ZANZIBAR: MAALIM SEIF AZUNGUMZA HAYA KUHUSU SIASA NA HATMA YA WAZANZIBARI
Posted in
afrika mashariki
No comments
Sunday, April 10, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
HOTUBA YA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI – PARK HYATT ZANZIBAR, TAREHE 10 APRILI, 2016
Ndugu zangu Waandishi wa Habari,
Ndugu Waalikwa,
Ndugu Waalikwa,
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na
uzima tukaweza kukutana hapa leo. Namshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa
kuijaalia nchi yetu kwa kiasi kikubwa kubaki katika hali ya amani na
utulivu licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa
na baadhi ya watu za kuivuruga amani yetu.
Naendelea kumuomba Mola wetu
aendelee kuibariki nchi yetu na watu wake, aijaalie kuwa nchi ya amani
na atujaalie hekima na busara katika kuendesha mambo yetu. Nichukue fursa hii pia kukushukuruni nyinyi waandishi wa habari kwa
kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza.
Shukrani maalum zije kwenu wale
ambao mmesafiri kutoka Dar es Salaam na kuja Zanzibar makhsusi kwa
ajili ya mkutano huu. Tunathamini sana mashirikiano yenu nyote
tukitambua nafasi na mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika
maendeleo ya nchi yoyote ile.
Mtakumbuka kwamba siku saba zilizopita tulizungumza nanyi ambapo
tuliwasilisha kwenu maazimio 13 ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
Chama Cha Wananchi (CUF) kuhusiana na msimamo wa Chama chetu dhidi ya
ubakaji wa demokrasia Zanzibar uliofanyika tarehe 20 Machi, 2016 na
ambao ulipewa jina la uchaguzi wa marudio.
Leo hii tumekuiteni ili kutimiza agizo nililopewa na Baraza Kuu
lililonitaka nizungumze na wananchi wa Zanzibar ili kuwaeleza kwa kina
mwelekeo wa hali ya kisiasa ya Zanzibar na hatua zinazochukuliwa na CUF
kuhakikisha maamuzi halali ya kidemokrasia ya Wazanzibari waliyoyafanya
tarehe 25 Oktoba, 2015 yanaheshimiwa.
UCHAGUZI WA TAREHE 20 MACHI, 2016
Nilieleza kwa urefu katika mkutano wangu na waandishi wa habari wa tarehe 11 Januari, 2016 nilioufanya Dar es Salaam juu ya nini kilitokea baina ya tarehe 25 Oktoba 2015 hadi tarehe 28 Oktoba, 2015, siku ambayo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alitoa tangazo batili na haramu la kufuta uchaguzi huru na wa haki uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015. Nilieleza pia hoja za kikatiba na kisheria za kwa nini tangazo lile ni haramu na batili na hoja zile hadi leo watawala wameshindwa kuzijibu.
Nilieleza kwa urefu katika mkutano wangu na waandishi wa habari wa tarehe 11 Januari, 2016 nilioufanya Dar es Salaam juu ya nini kilitokea baina ya tarehe 25 Oktoba 2015 hadi tarehe 28 Oktoba, 2015, siku ambayo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alitoa tangazo batili na haramu la kufuta uchaguzi huru na wa haki uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015. Nilieleza pia hoja za kikatiba na kisheria za kwa nini tangazo lile ni haramu na batili na hoja zile hadi leo watawala wameshindwa kuzijibu.
Kwa hoja hizo hizo, nikaeleza kwamba hakuna
vifungu vya Katiba wala Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984
vinavyozungumzia kitu kinachoitwa uchaguzi wa marudio ukiondoa pale
inapotokea wagombea wanapopata idadi sawa ya kura. Sikusudii kurudia yale ambayo nilishayaeleza siku ile maana hayo sasa yanaeleweka na kila mtu ndani na nje ya nchi.
Leo hii nataka niwapongeze kwa mara nyengine tena wananchi jasiri na
shupavu wa Zanzibar kwa kuitumia tarehe 20 Machi, 2016 kukifedhehesha
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mara ya pili ndani ya miezi sita mbele ya
macho ya Watanzania na mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa.
Wananchi
wazalendo wa Zanzibar wanaoipenda nchi yao waliwakataa watawala waovu wa
CCM na sera zao mbovu zinazoidhalilisha Zanzibar yao kupitia sanduku la
kura tarehe 25 Oktoba, 2015. Watawala waovu wa CCM wakaamua kutumia
mabavu na uvunjwaji wa katiba na sheria kuyapindua maamuzi ya
Wazanzibari, kwa sababu tu maamuzi hayo yalikuwa ni ya kuwakataa
watawala hao.
Kwa miezi mitano kuanzia Oktoba 2015 hadi Machi 2016, watawala waovu
wa CCM wakawaingiza wananchi watulivu na wanaopenda amani wa Zanzibar
katika idhilali na hilaki kubwa kwa kuwazuilia haki zao za msingi za
binadamu ili wasiweze kuonesha hisia zao dhidi ya watawala.
Kwa namna ya
pekee na ya ustaraabu wa hali ya juu na wa kupigiwa mfano, wananchi wa
Zanzibar wakaisubiri tarehe 20 Machi, 2016 na wakapeleka ujumbe wao kwa
watawala hao na kwa dunia nzima kwa njia za amani za kuususia uchafuzi
ulioitishwa siku hiyo. Hali halisi iliyoonekana na kila aliyetaka kuona
ni kwamba zaidi ya asilimia 80 ya Wazanzibari hawakwenda kupiga kura
siku hiyo ili kuonesha hisia zao na kuthibitisha tena maamuzi yao ya
tarehe 25 Oktoba, 2015.
Kituo cha televisheni cha ITV kilichokuwa kikirusha matangazo ya moja
kwa moja kutoka katika mikoa mitano ya Unguja na Pemba kilionesha vile
vilivyoitwa vituo vya kupigia kura vikiwa havina watu kabisa au vikiwa
na watu wachache sana. Walipowahoji wale walioitwa maofisa uchaguzi na
walioitwa mawakala kila mmoja alikuwa akija na majibu yake na takwimu
zake zinazopingana na za mwenzake. Vituo vya televisheni vya kimataifa
hasa kile cha Al-Jazeera na CCTV ya China vilionesha na kuripoti vituo
vikiwa vitupu.
Hata televisheni ya watawala ya ZBC ilikuwa ikipata
kigugumizi kuonesha hali ilivyokuwa katika vile vilivyoitwa vituo vya
kupigia kura hadi kuamua kukatisha matangazo ya moja kwa moja. Magazeti
ya Tanzania na ya nje ya nchi yaliripoti na kuchapisha picha
zilizoonesha kususiwa kwa uchafuzi huo ulioitishwa na watawala wakidhani
wanajihalalishia haramu yao.
Mitandao ya kijamii nayo ilijaa maelezo na
vielelezo kutoka watu na taasisi za kimataifa zinazoheshimika
vikionesha hali halisi ilivyokuwa na ujasiri wa Wazanzibari wa kuususia
uchafuzi huo. Na hatimaye nchi 16 zikatoa taarifa yao tarehe 21 Machi,
2016 wakieleza kwamba uchaguzi huo haukuwa wa kuheshimika kwa sababu
haukuwa shirikishi na wala haukuwakilisha matakwa ya wapiga kura wa
Zanzibar.
Nitumie fursa hii kwa mara nyengine tena kuwapongeza wananchi wote wa
Zanzibar kwa ujasiri, uzalendo na ari kubwa walioionesha kwa kuitikia
kwa kiasi kikubwa wito wa chama chao cha CUF wa kuwataka wasishiriki
katika uhuni na ubakaji wa demokrasia uliopewa jina la uchaguzi wa
marudio wa tarehe 20 Machi, 2016, na hivyo kuudhihirishia ulimwengu
kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina ridhaa ya wananchi wa Zanzibar.
Naungana na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kuwapongeza
waliokuwa wagombea wenzangu wa CUF kwa nafasi za Uwakilishi na Udiwani
kwa kusimama na wananchi wa Zanzibar na kutoshiriki katika uchaguzi huo
haramu na batili wa marudio, jambo ambalo limethibitisha kwamba hawapo
kwa ajili ya kutaka nafasi na vyeo binafsi bali wanachotaka ni kuleta
mabadiliko ya kweli kwa maslahi ya watu wote wa Zanzibar.
Pongezi zangu za dhati kabisa zinakwenda kwa wagombea Urais,
Uwakilishi na Udiwani wa vyama vyengine vya upinzani ambavyo ni NRA,
DEMOKRASIA MAKINI, SAU, UMD, JAHAZI ASILIA, CHAUMMA, UPDP, DP, na
ACT-WAZALENDO, na vile vinavyoshirikiana kupitia UKAWA ambavyo ni
CHADEMA, NCCR na NLD kwa kuungana pamoja na Wazanzibari kutetea
demokrasia yao.
CCM WANAPENDA NAMBA LAKINI HAWAJUI HESABU
Jambo moja ambalo CCM wamejifedhehesha wenyewe ni lile la kutangaza kile walichokiita matokeo ya uchafuzi wao bila ya kuzingatia kwamba takwimu zina sifa moja, huwa hazisemi uongo. Vijana wana msemo wao siku hizi; wanasema CCM wanapenda namba lakini hawajui hesabu. Matokeo ya tarehe 20 Machi, 2016 waliyoyatangaza ni kwamba eti jumla ya watu waliopiga kura walikuwa 341,865 na kwamba Dk. Ali Mohamed Shein eti alipata kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.
Takwimu za uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 zilionesha kwamba
jumla ya wananchi waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni 402,354 na Dk.
Ali Mohamed Shein alipata kura 182,011 sawa na asilimia 46.28.
Wakati huo huo kwa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzaia, wapiga kura kwa upande wa Zanzibar walikuwa 417,882 ambapo
mgombea wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli alipata kura 194,317 sawa na
asilimia 46.5.
Kwa hivyo, kwa kutumia takwimu hizi, mtu anapochukua takwimu hizi na
kulinganisha wapiga kura 402,354 waliojitokeza tarehe 25 Oktoba, 2015 na
wale wanaodai eti walijitokeza tarehe 20 Machi kwamba ni 341,865
watawala wa CCM walichotaka kutuaminisha ni kwamba tofauti ya waliokuwa
hawakujitokeza kupiga kura ilikuwa ni 60,489 tu. Suala la kujiuliza ni
kwamba iwapo hilo ni kweli kwa nini vituo vionekane vitupu kabisa tarehe
20 Machi, 2016?
Lakini kwa upande mwengine, mtu anapokosa hata tahayuri na kudai Dk.
Ali Mohamed Shein amepata kura 299,982 anachotaka kutwambia ni kwamba
ndani ya miezi mitano ya idhilali na mateso aliyowapatisha Wazanzibari
ameweza kuongeza kura 117,971.
Kufedheheka kwa CCM kunakuja zaidi kwamba walisahau kwamba
waliyakubali matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
tarehe 25 Oktoba 2015 kwa upande wa Zanzibar ambapo kama tulivyokwisha
onesha waliopiga kura walikuwa wengi zaidi wakiwa ni 417,882 (na hilo
ungetegemea lingeinufaisha CCM) na bado mgombea wa CCM akapata kura
194,317 sawa na asilimia 46.5.
Kwa kutumia idadi waliyotangaza ya kura
299,982 walizompa Dk. Shein wanataka kutwambia kwamba yeye amepata kura
105,665 zaidi kuliko Dr. Magufuli kwa Zanzibar. Kama takwimu zao zingekuwa sahihi ina maana pia wapiga kura
waliomuunga mkono mgombea wa CUF ambao hawakwenda kupiga kura ni 60,489
tu (sawa na asilimia 15 tu).
Hivi nani utamdanganya kwamba Maalim Seif
Sharif Hamad anaungwa mkono na asilimia 15 tu ya wapiga kura wa
Zanzibar? Nani utamdanganya kwamba ndani ya miezi mitano, CCM imeongeza
kura 105,665 zaidi ya alizopata mgombea wake Dk. Magufuli kwa upande wa
Zanzibar? Kutokana na ubabe na kiburi cha utawala walicho nacho CCM, wameishia
kujifedhehesha kwa takwimu zao za kupika wenyewe. Ndiyo vijana wakasema,
CCM wanapenda namba lakini hawajui hesabu.
NINI MWELEKEO WA CUF NA WAZANZIBARI BAADA YA UBAKAJI HUU WA DEMOKRASIA?
Wazanzibari walio wengi wamekuwa wakituuliza nini mwelekeo wa CUF baada ya ubakaji huu wa demokrasia? Wanatuuliza viongozi wao na hasa mimi tunatokaje katika hali hii ambayo imedumu miaka nenda miaka rudi kila pale Zanzibar inapofanya uchaguzi?
Wazanzibari walio wengi wamekuwa wakituuliza nini mwelekeo wa CUF baada ya ubakaji huu wa demokrasia? Wanatuuliza viongozi wao na hasa mimi tunatokaje katika hali hii ambayo imedumu miaka nenda miaka rudi kila pale Zanzibar inapofanya uchaguzi?
Kabla sijalieleza hilo, nataka niweke wazi leo kwamba tulipofanya
uamuzi wa kuususia uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016
tuliamua kusimama juu ya uamuzi unaoheshimu misingi ya kikatiba ambayo
watu wa Zanzibar tumeamua ndiyo inapaswa iongoze na iendeshe nchi yetu.
Tulijua kwamba uamuzi huo utakuwa na athari kwa CUF na kwa Zanzibar
lakini tulijua na tuliamini pia kwamba athari hiyo haiwezi kuwa kubwa
zaidi kuliko gharama ya kuikanyaga Katiba na Sheria za nchi yetu na
gharama za kupiga teke demokrasia, haki za binadamu na utawala wa
sheria.
Tulipima na tukatafakari kwa kina na kuona ni kheri kumeza machungu
ya athari binafsi kwetu lakini tusimame kidete na kifua mbele katika
kutetea maamuzi ya watu wa Zanzibar waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba,
2015, na pia kulinda misingi ya Katiba na Sheria za nchi yetu na misingi
ya demokrasia na haki za watu. Tuliona hayo ni kheri kwa huko twendako
badala ya kushiriki katika haramu ya ubakaji wa demokrasia na matumizi
ya nguvu za kijeshi kulazimisha watawala wasio na ridhaa ya watu.
Tulifanya maamuzi yale pia kwa lengo la kuepusha shari katika nchi yetu.
Leo Wazanzibari na dunia nzima ni mashahidi kwamba uamuzi ule ulikuwa
sahihi na wa busara. Maana mateso na vitisho walivyokumbana navyo
Wazanzibari wakati tumewaachia uchaguzi ule watawala waovu peke yao
vilikuwa vya kiasi kile kilichoshuhudiwa. Je, tungeliamua kushiriki na
kusimama kulinda na kutetea ushindi wetu hali ingekuwaje? Bila shaka
nchi ingetumbukia katika machafuko ambayo watawala waovu walikuwa tayari
yatokee kuliko kuridhia maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar.
Maamuzi yale yamethibitika pia kwamba ni sahihi kwa jinsi watu wa
Zanzibar walivyoudharau na kuupuuza uchaguzi haramu na batili wa tarehe
20 Machi, 2016. Watawala waovu wa CCM waliwadharau watu wa Zanzibar na
watu wa Zanzibar wakaamua kuwadharau wao tarehe 20 Machi 2016.
Kwa upande mwengine, uamuzi tuliouchukua na kuusimamia pia ni uamuzi
uliosimama juu ya misingi ya heshima na misingi ya utu wa watu, ambayo
yalikuwa ndiyo malengo sahihi ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, malengo sahihi ya Chama cha
Afro Shirazi na malengo sahihi ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Kwa hakika, uamuzi wa kuupuuza na kuudharau uchafuzi wa tarehe 20
Machi, 2016 ni ushindi mwengine wa Zanzibar katika historia yake ya
kisiasa. Nimalizie sasa kwa kujibu hoja ya ni upi mwelekeo wa CUF na wa
Wazanzibari baada ya ubakaji huu wa wazi wa demokrasia na haki za watu
wa Zanzibar?
Kwanza, nirudie na kusisitiza msimamo wetu kwamba hatukubaliani na
ubakaji wa demokrasia na haki za watu wa Zanzibar uliofanywa na watawala
waovu wakisaidiwa na vyombo vya dola. Kwa msingi huo, Wazanzibari
wataendelea kuipinga serikali isiyo na ridhaa ya watu kwa kutumia njia
za amani, za kidemokrsia na zinazoendana na misingi ya Katiba na Sheria
za nchi yetu.
Jana kumetangazwa kile kilichoitwa ni Baraza la Mawaziri. Msimamo
wetu uko pale pale. Kama tusivyomtambua aliyelitangaza Baraza hilo,
vivyo hivyo hatulitambui Baraza lake la Mawaziri. Kwa hakika, kwa sababu msingi wa watawala waliojinyakulia madaraka ni
kupitia uvunjwaji wa Katiba, kila kinachofuata kimekuwa kikiendeleza
uvunjwaji wa Katiba.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia
Marekebisho ya 10 ya mwaka 2010, Ibara ya 9 (1) inalazimisha Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Ibara za 39, 39A na 42 za Katiba zimeeleza namna Serikali hiyo ya Umoja
wa Kitaifa itakavyoundwa. Masharti yote hayo yanaendelea kuvunjwa na
mtawala aliyeamua kuyapiga teke maamuzi ya Wazanzibari na kujiweka
madarakani kwa nguvu. Kwa hivyo, Serikali yake haiwezi kuwa Serikali
inayokwenda na Katiba. Kwa ufupi, si Serikali halali kwa mujibu wa
Katiba.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF katika kikao chake cha tarehe 2
– 3 Aprili, 2016 lilipitisha maazimio yafuatayo miongoni mwa maazimio
yake:
“Azimio Nam. 9:
Haliyatambui matokeo ya uchaguzi huo haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa Wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani. Baraza Kuu linaungana na wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali watu hao na kwa hivyo halitoitambua Serikali, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa na watu hao. CUF haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu.
Haliyatambui matokeo ya uchaguzi huo haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa Wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani. Baraza Kuu linaungana na wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali watu hao na kwa hivyo halitoitambua Serikali, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa na watu hao. CUF haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu.
Kwa
vyovyote vile, Serikali itakayoundwa haitakidhi matakwa ya Katiba ya
Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa Katiba ambayo
inaeleza kwa uwazi kabisa namna ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa Zanzibar.
“Azimio Nam. 10:
Linawataka wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba na kisheria ambazo zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa watawala waovu na wasio na ridhaa ya watu waliojiweka madarakani kwa kutumia nguvu na ubakaji wa demokrasia kwa kutoipa ushirikiano Serikali itakayoundwa na watawala hao.”
Linawataka wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba na kisheria ambazo zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa watawala waovu na wasio na ridhaa ya watu waliojiweka madarakani kwa kutumia nguvu na ubakaji wa demokrasia kwa kutoipa ushirikiano Serikali itakayoundwa na watawala hao.”
Baada ya maazimio hayo ya Baraza Kuu, kinachofuata sasa ni
utekelezaji wake. Hivi sasa tunapanga mikakati madhubuti ya utekelezaji
wa maazimio hayo kwa kutumia njia za amani, za kidemokrasia na za
kikatiba ili kutufikisha kwenye malengo yetu ya kuona maamuzi ya watu wa
Zanzibar yanaheshimiwa.
Nina hakika kabisa kuwa mikakati tunayoipanga itazaa hatua ambazo zitaibana Serikali haramu na hatimaye itasalimu amri kwa wananchi wa Zanzibar ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ndiyo wenye mamlaka ya kuiweka madarakani Serikali wanayoitaka. Katika dunia ya leo, hatuwezi kuongozwa na watawala ambao hawakupewa mamlaka na watu wenyewe.
Nina hakika kabisa kuwa mikakati tunayoipanga itazaa hatua ambazo zitaibana Serikali haramu na hatimaye itasalimu amri kwa wananchi wa Zanzibar ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ndiyo wenye mamlaka ya kuiweka madarakani Serikali wanayoitaka. Katika dunia ya leo, hatuwezi kuongozwa na watawala ambao hawakupewa mamlaka na watu wenyewe.
Pili, naipongeza na kuishukuru jumuiya ya kimataifa na washirika wa
maendeleo kwa msimamo waliochukua wa kukataa kubariki ubakaji huo wa
demokrasia na haki za watu wa Zanzibar na kukataa kushiriki katika
uapishwaji wa mtu asiye na ridhaa ya wapiga kura wa Zanzibar.
Napongeza
hatua ambazo wameanza kuzichukua dhidi ya Serikali za CCM ambazo ndizo
zilizosimamia ubakaji huo wa demokrasia na haki za watu. Natoa wito kwao
kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya watawala hawa waovu zikiwemo
kuwawekea vikwazo vya kusafiri, kufuatilia akaunti zao za fedha nje ya
nchi na hatua za kuchunguza matendo yao ya uhalifu dhidi ya binadamu.
Wananchi waliodhulumiwa haki zao wanaziunga mkono hatua hizo wakiamini
kwamba CCM ni lazima iwajibishwe kwa matendo yake maovu dhidi yao.
Nitumie fursa hii kwa mara nyengine tena kuwataka wananchi wa
Zanzibar kudumisha amani ya nchi yetu na umoja wa watu wetu. Nikiwa
kiongozi wao ninayewapenda na ambaye nimejitolea kuwatumikia katika umri
wangu wote siwezi kuwaongoza kuelekea kwenye fujo na ghasia au vitendo
vitakavyopelekea kuiharibu nchi yetu na kuathiri watu wetu. Nina imani
kabisa kwamba njia tunayoifuata ni njia ya haki; na haki siku zote
itashinda.
Mwaka 2009, mimi na mwenzangu, Dk. Amani Abeid Karume, tuliwaongoza
Wazanzibari katika Maridhiano yaliyoashiria mwanzo wa ujenzi wa
mahusiano mapya baina ya watu wema wa Zanzibar kwa kuzika siasa za
ubaguzi, utengano, chuki, hasama na fujo na badala yake kusimamisha
siasa za maelewano, umoja, upendo, mshikamano na udugu katika jamii
yetu.
Tulitegemea kuanzia pale tungeendelea mbele kwa kuchukua hatua za
kuyaimarisha maridhiano yetu na kuyazamisha zaidi kwenye nyoyo za
Wazanzibari. Binafsi nasikitishwa na kuhuzunishwa sana kuona watawala
waovu wasiowatakia mema watu wa nchi hii wameturudisha tulikotoka kwa
maslahi yao binafsi.
Natoa wito kwa Wazanzibari wenzangu kuwa tukatae
kurudishwa kwenye siasa zile za ubaguzi, utengano, chuki, hasama na fujo
na kila mmoja afanye lile liliomo katika uwezo wake kuendeleza
maelewano, umoja, upendo, mshikamano na udugu katika jamii yetu.
Wazanzibari tumeamua kuisimamisha tena Zanzibar yetu na Zanzibar
itasimama tena Inshallah. Hilo sina wasiwasi nalo kama kiongozi wa
Wazanzibari waliyenipa ridhaa yao.
HATIMAYE TUTASHINDA.
WANANCHI JASIRI NA SHUPAVU WA ZANZIBAR WATASHINDA.
WANANCHI JASIRI NA SHUPAVU WA ZANZIBAR WATASHINDA.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :