Moses Sithole: Handsome aliyetikisa kwa mauaji ya kutisha ya wanawake 38….!

Posted in
No comments
Monday, June 17, 2013 By danielmjema.blogspot.com




  1. Dk. Mervyn Mansell
    Mmoja wa wahanga wake


    Moses Sithole
 Mnamo Septemba 17, 1995, Dk. Mervyn Mansell aliombwa na Polisi ili kusaidia kujua tarehe ya kifo cha mwili wa mtu uliyookotwa katika pori lililoko katika eneo la machimbo ya madini la Van Dyke eneo ambalo lipo jirani na mji wa Boksburg nchini Afrika ya kusini. Dk. Mansell mtaalamu wa elimu ya wadudu akifanya kazi katika kitengo cha utafiti wa kilimo katika halimashauri ya jiji la Pretoria alikuwa amepata taarifa hizo wiki mbili mapema kutoka kwa askari wa upelelezi aitwae Vivian Bieldt.

Askari huyo alikuwa amesoma utafiti fulani kuhusiana na funza kutumika kukadiria siku kifo kilipotokea kwa usahihi kabisa pale inapotokea mwili wa mtu aliyeuawa na kutekelezwa mahali na kuonekana baada ya siku kadhaa ukiwa umeshaanza kuharibika kwa kushambuliwa na funza.

Siku hiyo hiyo baadae Inspekta Bieldt alimpigia tena simu Dk. Mansell na kumjulisha kwamba, sio mwili wa mtu mmoja tena bali wamegundua miili ya watu watano. Kwa upande wa Dk. Mansell hii ilikuwa ni kesi ya kwanza nchini humo kuwahusisha wataalamu wa elimu ya wadudu katika upelelezi. Hata hivyo jambo la kushangaza ni kwamba mpaka siku ya pili wakiendelea kufanya upelelezi katika eneo hilo, walipata jumla ya miili watu kumi wote wakiwa ni wanawake. Hiyo ilionyesha kwamba muuaji alikuwa akiuwa na kufika pale kuitelekza miili ya watu aliowauwa katika eneo hilo.

Mwili wa kwanza uligunduliwa siku ya Jumamosi jioni ya Septemba 16 1995, wakati Polisi mmoja alipotoka na mbwa wake kwenda kuwinda sungura katika pori hilo. Zaidi ya Polisi 30 wakiwemo askari wa upelelezi kutoka katika kitengo cha upelelezi wa kesi za mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha cha East Rand waliwasili katika eneo hilo, pia walikuwepo wataalamu wa kukusanya ushahidi kitaalamu ambao walikuwa na jukumu kubwa la kuchunguza eneo la tukio ili kukusanya ushahidi kwa siku kadhaa.

 Si hivyo tu, bali pia Helikopta na mbwa wa Polisi vilihusishwa ili kuchunguza iwapo kulikuwa na miili mingine iliyotelekezwa katika eneo hilo.Micki Pistorius Polisi na mwanasaikolojia alikuwepo pia katika eneo hilo. Akizungumzia hali aliyokutana nayo katika eneo hilo, alisema kwamba hali ilikuwa ni ya kutisha sana na hajawahi kukutana na hali hiyo tangu kuzaliwa kwake.

 “Haya ni moja ya mauaji ya kutisha ambayo sijapata kuyashuhudia katika maisha yangu, miili ya watu waliouawa ilikuwa imetapakaa kila mahali huku mingine ikiwa imekaribiana kwa umbali wa mita kadhaa kutoka ulipo mwili mwingine. Funza walikuwa ni wengi katika eneo hilo kiasi cha kutupanda katika nguo zetu.” Alisema mama huyo, Polisi na mwanasaikolojia.

Kuna uwezekano kwamba baadhi ya wanawake wale waliouawa katika eneo hilo na kutelekezwa mahali hapo. Ilikuwa ni vigumu kuamini kwamba muuaji alikuwa akiwachukua wahanga wake na kuwapeleka katika eneo hilo ambapo kulikuwa na miili ya watu waliuawa na muuaji huyo tena ikiwa tayari imeshaanza kuharibika ili kuwatisha na kuwajengea hofu kabla ya kuwabaka kuwauwa na kutelekeza miili yao mahali hapo. 

Ili kuthibitisha kuwa lengo la muuaji kuwapeleka wahanga wake katika eneo hilo ni ili kuwatisha na kuwajengea hofu, mmoja wa wanawake waliouawa alikuwa amejikojolea kwenye suruali yake ya jinzi kwa hofu kabla ya kuuawa.Wakati Polisi wakiendelea kujitetea kutokana na mauaji ya Mtuhumiwa wa mauaji ya kutisha David Selepe aliyeuawa Desemba 17, 1994 akiwa mikononi mwa Polisi, walidai kwamba wana ushahidi ambao unamuhusisha David Selepe na vifo vya wanawake sita ambao miili yao ilipatikana katika eneo la Cleveland.

David Selepea alikuwa akituhumiwa kwa vifo vya wanawake 4, lakini alipokamatwa alikiri kuuwa wanawake 15. Ni wakati alipokuwa akiwapeleka askari wa upelelezi katika eneo alipotekeleza miili ya wanawake wengine ndipo alipouawa kwa kupigwa risasi ya kichwa wakati alipojaribu kutoroka. Polisi waliamini kwamba yeye ndiye aliyehusika na mauaji ya vifo vya wanawake hao sita.

Mwili wa kwanza ulipatikana hapo mnamo Januari 4, 1995, ukiwa umetelekezwa porini nusu uchi. Mwili wa mwanamke huyo haukupata kutambuliwa. Mwili wa pili ulipatikana hapo mnamo Februari 9. Alikuwa ni mwanamke na alikuwa uchi wa mnyama na nguo zake ziliwekwa kifuani mwake zikiwa zimewekewa jiwe juu yake.

 Alama zake za vidole ndizo zilizoharakisha kutambuliwa kwake. Alikuwa ni binti mrembo aliyejulikana kwa jina la Nuku Soko aliyekuwa na umri wa miaka 27. Alipotea tangu Januari pale alipoaga kwamba anakwenda kwa dada yake aishie katika eneo la Klipgat, na hakuonekana tangu siku hiyo.

Asubuhi ya Machi 6, wafanyakazi wa ujenzi walikuwa wanachimba shimo katika eneo la Atteridgevile, na walipatwa na mshtuko walipoona matiti ya mwanamke kuashiria kwamba kulikuwa na mwili wa mwanamke uliozikwa katika eneo hilo. Waliufukua mwili huo na baadae ulitambuliwa kwamba ni wa mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Sara Matlakala Mokono.

 Alikuwa na umri wa miaka 25, na lipotea siku tatu zilizopita wakati akiwa njiani kwenda kuonana na mtu aliyemuahidi kumpatia kazi.Mnamo April 12 mwili mwingine uligunduliwa katika eneo la Atteridgeville. Mwanamke huyo mikono yake imefungwa kwa nyuma kwa kutumia sidilia yake. Alikuwa amenyongwa. Ingawa nguo zake zilikuja kuonekana katika eneo hilo lakini chupi yake haikupata kuonekana.

Alikuja kutambuliwa baadae kama Letta Nomthandazo Ndlangamandia aliyekuwa na umri wa miaka 25. 

Mnamo April 17, gazeti maarufu nchini humo linaloandikwa kwa lugha ya Afikaans liliibuka na habari kwamba kuna miili ya wanawake wanne imegunduliwa na likahitimisha kwa kusema kwamba mtindo uliotumika katika kutekeleza mauaji hayo (modus operandi) unafanana kabisa na namna muuaji maarufu wa Cleveland alivyokuwa akiuwa ambaye anaaminika kuwa ni Davidi Selepe. 

Mnamo April 19, Polisi walitangaza rasmi kwamba kuna uwezekano kuna muuaji mwingine anayeendesha mauaji kaika eneo hilo la Atteridgeville. Walituhumu kwamba huenda kuna mtu anaiga mtindo wa muuaji wa Cleveland ili kuwachanganya askari wa upelelezi.

Siku iliyofuata mwili wa mtoto wa kiume uligunduliwa jirani kabisa na ulipokutwa mwili wa Letta Ndlangamandla. Ilibainika kwamba mwili huo ni wa mtoto aitwae Sibusiso aliyekuwa na umri wa miaka 2. 

Mwili huo ulikutwa umbali wa futi 65 kutoka ulipokuwa mwili wa mama yake. Letta aliondoka mapema Mwezi April kwenda Mashariki mwa jiji la Pretoria kukutana na mtu ambaye alimuahidi kumpatia kazi.

 Kwa kuwa hakuwa na mtu wa kumuachia mwanaye Letta aliamua kuondoka naye. Wataalamu wa uchunguzi wa maiti walishindwa kubaini sababu ya kifo cha mtoto huyo ingawa alikuwa na jeraha kichwani na haikujulikana ni yupi alitangulia kufa kati ya mama au mtoto. 

Kulikuwa na uwezekano kuwa mtoto Sibusiso alikufa kutokana na kupigwa na baridi kali porini baada ya mama yake kuuawa. 

Hebu fikiria mtoto mdogo wa miaka miwili alikuwa akirandaranda porini peke yake karibu na ulipolala mwili wa mama yake kwa sababu hakujua mahali pa kwenda kutokana na kuwa na umri mdogo hadi alipokufa.

Mnamo may 13, mwili wa Esther Moshibudi Mainetjas uligunduliwa katika msituni jirani na eneo la Hercules magharibi mwa jiji la Pretoria. 

Alikuwa nusu uchi na alikuwa amenyongwa kwa kutumia nguo. Kwa mara ya mwisho alionekana jioni ya siku iliyopita.

Mwili wa mwanamke mwingine uligunduliwa mwezi mmoja baadae, ingawa kulikuwa na wanawake wengine watano waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa nyakati tofauti. 

Francina Nomsa Sithebe aliyekuwa na miaka 25, mwili wake ulikutwa ukiwa umekalishwa ukiwa umeegemea mti hapo mnamo Juni 13. Ingawa alikuwa amevaa gauni.

wachunguzi wa maiti walibaini kwamba chupi yake na mkanda wa mkoba wake ulikuwa umefungwa shingoni mwake na kisha ukafungwa kwenye mti.Siku tatu baadae, mnamo Juni 16, Elizabeth Granny Mathetsas mwili wake uligunduliwa ukiwa uchi katika eneo la viwanda la Rosslyn kama maili 9 kaskazini magharibi mwa jiji la Pretoria. Alikuwa na umri wa miaka 19 na mara ya mwisho alionekana akiwa hai hapo mnamo Mei 25.

Mnamo Juni 22 mwili wa mwanamke mwingine uligunduliwa katika eneo la Rosherville. Alikuwa amebakwa na kisha kunyongwa. Nyaraka za utambulisho wake zilikutwa katika eneo hilo na kurahisisha kutambuliwa kwake.

alikuwa anaitwa Ernestina Mohadi Mosebo. Alikuwa na umri wa miaka 30.Siku mbili baadae mnamo Juni 24, mwili wa Nikiwe Dikos uligunduliwa katika eneo la Atteridgeville. 

Alikuwa ametoweka tangu April 7, wakati alipoaga kuwa anakwenda kuonana na mtu aliyemuahidi kumpatia kazi. Mwili wake ulikuwa umeshambuliwa na mbwa mwitu kiasi cha kutawanywa vipande vpande kila mahali. Mikono yake ilikuwa imefungwa na chupi yake.

Kutokana na mwili wake kutawanywa na Mbwa Mwitu, Polisi walifanikiwa kupata fuvu la kichwa chake siku iliyofuata, futi 130 kutoka yalipolala mabaki ya mwili wake. 

Alkuwa amenyongwa kwa kutumia chupi yake ikiwa imekazwa kwa kutumia kipande cha mti, pia kulikuwa ana kipande cha mti kilichosokomezwa kwenye uke wake. Alikuwa amevaa pete yake ya ndoa na mabaki ya mwili huyo yalitambuliwa na mumewe.

Absolom Sangweni alikuwa akiishi kwenye nyumba yake ya turubai katika eneo la Beyers Park katika mji wa Boksburg. Mnamo July 17, 1995, aliwaona mwanaume na mwanamke wakitmbea kuelekea kwenye kijipori kilichokuwa jirani na hapo nyumbani kwake. Kwa kuwa alikuwa anajua kwamba kuna uzio uliozungushwa katika kijipori hicho alijua watu wale wasingeweza kuendelea na safari yao. 

Aliwaita, lakini yule mwanaume alimjibu kwamba analifahamu vizuri eneo hilo. baadae kidogo walipotea machoni mwake. Hata hivyo Absolom aliendelea kuchunguza walipopotelea watu wale. 

Baadae kidogo alimuona yule mwanaume akitokea lakini akiwa peke yake. Absolom alidai kuona kitu kinachong’aa mkononi mwa mwanaume yule na alikuwa akiangalia huku na huko kama vile alikuwa na wasiwasi kwamba kuna mtu amemuona akifanya jambo na hivyo alikuwa anataka kuondoka katika eneo hilo haraka iwezekanavyo. Hata hivyo alitoweka. 

Absolom alikwenda katika kijipori hicho na kumkuta yule mwanamke akiwa amenyanyaswa kijinsia na alikuwa amepoteza fahamu. Absolom alikwenda katika supermarket moja iliyokuwa jirani na kuwajulisha Polisi waliokuwa katika eneo hilo. Sajenti Gideon ONeal alifika katika eneo la tukio na kumkuta mwanamke huyo akiwa amepoteza fahamu. Hakukuta mkoba wa mwanamke huyo na hivyo kupata ugumu wa kumtambua. 

Askari mwenzake aliwasili katika eneo hilo akiwa na mkoba wa huduma ya kwanza lakini walishindwa kuokoa maisha yake. Alifariki dunia. Alikuwa amenyongwa na mkanda wa gauni lake. Absolom alidai kwamba alikuwa mbali na hakuweza kumtambua mwanaume huyo.Mwanamke huyo altambuliwa kwa jina la Josephine Mantsali Mlangeni. Alikuwa na mri wa miaka 25 na mama wa watoto wanne. 

Alikuwa ameaga nyumbani kwamba anakwenda kukutana na mtu ambaye alimwahidi kumapatia kazi nzuri.Miili mingine ya wanawake waliouawa iliogunduliwa ni hii ifuaayo:

Granny Dimakatso Ramela. Mwili wake uligunduliwa Magharibi mwa jiji la Pretoria. Alikuwa akiwa amelala kifudifudina kamba iliyotumika kumnyongea ilikuwa bado iko shingoni mwake. Alikuwa na umri wa miaka 21 na alikuwa ametoweka kusikojulikana tangu Mei 23. 

Mildred Ntiya Leple aliyekuwa na umri wa miaka 28 alipelekwa Pretoria na mumewe baada ya Granny Ramela kutoweka, ili kuonana na mtu ambaye alimwahidi kumpatia kazi. 

Hakupata kumuona mke wake tena hadi pale mwili wake ulipopatikana hapo mnamo Julai 26 jirani na bwawa la Bon Accord karibu na mji wa Onderstepoort, takriban maili 9 kaskazini mwa jiji la Pritoria. Alikuwa amenyongwa kwa kutumia chupi yake.

Polisi ilibidi waandae chumba maalum cha kufanyia uchunguzi wa miili ya wanawake iliyokuwa ikiokotwa kila uchao baada ya kuuawa kwa mtindo unaofanana.Mnamo August 8, mwili mwingine wa mwanamke uligunduliwa katika mji wa Onderstepoort. 

Alitambuliwa kutokana na nyaraka zilizokutwa ndani ya mkoba wake. Alijulikana kwa jina la Elsie Khoti Masango aliyekuwa na umri wa miaka 25. Alikuwa ametoweka tangu Julai 14.

Mwili wa mwanamke mwingine uligunduliwa katika eneo hilo hilo, lakini ulikuwa umechomwa moto kiasi cha kutotambuliwa. Haikujulikana kwamba mwili ule ulikuwa umetelekezwa katika eneo hilo kwa muda gani.

Wiki mbili baadae mnamo Agost 23, mwili wa mwanamke mwingine aliyejulikana kwa jina la Oscarina Vuyokazi Jakalases aliyekuwa na umri wa miaka 30 uligunduliwa jirani na eneo la Boksburg. Alikuwa ametoweka siku ulipopatikana mwili wa Elsie Masangos. Ilikuwa ni Agosti 8.

Mnamo Agosti 28 na 30, miili mingine ya wanawake wawili iligunduliwa katika bwawa la Bon Accord karibu na mji wa Onderstepoort. 

Mwili wa mwanamke wa pili ulionyesha kwamba ulitelekezwa kwa miezi kadhaa katika eneo hilo, na haukuweza kutambuliwa.Kwa kifupi ni kwamba kwa nyakati tofauti miili zaidi ya wanawake 38 ilipatikana katika maeneo tofauti tofauti wote wakiwa wameuawa kwa mtindo unaofanana huku wengine wakiwa wamebakwa. 

 Kutokana na mauaji hayo ya kutisha na ya mfuatano, yaliwapa askari wa upelelezi nchini humo wakati mgumu, hivyo waliamua kuwatafuta wataalamu waliobobea kwa kazi ya upelelezi nje a nchi hiyo hususan Ulaya au Marekani.

Mmoja wa wapelelezi wa kesi hiyo mwanamama Micki Pistorius alikwenda kuhudhuria kongamano moja nchini Skotland mnamo Juni, ambapo alikutana na Robert Ressler na Roy Hazelwood wote waliwahi kufanya kazi katika shirika la upelelezi la Marekani FBI, lakini walikuwa wamestaafu wakati huo. 

baada ya kuzungumza nao walikubali kwenda nchini humo kusaidia katika upelelezi wa kesi hiyo.Micki Pistorius akishirikiana na Robert Rissler walitengeneza taarifa fupi kuhusiana na mauaji huyo ili kurahisisha upelelezi wa kesi hiyo.

Taarifa hiyo ilionyesha kwamba kulikuwa na maeneo maalum ambapo miili ya wanawake hao iliteekezwa. Wanawake nane waliouawa walitupwa jirani na mji wa Atteridgeville akiwepo mtoto wa kiume wa miaka miwili. 

Miili ya wanawake sita iligunduliwa katika eneo la Onderstepoort, miili ya wanawake wengine 12 ilikutwa imetupwa katika eneo la Boksburg, pia kulikuwa na mwanamke aliyeokotwa jirani na mji wa Cleveland. Wataalamu hao walibaini kwamba mauaji ya wanawake 27 yalikuwa yanafanana. 

Lakini pia waliamini kwamba huenda mauaji hayo yalitekelezwa na muuaji zaidi ya mmoja. Ilionyesha kwamba maeneo ilipotelekezwa miili hiyo ilikuwa imechaguliwa kwa umakini wa hali ya juu mno, na muuaji (wauaji) alikuwa anawafahamu wahanga hao.

 Maeneo ilipotupwa miili hiyo ilikuwa inafikika kiurahisi na hata namna miili hiyo ilivyokuwa ikitelekezwa muuaji hakuonekana kama alikuwaana dhamira ya kuificha ili isipatikane.

 Miili mingine ilikuwa imelaliana.Katika taarifa yao wataalamu hao pia walibainisha kwamba, wanawake wote waliouawa kwa mujibu wa ndugu zao walikuwa wanaaga kwamba wanakwenda kuonana na mtu aliyewaahidi kuwapatia kazi. Alikuwa anawabaka na kuwauwa na kisha kutelekeza miili hiyo. 

Walimuelezea muuaji huyo kama ni (1)mwanaume mweusi mwenye umri kati ya mika 20 au alikuwa anakaribia miaka 30 (2)Alikuwa amejiajiri ambapo likuwa ana uwezo wa kuwa na fedha za kutosha. (3) huenda alikuwa anaendesha gari la kifahari. (4)anavaa mavazi ya gharama na vito vya thamani. (5) ni mtu anayejichanganya na watu, mcheshi na ni mtu wa wanawake. (6) kuna uwezekani ameoa, au ametengana na mke wake au ameachana na mke wake. 

(7) ni mtu wa kujirusha kwenye vilabu na kujichanganya na watu. (8) anaweza kuwa anajihusisha na utapeli au wizi (9) atakuwa anawafuatilia ripoti za Polisi jinsi wanavyofanya pelelezi wao kupitia vyombo vya habari.

 (10) anaonekana kuwa na chuki na wanawake ingawa anaonekana kuwachangamkia.

 (11) huwa anapiga punyeto baada ya kufanya mauaji juu ya miili ya wanawake hao kabla ya kuitelekeza (12) anaonekana kupenda sana wanawake na huwa anaangalia picha za ngono (13) kunauwezekano aliwahi kunyanyaswa kijinsia alipokuwa jela hususan jela ya watoto.

 (14) anaonekana kuwa na akili sana na ni kijana wa mtaani aliyebobea kwenye vitendo vya kihalifu.Mkoba wa mmoja wa wanawake waliouawa na kutelekezwa katika eneo la Boksburg ulikutwa na nyaraka ambazo ndizo zilizosababisha mwili huo utambuliwe kuwa ni wa Amelia Rapodile. Askari wa upelelezi walipofuatilia mahali alipokuwa akifanya kazi, wafanya kazi wenzie walidai kwamba alikuwa na miadi na mtu aliyemtaja kwa jina la Moses Sethole mnamo Septemba 7. Hiyo ndiyo siku aliyotoweka.

 Polisi pia walikuta barua ya maombi ya kazi kwenye taasisi ya Sethole iliyotajwa kwa jina la Youth Against Human abuse organization, ambapo alikuwa amemwahidi kumuajiri Amelia.Walipofuatilia kwa kutumia namba za simu zilizokutwa kwenye maombi ya kazi walikutana na mwanamke alijitambulisha kwa jina la Kwazi Sithole anayeishi katika eneo la Wattville kusini mwa mji wa Boksburg. Alikuwa ni dada yake Moses. 

Lakini aliwambia askari wa upelelezi kwamba Sithole haishi pale na hajulikani mahali alipo.Kuanzia hapo askari wa upelelezi wakajua kwamba wanaye mtu sahihi aliyehusika na mauaji hayo na si mwingine bali ni Moses Sithole.Kutokana na taarifa za mauiaji hayo kusambaa nchi nzima, na kuleta hofu miongoni mwa jamii ya wa Afrika Kusini, Polisi walitangaza zawadi nono kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea muuaji huyo kukamatwa. 

Pia aliyekuwa raisi wa chi hiyo wakati huo Nelson Mandela aliingilia kati jambo hilo na kuwahimiza Polisi wakakikishe muuaji anakamatwa haraka iwezekanvyo na kurejesha utulivu kwa wananchi wa nchi hiyo ambao walikuwa wametaharuki kutokana na mauaji hayo.

Mnamo Octoba 3, mtu mmoja alipiga simu katika gazeti maarufu la The Star la nchini humo na kuongea na mwandishi wa habari aitwae Tamsen de Beer. 

 Mtu huyo alijitambulisha kwa jina la Joseph Mangwena na alidai kwamba ndiye anayehusika na mauaji Gauteng (Gauteng ni jimbo yalipo majiji la Johannesburg na Pretoria). Kwa kauli yake mwenyewe mtu huyo alisema kwa utulivu. “Mimi ndiye mtu ninayetafutwa kwa udi na uvumba.” Alisema kwamba anataka kujisalimisha. Mwandishi huyo wa habari aliwasiliana na Polisi. 

Mtu huyo alipiga simu mara kadhaa katika ofisi za gazeti hilo na simu yake ilirekodiwa. Na katika maelezo yake kwa mwandishi huyo wa habari alieleza kwa undani jinsi alivyotekeleza mauaji hayo. Alidai kwamba alianza kuuwa baada ya mwanamke mmoja kumtuhumu kimakosa kwamba alimbaka ambapo alishitakiwa na kuhukumiwa kwenda jela. Wakati alipokuwa jela aliteswa sana na wafungwa wenzake. “Nilipotoka niliamua kulipiza kisasi. 

Nilikuwa namlazimisha mwanamke ninayetaka kumuuwa kwenda mahali ninapotaka na tunapofika hapo ninamwambia, ‘Unajua kwa nini?’ Niliteseka sana na sasa ni wakati wangu kulipiza kisasi, na ndipo huwauwa.” 

Alisema mtu huyo katika mazungmzo yake kwa njia ya simu na mwandishi huyo wa habari. Alisema kwamba alikuwa anatumia nguo za wahanga wake kuwanyongea na alikuwa anapendelea chupi zao kwa sababu haziachi alama za vidole. Aliendelea kusema kwamba baadhi ya wanawake aliowauwa walikuwa wakishuhudia maiti za wenzao aliowaua na kutelekeza miili yao mahali hapo. 

Hata hivyo alikanusha kuhusika na mauaji ya Letta Ndlangamandla na mwanaye wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 2. Alidai kwamba yeye anawapenda watoto hivyo asingeweza kumuua mwanamke huyo wala mtoto wake.Alielezea mahali alipotelekeza miili mingine ambayo Polisi walikuwa hawajaiona. Kutokana na maelezo hayo waliamini kwamba huyo ndiye muuaji waliyekuwa wakimtafuta.

Hata hivyo kutokana na ugumu wa kumpata huyo muuaji aliyepiga simu, askari wa upelelezi waliamua kuendelea kumtafuta mtuhumiwa wanayemfahamu Moses Sethole. Walitoa picha zake kwenye magazeti hapo mnamo Octoba 13, na waliwaomba wananchi wasaidie kupatikana kwa mtu huyo.

Siku chache baada ya picha yake kuwekwa magazetini, Sithole aliwasiliana na shemejie aliyemuoa dada yake akimuomba amtafutie bunduki ya kujilinda.

Walikubaliana na shemejie wakutane kwenye eneo la viwanda la Mintex lililopo katika mji wa Benon ambapo atapewa hiyo silaha. Dada yake aliwasiliana na Polisi na kuwaeleza kuhusu ombi la Sithole kwa shemejie la kutaka atafutiwe silaha ya kujilinda. Kapteni Vinol Viljoen na Frans van Niekerk waliona huo ndio wakati muafaka wa kumtia muuaji huyo mbaroni. 

Walikutana na uongozi wa kiwanda na kukubaliana kuwa Inspekta Francis Mulovhedzi ajifanye ni mlinzi wa kiwanda akae getini. Ilipofika saa 9 usiku mnamo Octoba 18, 1995, Sithole aliwasili na kumuulizia Maxwell. Askari aliyekuwepo getini alimwambia Inspekta Mulovhedzi aende kumtafuta Maxwell ndani ya kiwanda. 

 Kwa kuwa alikuwa ni mgeni pale na hakutaka kumuachia Sithole aondoke, alikataa kwenda ndani kumtafuta Maxwell, jambo hilo lilileta ubishani kidogo na hivyo kumfanya Sithole ajenge wasiwasi na kukimbia kutoka katika eneo hilo.Inspekta Mulovhedzi alimfuata kule gizani alipokimbilia. Alijitambulisha kama Afisa wa Polisi akimpigia Sithole kelele asimame na kupiga risasi mbili hewani. 

Pamoja na kwamba katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na mwandishi wa habari alidai kwamba anataka kujisalimisha, lakini hakujisalimisha kirahisi kama ilivyotarajiwa. Alimjia yule Polisi akiwa na shoka. Ili kujihami askari huyo alimpiga risasi ya miguuni hata hivyo pamoja na kupigwa risasi lakini aliendelea kutaka kumpiga askari huyo na shoka ambapo alimpiga tena risasi ya miguuni mpaka akaanguka. 

Alikuwa amepigwa risasi ya miguuni na tumboni hivyo alikimbizwa katika hospitali ya Glynwood iliyoko Benoni ambapo alifanyiwa upasuaji siku iliyofuata.

Wakati Brigedia Suike Britz Kamanda wa kitengo cha mauaji na ujambazi wa kutumia silaha alipopata taarifa za Sithole kupigwa risasi, moyo wake ulisimama kwa sekunde kadhaa kwa mshtuko. Baadaye akizungumzia tukio hilo alisema, 

“Ilikuwa kama déjà vu kutokana na kufanana kwa usahihi kabisa na tukio la kuuawa kwa David Selepe, tukio ambalo hadi sasa vyombo vya habari vimelishupalia wakitushutumu kwa uzembe. Nilisali wakati wote nikihofu kwamba Sithole naye angekufa na nilikuwa napiga simu kila saa ili kufuatilia hali ya afya yake.” (Déjà vu ni kitendo cha kufanana kwa jambo au matukio).

Hata hivyo Sithole alipata nafuu na hivyo kuhamishiwa katika hospitali ya kijeshi iliyoko katika jiji la Pritoria, ambapo ulinzi uliimarishwa. 

Habari ya kukamatwa kwa Moses Sithole zilisambaa nchini humo kama moto wa mwituni.Mnamo Octoba 28 magazeti nchini humo yaliripoti kwamba Sithole alikutwa na Maradhi ya Ukimwi (HIV), hata hivyo Polisi hawakutoa maoni yao kuhusiana na taarifa hizo. Ilidaiwa kwamba kuna uwezekano maradhi hayo aliyapata kutoka kwa mmoaj wa wahanga wake aliowabaka na kuwauwa.

Wakati huo huo askari wa upelelezi Viljoen na Frans Van Niekerk walimtembelea Sithole hospitalini kwa ajili ya kumuhoji, lakini alikuwa mkaidi kujibu maswali yao. Alipoingia askari mwanamke kumuhoji alikiri baadhi ya mauaji aliyoyafanya na kitendo cha kupiga punyeto kwenye miili ya wanawake hao baada ya kuwauwa. Mahojiano hayo yalirekodiwa.Kwa maneno yake mwenyewe Sithole alisema. 

“katika eneo la Atterdgeville niliuwa wanawake labda kumi hivi, siwezi kukumbuka kwa usahihi, nilikuwa nawakamata kwa mikono yangu shingoni na kuwanyonga na wakati mwingine nilikuwa natafuta kitu kama kamba ya kuwanyongea. Nilikuwa natumia soksi ya viatu na kuwafunga shingoni na kisha kuwanyonga. Mimi sipendi kuona damu. Nilikuwa nawalazimisha kulala kifudifudi wakati nikiwabaka na baada ya kufanya hivyo nawanyonga na wakati nikiwaangalia wakifa, napiga punyeto juu ya miili yao.

Sithole alikanusha kushirikiana na mtu yeyote katika kutekeleza mauaji hayo lakini alisema kwamba kuna uwezekano kuna mtu mwingine aliyekuwa akifanya mauaji sambamba na yeye. Mnamo Novemba 3, Sithole aliruhusiwa kutoka hospitalini na kupelekwa katika jela ya Boskburg, jela ambayo aliwahi kufungwa wakati fulani kwa kosa la kubaka. 

Jela hiyo iko jirani kabisa na eneo alilokuwa akiitelekeza miili ya wanawake aliokuwa akiwauwa.Baadae aliwapeleka Polisi sehemu mbalimbali ambazo alitelekeza miili ya wanawake wengine aliowauwa ambapo baadhi ya sehemu hizo hazikupata kujulikana na polisi.

Mnamo Mei 20, Sithole alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na baada ya kusomewa mashitaka kesi iliahirishwa mpaka baaba ya miezi mitano ndipo itakapoanza kusikilizwa rasmi. Alikuwa akitetewana wakili wa kujitegemea aitwae Eben Jordaan ambapo gharama za kumtetea zilibebwa na serikali ya Afrika ya Kusini.

Mnamo Octoba 28, Moses Sithole alifikiswa mahakamni na kusomewa mashikiwa kwa makosa mauaji ya wanawake 38 akiwemo mtoto mmoja wa miaka 2, makosa 40 ya ubakaji na makosa 6 ya uporaji wa kutumia silaha. Sithole alikanusha mashitaka hayo.

Mnamo Desemba 5, 1997, Sithole alihukumiwa cha miaka 50 kwa kila kosa la mauaji ya wanawake 38, miaka mingine 12 kwa kila kosa la ubakaji wa wanawake 40 na miaka 5 kwa kila kosa la ujambazii wa kutumia silaha. Kwa kuwa kifungo cha makosa hayo kitaenda pamoja, alitakiwa atumikie kifungo cha miaka 2,410. Mheshimiwa Jaji David Carstairs aliagiza atumikie angalau kifungo cha miaka 930, ndipo afikiriwe kupewa fursa ya kutumikia kifungo cha nje (Parole).

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .