TATIZO LA DOMAYO NI HILI...............
Posted in
No comments
Monday, January 28, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
Frank Domayo jana Uwanja wa Taifa |
KIUNGO tegemeo wa Yanga SC ya Dar es Salaam, Frank Domayo ana
tatizo a kupatwa na kizunguungu ambalo humtokea mara kwa mara na sasa klabu
yake hiyo imeamua kulifanyia uchunguzi wa kina ili kulipatia ufumbuzi,
imeelezwa.
Msemaji wa klabu hiyo bingwa Afrika Mashariki na Kati, Baraka
Kizuguto ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Domayo aliyepatwa na hali hiyo
ghafla jana muda mfupi kabla ya timu hiyo kuingia uwanjani kumenyana na Prisons
katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa sasa yupo chini ya
uangalizi wa Daktari wa timu, Nassor Matuzya.
“Leo tulikuwa na mazoezi kidogo asubuhi, Domayo naye alifanya
kidogo mazoezi, ila Daktari akamuambia apumzike, na baada ya mazoezi akaondoka
naye kwenda kumfanyia uchunguzi zaidi, taarifa zaidi zitatolewa baadaye,”alisema
Kizuguto.
Domayo jana alizidiwa ghafla Uwanja wa Taifa, akiwa tayari
amefika kwenye chumba cha kubadilishia nguo na amevaa jezi akiwa miongoni mwa
wachezaji 11 waliopangwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts kuanza mechi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, benchi la ufundi la Yanga lilidhani ni
Malaria na kumkimbiza katika Zahanati ya Uwanja wa Taifa, ambako alipatiwa
huduma ya kwanza na kupata nafuu.
Kwa sababu hiyo, ilibidi nafasi yake aanze kiungo mwingine,
Nurdin Bakari na timu ikafainiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, hivyo kuzidi
kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu, ikifikisha pointi 32, baada ya kucheza
mechi 14, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27 na Simba 26.
Hadi mapumziko jana, timu hizo zilikuwa tayari zimefungana
bao 1-1, Yanga wakitangulia kupata bao lao dakika ya 10 kabla ya Prisons
kusawazisha dakika ya 17.
Bao la Yanga lilifungwa na Jerry Tegete aliyeunganisha krosi
nzuri ya Simon Msuva kutoka wingi ya kulia, wakati la Prisons lilifungwa na Elias
Maguri, aliyeunganisha krosi nzuri ya Misango Magai kutoka wingi ya kushoto.
Yanga walicheza vizuri dakika 15 za mwanzo na baada ya hapo,
timu hizo zilianza kushambuliana kwa zamu, ingawa Watoto wa Jangwani ndio
waliopoteza nafasi nzuri zaidi za kufunga.
Kipindi cha pili, Yanga walirudi na kasi nzuri kusaka ushindi
na iliwachukua dakika 11 tu kupata bao la pili, lililofungwa na Mbutu Twite
baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Prisons.
Wakati Prisons wakiwa kwenye jithada za kusaka bao la
kusawazisha, walijikuta wakitandikwa bao la tatu, Tegete tena akiwainua vitini
mashabiki wa Yanga, baada ya kupokea pasi nzuri ya Nurdin Bakari dakika ya 65.
Baada ya bao hilo, Yanga walianza kuonyesha vitu vya Uturuki
walipoweka kambi ya wiki mbili kabla ya kuanza kwa mzunguko huu wa pili wa Ligi
Kuu, wakicheza soka ya madoido pasi nyingi, uzungu na kila aina ya mbwembwe,
ili mradi tu kuwaburudisha mashabiki wake.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :