BARAZA LA MAWAZIRI;PRESHA INAPANDA PRESHA INASHUKA
Posted in
No comments
Sunday, December 22, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
JOTO
la nani ataondolewa kwenye Baraza la Mawaziri na nani atateuliwa
limeanza kupanda miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tayari majina kadhaa yameshaanza kutajwa kurithi viti vya mawaziri
wanne walioondolewa madarakani juzi na Rais Jakaya Kikwete, baada ya
wizara zao kuhusishwa na Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyoendeshwa kwa
misingi ya kukiuka haki za binadamu.
Mawaziri walioondolewa madarakani ni Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii),
Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani) na David Mathayo (Mifugo na Uvuvi).
Kuondolewa kwa mawaziri hao pia kunaelezwa kumelenga kumnusuru Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amekuwa akitajwa kwa kushindwa kuwasimamia
mawaziri walio chini yake.Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa hatua hiyo pia itamsaidia Rais
Kikwete kutimiza mapendekezo ya Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyotaka
awaondoe mawaziri saba iliyowaita ‘mizigo’.
Iwapo Rais Kikwete ataridhia pendekezo hilo, itamlazimu ateue
mawaziri wengine 10, huku akikabiliwa na mtihani mkubwa wa kumuondoa
Pinda.Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa baadhi ya wabunge ambao
wamekuwa wakiikosoa zaidi serikali wanaandaliwa nafasi za uwaziri kwa
lengo la kuwaziba mdomo.
Hoja hiyo inashibishwa na uteuzi aliowahi kuufanya Kikwete huko nyuma
kwa kuwateua Dk. Harrison Mwakyembe, Januari Makamba na George
Simbachawene walioonekana kuwa mwiba kwa serikali katika uchangiaji wa
mijadala mbalimbali ndani na nje ya Bunge.
Wanaotajwa kuteuliwa kwenye uwaziri ni Dk. Asha Rose Migiro, Zakhia Meghji, Kangi Lugola na James Lembeli.Tanzania Daima Jumapili, liliwasiliana na Lembeli juu ya tetesi hizo
ambapo alisema ukosoaji wanaoufanya unalenga kuboresha utendaji wa
serikali na wala si kutafuta vyeo.
Pinda ang’ang’aniwa
Wakati homa ya uteuzi wa mawaziri ikionekana kuwatia kiwewe mawaziri
na wabunge, wadau mbalimbali wametaka Pinda kung’oka kwa madai kuwa
ameshindwa kuwaongoza mawaziri walio chini yake.
Pia wanataka kubadilishwa kwa mfumo wa utendaji wa serikali ambao umekuwa ukilinda, kufadhili maovu mbalimbali.
Mbunge wa Mwibara, Lugola (CCM), alisema Pinda asipong’oka bado
mawaziri watakaoteuliwa wataendelea kuwajibika kwa kiwango cha chini.Alisema Pinda ana tatizo la upole jambo aliloeleza kuwa halina dawa
na kwamba hata mawaziri walioondolewa kwa kiasi kikubwa walipaswa kupata
maelekezo bora kutoka kwake.
“Pinda kazidi upole, ni afadhali aondoke hapo akae mtu asiyewachekea
watendaji wazembe. Kama utakumbuka kabla hata ya taarifa ya operesheni
hii kulikuwa na malalamiko katika wizara mbalimbali juu ya utendaji wao,
na Pinda ni mdau katika wizara zote,” alisema Lugola.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), alisema kuondoka
kwa mawaziri hao hakutabadili lolote, kwa kile alichoeleza kuwa wengi
wameshajiuzulu au kufukuzwa kabla ya hapo, na hakuna mabadiliko ukiachia
maeneo machache kama madini na uchukuzi.
Alisema mfumo mzima umeoza na kwamba changamoto za Watanzania ni zaidi ya watu na vyama vyao.
“Uwezo wa wanasiasa kubadili mfumo ni mdogo sana, nchi inahitaji
mapinduzi! Wanasiasa wanahubiri status quo… Mauaji kama ilivyo ufisadi
yamekuwa ni sehemu ya utamaduni wetu na sasa inageuka kuwa hulka ya nchi
yetu kiasi kwamba hata wale enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere
tuliwaita manyang’au sasa wanatushangaa jinsi tunavyojimaliza,” alisema
Zitto.
Aliongeza kuwa hatua nchi ilipofikia ni zaidi ya tatizo la kisiasa,
uongozi ama mfumo, na kwamba tatizo la mauaji, ufisadi na maovu mengine
yanakuwa ni sehemu ya utamaduni wa nchi.Mwanahabari mkonge nchini, Jenerali Ulimwengu alisema wanaweza
kubadilishwa mawaziri wote na kusiwe na mabadiliko ya aina yoyote kwa
kile alichoeleza suluhisho ni kubadili mfumo.
Ulimwengu alitaka Pinda asilaumiwe pasi kuangalia utendaji wa ofisi
yake kama ina uwezo wa kufanya uamuzi dhidi ya watendaji wengine wa
serikali.“Sidhani kama tatizo ni Waziri Mkuu, ofisi hiyo haina maelezo ya
kutosha, haina madaraka, haimfanyi kiongozi huyo afanye kazi yake
ipasavyo… huu ni mfumo unaopaswa kubadilishwa,” alisema Ulimwengu.
Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema si jambo rahisi kutenganisha utendaji wa Bunge na serikali.Alisema Bunge limejaza wabunge wengi wa chama kimoja jambo linalochangia baadhi ya mambo kutokwenda kwa hali inayotakiwa.
Bashiru alisema Bunge linapaswa lijitafakari kama kazi yao itakuwa ni
kufukuza mawaziri badala ya kuhakikisha mfumo wa uongozi unabadilika.Aliongeza kuwa kama Bunge limedhamiria kufanya kazi yake linapaswa
lianike hadharani ripoti ya kamati iliyoenda Mtwara katika sakata la
wananchi dhidi ya gesi badala ya kuchagua ripoti za kutoa hadharani.
Dk. Slaa aing’ang’ania CCM
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amesema chama chake
kitapita nchi nzima kuelezea kile kilichodai kuwa ni ‘ukweli wa
udhalimu’ wa serikali (ya CCM), iwapo Pinda hawatawajibika kwa makosa
ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Chama hicho kimewataka Watanzania wote waungane kupiga kelele za
kudai uwajibikaji wa serikali kutokana na damu ya watu iliyomwagika
kutokana na mateso na vifo wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Alisema kuwa serikali haiwezi kusafishika kwa mawaziri wanne kuondoka
madarakani, bali kwa wote waliohusika kuwajibika au kuwajibishwa.Akihutubia mikutano ya hadhara katika maeneo ya Lusu na Nzega mjini
mkoani Tabora jana, Dk. Slaa, alisema Pinda na watendaji wengine
waliohusika katika usimamizi wa opereseheni hiyo hawawezi kukwepa
uwajibikaji kutokana na makosa yaliyofanyika, ikiwemo mauaji.
“Tunataka kumwambia Kikwete serikali yake imezidi kuchafuka.
Imechafuka sana. Haiwezi kusafishika kwa mawaziri wanne kuondolewa
katika nafasi zao. Watanzania wanataka kuona Waziri Mkuu anawajibika.
Hakuna mzaha katika damu ya watu.
“Watu wameteswa kwa mateso ya kila aina, ikiwemo kuwekewa chupa na
‘spoke’ sehemu za siri, watu wamepigwa, watu wameuawa, watu wamebakwa.
Diwani wangu pale Serengeti amefanyiwa ukatili mkubwa, Waziri Mkuu yupo,
hakuwahi hata kutoa kauli bungeni.
“Mawaziri walioondoka hata hawakuwemo kwenye ile orodha yao wenyewe
CCM waliosema ni mizigo… nafikiri David Mathayo tu alikuwemo… sasa
unaweza kuona namna gani serikali hii imeoza.“Hawa walikuwa wabovu bado na wale wengine sita waliowataja wenyewe,
yupo na mwingine anaitwa Prof. Muhongo ni mzigo na muongo vile vile.
Kikwete aunde serikali upya.
“Hakuna suala kubwa linaweza kuvuka haki za binadamu, tena linalohusu
uhai wake. Kama Kikwete hamwajibishi Pinda na watendaji wake
waliohusika katika unyama huu, tutachanja mbuga nchi nzima kuwaeleza
ukweli Watanzania. Tuna ushahidi wa yote yaliyofanyika.
“Watanzania pazeni sauti, pigeni kelele Mizengo Pinda aondoke. Hapa
tunazungumzia haki za binadamu waliouawa na kuteswa. Mifano ni mingi
sana… serikali hii haiwezi kusafishika kwa mawaziri wanne tu.
Tutawaeleza Watanzania namna ambavyo Serikali ya CCM yenyewe ndiyo mzigo
unaozidi kuelemea Watanzania kwa kuwatesa na kuwaua,” alisema Dk. Slaa.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :