MTUHUMIWA MUHIMU KESI YA MAUAJI YA BILIONEA WA TANZANITE ERASTO MSUYA AMEFIKISHWA MAHAKAMANI LEO
Posted in
No comments
Tuesday, October 15, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
Mmoja wa askari akijaribu kutoa maelekezo kwa mtuhumiwa wa mauaji ya mfanyabiashara wa madini Erasto Msuya wakati akielekea chumba cha mahakama ya hakimu mkazi mjini Moshi. |
Ndugu wa marehemu Erasto Msuya wakiwa nje ya jengo la mahakama ya hakimu mkazi mjini Moshi wakitizama watuhumiwa wa mauaji ya ndugu yao. |
Watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini Erasto Msuya wakitolewa katika chumba cha mahakama mara baada ya kuahirishwa kwa shitaka linalo wakabili. |
Watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini Erasto Msuya wakitolewa katika chumba cha mahakama mara baada ya kuahirishwa kwa shitaka linalo wakabili. |
Mtuhumiwa namba mbili, Shaibu Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredi (38) anayetuhumiwa kushiriki Mauaji ya mfanyabiashara wa madini Erasto Msuya, akisaidiwa kupanda katika gari mara bada ya kuahirishwa kwa shitaka linalo wakabili. |
Mtuhumiwa huyo aliyekamatwa Oktoba 8, mwaka huu, alinaswa mkoani Kigoma akijaribu kutorokea nchini Burundi baada ya kufanikiwa kukimbia mitego ya polisi katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Mwanza na kurudishwa mkoani kilimanjaro ambapo jana aliunganishwa katika kesi ya Mauaji ya Msuya.
Akisoma Mashtaka yanayomkabili Mtuhumiwa huyo mbele ya Mahakama ya Hakimu Munga Sabuni, Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Janet Sekule alisema Mshtakiwa huyo pamoja na wenzake Saba, wanashtakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia kinyume cha kinyume cha kanuni namba 16,kifungu cha 196 ya sheria za makosa ya jinai, “Kinyume cha sheria ya makosa ya jinai, kanuni ya 16, kifungu cha 196, Ally Mussa au kwa jina lingine Majeshi, walimuua Erasto Msuya katika maeneo ya Mjohoroni, njia panda ya Arusha na KIA kwa kumpiga risasi,” alisema Sekule.
Aidha baada ya kusoma maelezo ya shtaka hilo, upande wa Jamhuri, ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Janet Sekule iliiomba Mahakama ya Hakimu Sabuni kuipa muda kuweza kukamilisha upelelezi ambapo kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 28, mwaka huu, itakapo tajwa tena.
Ally Mussa “Majeshi”, anayedaiwa kuwahi kulitumikia Jeshi la kujenga Taifa (JKT), kabla ya kufukuzwa anaungana na Sharif Mohamed Athuman (31) mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredi (38), mkazi wa Songambele Wilaya ya Simanjiro.
Wengine ni Joseph Damas Mwakipesile maarufu kama Chusa (36), mfanyabiashara wa madini na mkazi wa Arusha, Jalila Zuberi Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Mohammed Jabir ‘Msudani’ au ‘Mnubi’(32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata wilayani Hai na Karim Kihundwa (33) mkazi wa Kijiji cha Lawate Wilaya ya Siha na Mussa Juma Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu mkoani Arusha.
Hata hivyo Mwandishi wa Habari hizi alishuhudia kesi hiyo ikisomwa katika hali ya utulivu tofauti na ilivyozoeleka kwani katika mara zote kesi hiyo ilipofikishwa Mahakamani hapo kulikuwa na umati mkubwa wa watu wakiwemo ndugu za Marehemu Erasto Msuya.
Mfanyabiashara Erasto Msuya, aliuawa Agosti 7, mwaka huu majira ya 6:30 mchana kwa kupigwa risasi 13 kifuani, kando ya barabara kuu ya Arusha– Moshi katika eneo la Mjohoroni, Wilaya ya Hai, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :