ECOWAS kuongeza vikosi vyake Mali
Posted in
No comments
Sunday, January 27, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
Mataifa ya Afrika Magharibi yamekubali kuongeza idadi ya wanajeshi wake
watakaopelekwa Mali kuwaunga mkono wanajeshi wa nchi hiyo kupambana na
waasi wenye itikadi kali za Kiislamu
Uamuzi huo umefikiwa wakati ambapo vikosi vya Mali na Ufaransa
vikidhibiti maeneo muhimu ya Gao. Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya
Afrika Magharibi-ECOWAS waliokutana mjini Abidjan, Cote d'Ivoire
wamefikia uamuzi huo ambapo sasa wanajeshi watakaopelekwa Mali watakuwa
7,700 badala ya 3,300 waliokubaliana awali. Mkuu wa Majeshi wa Cote
d'Ivoire, Jenerali Soumaila Bakayoko amesema kuwa hadi sasa wanajeshi
1,750 kutoka nchi jirani za Afrika Magharibi wako Mali, huku Chad na
Niger zikitoa wanajeshi 550 kila mmoja.Hali ilivyo ndani ya Mali
Nchini Mali kwenyewe, vikosi vya Mali na Ufaransa vimefanikiwa kuudhibiti uwanja wa ndege na daraja muhimu katika mji wa Gao. Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian amesema kuwa wanajeshi hao wameudhibiti mji huo uliokuwa ukidhibitiwa na waasi tangu mwezi Juni mwaka uliopita na kwamba ngome kuu na magari ya waasi yameharibiwa.
Wanajeshi wa Ufaransa walioko Mali
Uungaji mkono wa kimataifa
Wakati huo huo, Rais Barack Obama wa Marekani amekubali ombi la Rais Francois Hollande wa Ufaransa la kujaza mafuta ndege za kivita za Ufaransa ambazo zinaendesha operesheni dhidi ya waasi wa Mali.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, George Little amesema viongozi hao pia wamejadiliana kuhusu mipango ya Marekani kusafirisha wanajeshi kutoka mataifa ya Afrika katika jitihada za kuunga mkono juhudi za kimataifa katika suala la Mali.
Aidha, Umoja wa Ulaya umesema jana kuwa utaanza kupeleka wakufunzi wa kijeshi ili kuwapatia mafunzo wanajeshi wa Mali katikati ya mwezi Februari huku wakufunzi wote 200 hadi 250 wakiwa Mali ifikapo katikati ya mwezi Machi. Ujerumani imegusia uwezekano wa kuiunga mkono Mali katika mkutano ujao wa wafadhili.
Mzozo wa Mali kutawala mkutano wa Umoja wa Afrika
Viongozi wa Umoja wa Afrika wanakutana leo mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambapo pamoja na mambo mengine wataujadili mzozo wa Mali, likiwemo suala la kupelekwa haraka kwa kikosi cha Afrika nchini humo.
Viongozi wa Umoja wa Afrika
Umoja huo pia utaomba msaada wa muda wa kimkakati kutoka kwenye Umoja wa Mataifa kwa ajili ya AFISMA na kuuomba umoja huo kuidhinisha kuanzishwa haraka mipango ambayo itaiwezesha AFISMA kupeleka haraka wanajeshi wake na kupewa mamlaka ya kuendesha operesheni. Msaada wa kimkakati utajumuisha usafiri, madawa na hospitali katika maeneo ya mapambano.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :