaj Bashir K. Swanzy, raia wa Ghana aliyemteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kushika nafasi ya Damian Lubuva, na kumpa uraia kwa njia ya usajili, Rais Jumbe aliandaa Hati ya Mashtaka kuhoji muundo na uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalum ya Kikatiba ya Jamhuri ya Muungano, ambayo kwa mujibu wa Ibara ya 125 na 126 ya Katiba ya Muungano ya mwaka 1977, kazi yake pekee (nanukuu) “ni kusikiliza shauri lililoletwa mbele yake na kutoa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba; iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”

Katika hili, Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Wolfgang Dourado (sasa marehemu), naye alishirikishwa.  Hata hivyo, Hati hiyo ya mashitaka ilipotea mezani kwa Rais Jumbe katika mazingira ya kutatanisha, na hatimaye kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere (Ikulu, Tanzania Bara).

Mbali na Hati ya Mashtaka, Rais Jumbe aliandika pia barua ndefu kwa Mwalimu kubainisha jinsi Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano zilivyoendelea kukiukwa na utawala wa nchi, na kuhoji pia mantiki ya kuunganishwa kwa TANU na ASP kuunda CCM, na mamlaka turufu Chama hicho kiliyojipa kusimamia Muungano, wakati vyama vya siasa si jambo la Muungano.

Kwa msaada pia wa Jaji Swanzy, Rais Jumbe alifanya rejea kwa kuhoji uhalali wa Sheria Namba 18 ya mwaka 1965, iliyoahirisha kwa kusogeza mbele muda wa kuitisha Bunge la Katiba, ubabe wa Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1965 na ubatili wa Katiba ya Kudumu ya mwaka 1977 kwa namna ilivyobuniwa na kutungwa bila kuzingatia matakwa ya Mkataba na Sheria ya Muungano.

Kwa kuwa barua hiyo iliandikwa kwa lugha ya Kiingereza, alimwagiza aliyekuwa Waziri Kiongozi wake, Ramadhan Haji, ahakikishe imetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili iweze kujadiliwa kikamilifu kwenye Baraza la Mapinduzi.

Kabla ya hapo, akihutubia kwenye kilele cha Sherehe za Mapinduzi Zanzibar, Januari 12, 1984, Rais Jumbe alionyesha kukerwa na jinsi Muungano ulivyokuwa ukiendeshwa na kuwataka Wazanzibari wavute subira wakati tatizo hilo likishughulikiwa, na kwamba bila ya mwafaka na maridhiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Muungano juu ya muundo sahihi wa Muungano, Zanzibar ingekwenda Mahakamani.

Kwa mara nyingine, kama ilivyopotea Hati ya Mashitaka katika mazingira ya kutatanisha, ndivyo pia barua hiyo ndefu ilivyopotea hata kabla Rais Jumbe Mwinyi hajaitia sahihi na kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere.

Kwa kuona hatari mbele yake, haraka haraka kikaitishwa kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM mjini Dodoma kumjadili Rais Jumbe kwa dhambi kuu ya kuthubutu kutua mahali ambapo ‘Malaika’ waliposhindwa kutua.

Humo ndani ya kikao, mizinga ikalia. Mizinga ya piga nikupige, huku kambi mbili za Kizanzibari zikiumana kutaka kuangamizana. Kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ (Frontliners) ilitaka Rais Jumbe atoswe, huku ikimwelezea kama msaliti wa Muungano, kiongozi dhaifu na asiyekubalika Visiwani, mbinafsi na mwenye makundi.

Kambi ya pili, ya ‘Wakombozi’ (Liberators), iliona Rais Jumbe anazushiwa mengi na wabaya wake, wapinga Mapinduzi wasioitakia mema Zanzibar. Kanali Seif Bakari (marehemu), ambaye wakati huo alikuwa pia Naibu Waziri wa Ulinzi, alijitahidi mno kumwokoa Rais Jumbe kikaoni humo bila mafanikio, lakini baadaye akaishia kuwekwa chini ya ulinzi nyumbani, na hatimaye kutiwa kizuizini Tanzania Bara kwa zaidi ya miezi sita.

Kwa kutumia kofia yake ya Mwenyekiti wa CCM, na kwa kutumia pia udhaifu wa Wazanzibari, kama ulivyojidhihirisha wakati huo kwa utengano wao, wivu na chuki miongoni mwao kwa wao, ilikuwa rahisi kwa Mwalimu kumtungua Rais Jumbe bila sauti ya umoja kutoka Zanzibar, na saa ilipowadia; akavuliwa nyadhifa zake zote za uongozi kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza ya makala haya.

Tetemeko na mafuriko yakawakumba pia wasaidizi wake wa karibu, wakiwamo aliyekuwa Waziri Kiongozi, Ramadhani Haji; Waziri wa Nchi wa Zanzibar, Aboud Talib, ambapo Mwanasheria Mkuu Mteule wa Rais Jumbe, Jaji Bashir Swanzy, alifukuzwa Zanzibar kwa taarifa ya saa 24 na kurejeshwa kwao Ghana.

Naye Jaji Dourado, kama ilivyokuwa kwa Rais Jumbe na Kanali Seif Bakari, aliwekwa kizuizini kwa miezi sita, kisha ikatangazwa sawia hali ya hatari kisiasa, maarufu kama ‘kuchafuka kwa hali ya hewa Visiwani.’ Mambo ya Usalama wa Taifa, ambayo kabla ya hapo hayakuwa jambo la Muungano (ilikuwa ni Ulinzi tu), yakaingizwa kwenye Katiba kuwa jambo la Muungano, na kwa hiyo ikasomeka ‘Ulinzi na Usalama’ ili kudhibiti zaidi hali hiyo. Kufikia hapo, ilikuwa ushindi mkubwa kwa kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ dhidi ya kambi ya ‘Wakombozi.’ 

Mwandishi wa makala haya, ambaye alikuwa mmoja wa Vijana wa CCM kutoka Tanzania Bara, walioshiriki kwenye zoezi la kulegeza na kudhibiti mkakamao wa hali hiyo tete Visiwani, kwa lengo la ‘kusafisha’ hewa iliyochafuka, alishuhudia jinsi kambi hizi mbili zilivyokamia kuumizana, licha ya Zanzibar kupata Rais mpya, Sheikh Ali Hassan Mwinyi; huku kambi ya ‘Wakombozi’ iliyoshindwa ikiapa kulipiza kisasi kwa ‘Wanamstari wa mbele’ na kwa Mwalimu Nyerere pia. Nafasi hiyo ilikuja pale Mwalimu Nyerere alipotangaza nia yake ya kung’atuka mwaka 1985 na kutafuta mrithi wake.

Nyerere aandaa mrithi wake

Kifo cha Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine, ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Dk Salim Ahmed Salim, kilimweka Mwalimu njia panda kuhusu uteuzi wa mrithi wake baada ya yeye kung’atuka. Ili kuweka mzani wa kidiplomasia za kimuungano sawa na kwa lengo maalum, iliazimiwa kwamba Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano, atoke Zanzibar.

Na katika kutekeleza lengo hilo, nafasi za wagombea zilidhibitiwa kuwa watatu tu. Nao walikuwa ni Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Muungano na pia Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Ali Hassan Mwinyi; Waziri Mkuu wa Muungano na Mjumbe wa NEC na Kamati Kuu (CC)  ya CCM, aliyekuwa na nguvu kubwa kisiasa wakati huo, Dk Salim Ahmed Salim; na Mjumbe mwingine wa NEC na CC, aliyekuwa na nguvu kubwa pia kisiasa, Rashid Mfaume Kawawa.

Ukimwacha Kawawa ambaye alikuwa anatokea Bara, Mwinyi na Dk Salim ndio pekee walikuwa Wazanzibari, na hivyo kufifisha dhamira nzima kwamba Rais wa Awamu ya Pili atoke Zanzibar. Mwinyi, pamoja na kuzaliwa Kisarawe (Tanzania Bara), alikulia na kusomea Zanzibar. Na kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Mtanzania yeyote aliyeishi Zanzibar kwa miaka sita mfululizo, anastahili kuitwa Mzanzibari; na ndivyo ilivyokuwa kwa Mwinyi.

Mwalimu Nyerere alikuwa na mtihani mgumu kumpata mrithi kutokana na vigogo hao watatu waliokuwa na sifa na nguvu sawa katika siasa za Tanzania enzi hizo. Kwa hiyo, akaanzisha mchezo wa karata na ushawishi katika ngazi za juu za Chama, lakini bila rushwa wala matumizi ya fedha kama ilivyo siku hizi ndani ya CCM.

Ikumbukwe kwamba katika ngazi hizo za juu, kwa maana ya NEC na CC ya CCM, zilikutanishwa kambi mbili zenye kuhasimiana juu ya ukuu wa kisiasa Zanzibar. Kambi hizo zilikuwa ni zile zile za ‘Wakombozi’ (Liberators), iliyoongozwa na Brigedia Abdullah Said Natepe. 

Wengine walikuwa ni Ali Mzee (aliyekuwa Waziri wa Nchi (Serikali ya Muungano), Hassan Nassoro Moyo (aliyekuwa Waziri wa Kilimo Zanzibar), Mohammed Seif Khatib (aliyekuwa Katibu Mkuu na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM), pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Muungano, Dk Salmin Amour Juma.

Kambi hii ilikuwa pia na maofisa wastaafu wa Jeshi na Usalama wa Taifa. Hao walikuwa ni pamoja na Brigedia Mstaafu na Waziri Kiongozi wa zamani, Ramadhan Haji (aliyeng’olewa pamoja na Jumbe) na Mkuu wa Jeshi la Zanzibar, Brigedia Khamis Hemed.

Kambi hiyo ya Wakombozi ilikuwa bado ikipiga kampeni kushinikiza kuachiwa kutoka kizuizini mtu wao, Kanali Seif Bakari, pamoja na Mjumbe mwingine wa zamani wa Baraza la Mapinduzi, Hafidh Suleiman, ambao hao wawili walikuwa sehemu ya watesi maarufu (Genge la watu 14) na vinara wa ukiukaji wa haki za binadamu na mauaji enzi za utawala wa Abeid Amani Karume.

Kwa upande wa kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ ilikuwa na Dk Salim Ahmed Salim, Seif Shariff Hamad (wakati huo Waziri Kiongozi), Hamad Rashid) wakati huo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Muungano) na Khatib Hassan. Wengine walikuwa ni Kanali Adam Mwakanjuki, Isaac Sepetu, Shaaban Mloo, Ali Salim na Ali Haji Pandu, ambao wote walikuwa Wajumbe wa NEC ya CCM.

Kambi ya ‘Wakombozi’ ilijua mapema chaguo la Mwalimu Nyerere ni Dk Salim Ahmed Salim kuwa kumrithi wake. Kambi hiyo ikaona hiyo ilikuwa ni nafasi nzuri kulipiza kisasi kwa majeraha iliyopata kutokana na mtu wao Aboud Jumbe, kuondolewa madarakani.

Mwalimu akwaa kisiki kuteua mrithi

Tangu mwanzo, kambi hii ya ‘Wakombozi’ ilikuwa na chuki ya kudumu dhidi ya Dk Salim kwa sababu za kisiasa na kijamii. Mwaka 1982, wakati Dk Salim alipoteuliwa na Mwalimu kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Brigedia Natepe (wakati huo akiwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Usalama wa Taifa) na Ali Mzee (wakati huo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais), walikwenda kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Sokoine, wakadai kwamba walikuwa na maagizo kutoka kwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe na Kanali Seif Bakari, ya kuzuia Dk Salim asiwe Waziri wa Mambo ya Nje.

Walitoa sababu mbili. Mosi, kwamba kuna makubaliano ya siri tangu enzi za Karume, kwamba wanachama wa zamani wa vyama vya zamani vya siasa mbali na ASP, na ndugu zao, wasipewe nafasi za uongozi katika Chama, Serikali ya Zanzibar wala katika Serikali ya Muungano; bali watumike kwa shughuli za kitaalam tu.

Dk Salim alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa chama cha siasa cha mrengo wa kushoto (Ki-Marxist/Kikomunisti) cha Umma Party kilichofanikisha Mapinduzi ya 1964 kwa kushirikiana na ASP, kisha akateuliwa na Karume kuwa Balozi wa Zanzibar nchini Misri, chini ya Serikali ya mseto kati ya ASP na Umma Party. Pili, walidai kwamba rangi ya ngozi ya Dk Salim iliwakumbusha Wazanzibari, kwa kilio cha kusaga meno, utawala wa Sultani aliyepinduliwa Januari 12, 1964.

Sokoine, Waziri Mkuu ambaye hakupenda mzaha wala majungu, aliwafukuzia mbali viongozi hao. Kuanzia hapo, nyota ya Dk Salim ilizidi kung’ara na hatimaye kumrithi Sokoine alipofariki kwa ajali ya gari miaka minne baadaye.

Mikakati ya ‘Wakombozi’ kumzuia Dk Salim asimrithi Mwalimu Nyerere ilikuwa thabiti ikihusisha vigogo wa Visiwani na Bara pia. Wasukaji wa mikakati Visiwani, walikuwa ni Hassan Nassoro Moyo, Natepe, Ramadhan Haji na Aboud Talib, kwa kumshirikisha mwanamkakati kiungo chao Tanzania Bara, Waziri wa Utalii wa wakati huo, Paul Bomani, aliyeunda na kuongoza kikosi cha Wajumbe wa NECwa Bara dhidi ya Dk Salim.

Mwalimu Nyerere alijua yote haya, lakini hakujihusisha kupiga kampeni kwa kuheshimu demokrasia na misingi ya uongozi bora. Mwinyi alifuatwa na ‘Wanamstari wa mbele’ siku ya uteuzi na kushauriwa, naye akakubali, kujitoa katikati ya mchakato ili kumwachia Mzanzibari mwenzake, Dk Salim.

Walidhani wamemshawishi vya kutosha kufikia uamuzi huo, lakini mambo hayakuwa kama walivyotarajia siku ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM cha kuteua mgombea, hapo Agosti 12, 1985. Kawawa, kama ilivyotarajiwa, alijitoa kugombea, kwa hiyo wakabakia wawili. Mwinyi na Salim wakatoka nje ili wajadiliwe, lakini hadi hapo bila dalili zozote za Mwinyi kujiengua.

‘Wakombozi’ wa Visiwani na maswahiba wao wa Bara, walitumia vizuri nafasi waliyopewa na hivyo kutawala mazungumzo, huku Moyo na Natepe wakiongoza. Mjumbe mwingine aliyezungumza, alikuwa Getrude Mongella, wakati huo akiwa pia Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (kikulacho kinguoni mwako?) na mpambe mku wa Bomani kwa kampeni za Bara.

Hoja ya Mongella ilikuwa kwamba kumwacha Mwinyi ambaye alikuwa Makamu wa Rais na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, na kumteua Dk Salim, kungetafsiriwa vibaya kitaifa na kimataifa kwamba Watanzania hawaheshimiani kiuongozi. Kamati kuu ikamteua Mwinyi. Kambi ya ‘Wakombozi’ ikachekelea kwa ushindi.

Bado ilitarajiwa kuwa Mwinyi angejitoa baada ya hapo, lakini hakufanya hivyo. Akajikausha chini ya mkazo wa macho ya ‘Wanamstari wa mbele’ waliotarajia afanye hivyo. Kinyume chake, alipojulishwa juu ya kuteuliwa kwake kikaoni humo, jibu lake lilikuwa rahisi na fupi. 

Alisema: “Kama hayo ndiyo matakwa ya watu, nakubali.” Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere hakupinga. Tayari alikuwa amekwaa kisiki cha ‘Wakombozi,’ wakafanikiwa kulipiza kisasi chao kwake.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .