CHADEMA yapanga mikakati ya urais 2015
Posted in
No comments
Monday, January 28, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
KAMATI Kuu
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imekutana katika kikao
maalumu kutafakari na kupanga mikakati katika mambo makuu manne,
likiwamo la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2014/2015.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Blue
Pearl, ambako kikao hicho kinaendelea leo, Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema wameamua kujifungia na kupanga
mikakati ya Uchaguzi wa Serikali na Mitaa mwaka 2014 na ule Mkuu wa
mwaka 2015 ili kujiweka sawa.
Hatua hiyo
ya CHADEMA imekuja wakati ambapo vita ya urais imeendelea kushamiri
ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku vigogo wanaotajwa kuwania
nafasi hiyo nao wakionekana kujipanga na kuandaa mikakati kuelekea mwaka
2015.
CHADEMA
kinaonekana kuwa ndicho chama pekee cha upinzani ambacho kimejizolea
umaarufu mkubwa kwenye medani ya siasa katika miaka ya hivi karibuni,
kikichukua nafasi iliyokuwa imekaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), hivyo
kuonekana kuwa tishio dhidi ya chama tawala.
Upepo wa
CHADEMA ulionekana kuvuma vema wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010
ambapo kilishika nafasi ya pili nyuma ya CCM, hali ambayo imesababisha
macho na masikio mara zote kuelekezwa kwenye chama hicho kikuu cha
upinzani, hasa linapokuja suala zima la kuangalia jinsi kilivyojipanga
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika
mkutano huo wa jana na wanahabari, Mnyika alisema kikao hicho cha siku
mbili ambacho kinamalizika leo kimekuwa maalumu kwa sababu ya unyeti
wake, lakini pia kimeshirikisha wabunge wa chama hicho na kuahidi
kueleza namna uamuzi utakavyofikiwa mara baada ya kikao hicho.
Wakati
wakipanga mikakati ya 2014/2015, pia vigogo hao wa CHADEMA wanaangalia
namna ya ujenzi wa oganaizesheni ya chama nchi nzima wakati ambapo mwaka
huu watakuwa na uchaguzi mkuu wa ndani.
Katika
kujipanga huko, CHADEMA pia imesema kuwa imejiweka sawa kuangalia namna
ya utekelezaji wa kile ambacho chama kiliahidi kukifanyia kazi kutoka
katika maeneo ambayo ina wabunge sambamba na kutafakari namna ambavyo
kambi rasmi ya upinzani bungeni inatekeleza majukumu yake.
Baada ya
kikao hicho cha Kamati Kuu, Mnyika pia alisema CHADEMA inajiandaa kutoa
kauli nzito kuhusiana na migogoro inayoendelea nchini, ikiwamo ya
wafugaji na wakulima mkoani Morogoro, wanafunzi wa vyuo vya St. John,
IFM pamoja na suala zima la gesi ya Mtwara mara baada ya kukutana na
Baraza Kuu kesho, ambapo pamoja na mambo mengine watapatiwa taarifa
rasmi kutoka kwa viongozi wao Mtwara, ikiwa ni pamoja na mapendekezo
yao.
Akisisitiza
kuhusu suala hilo la gesi, Mnyika alisema kuwa mgogoro unaoshamiri wa
gesi mkoani Mtwara ni matokeo ya sera mbovu ya usimamizi wa rasilimali
za umma, na udhaifu wa kiongozi kushughulikia migogoro.
Katika hilo,
Mnyika alisema wao kama CHADEMA wanatoa wito kwa rais pamoja na
serikali yake kurekebisha kauli za vitisho zilizotolewa dhidi ya
wananchi wa Mtwara, kwani ndiyo sababu ya kuendelea kuchochea mgogoro
huo.
CHADEMA
mbali na kumtaka rais kutoa kauli zinazojenga muafaka, pia wamewataka
wananchi wa Mtwara wawe watulivu wakati kiongozi huyo wa nchi pamoja na
serikali watakapokwenda kurekebisha kauli.
“Baraza kuu
la chama litakutana na wilaya zote Tanzania na tunahitaji taarifa kutoka
Mtwara na hatua wanazozipendekeza tuchukue, hii ni pamoja na migogoro
mingine…hatua ambazo CHADEMA itachukua itatolewa baada ya mkutano wa
Baraza Kuu la chama,” alisema.
Kuhusu suala
la baadhi ya wabunge kuhongwa na kwamba wao ndio wamewachochea wananchi
kufanya vurugu, Mnyika alisema jambo hilo kamwe lisipotoshwe na kuitaka
serikali ijibu hoja za wananchi.
Aidha,
akifafanua kuhusu hilo Mnyika alikwenda mbali zaidi akisisitiza kuwa
wabunge pia wametofautia mitizamo, lakini akasisitiza kuwa wananchi
wamesukumwa kudai masilahi yao.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :