KILIMANJARO MARATHON YATANGAZA NJIA MPYA.
Posted in
Michezo
No comments
Sunday, February 16, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
Waandaaji wa mbio za Kilimanjaro Marathon wametangaza njia
mpya zitakazotumika kwa mbio za mwaka huu ikiwa ni hatua nyingine muhimu katika
mafanikio ya mbio hizo ambazo sasa zinaingia mwaka wa 12 tangu kuanzishwa. Njia
mpya zimelenga kuboresha mwendo wa washiriki barabarani na kuwafanya wafurahie
zaidi mbio hizo zilizopangwa kufanyika tarehe 2 Machi, 2014 mjini Moshi.
Akitangaza njia hizo mpya jana, John Addison, Mkurugenzi wa
Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo alisema alisema: Tumeanzisha njia mpya
ili kuzuia msongamano wa watu wakati wa mbio kutokana na kuongezeka idadi ya
washiriki kila mwaka. Washiriki wa mbio ndefu za marathon ya km 42, nusu
marathon km 21, mbio ya walemavu na mbio ya kujifurahisha ya Vodacom 5km Fun
Run sasa hawatapishana tena barabarani bali kila njia itatiririka katika
muelekeo mmoja.
“Pia kutokana na mabadiliko haya washiriki watakuwa wameepuka
kilomita 3 za mwinuko mkali kuelekea Chuo cha Mweka ambapo awali ndio palikuwa
mahali pa kugeuzia washiriki wa mbio za full marathon na nusu marathon. Mbio ya
walemavu za Gapco ambazo zitakuwa na makundi mawili tu mwaka huu ya kiti cha
magurudumu (wheelchair) na baisikeli ya mikono (handcycle) imefupishwa kutoka
nusu marathon na kuwa kilomita 10 ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi
kushiriki na njia sasa itapita eneo tambarare na lenye kivuli.
Mkurugenzi wa Wild Frontiers ambao ni waandaaji wakuu wa Kilimanjaro Marathon, John Addison(kulia) Akizungumza na Meneja wa Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe. |
Mbio ndefu za Kilimanjaro Premium Lager 42km Marathon
zitaanza saa 12.30 asubuhi kutokea uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara
(MUCCoBS) na kuelekea barabara iendayo Dar es salaam kwa kilomita kumi na
kurudia geti la ushirika halafu zitaenda kilomita 8 kuelekea hospitali ya KCMC
na kukata kushoto hadi Barabara ya Lema (Lema Road). Wanariadha watatelemka na
Lema Road wakitelemka kupitia shule ya ISM halafu watamalizia na kipande
tambarare cha Barabara ya Kilimanjaro na kipande cha mita chache za barabara ya
Sokoine kuelekea uwanjani.
Mkurugenzui wa Executive Solution ambao ndio waratibu wa mbio za Kilimanjaro Marathon, Aggrey Mareale (katikati) katika moja ya matukio ya uzinduzi wa mbio hizo. |
Mbio za Nusu Marathon zitaanza saa moja kamili asubuhi
kutokea MUCCoBS na kupandisha kaskazini kuelekea hospitali ya KCMC kwa kilomita
8 ambazo ni sawa na ongezeko la mwinuko wa futi 250 kutoka usawa wa bahari.
Halafu mbio hizo pia zitapita njia ya Lema Road na kurudi uwanjani.
Addison alisema kuwa mbio za full marathon na nusu marathon
zinapita kwenye maeneo mbalimbali yenye vivutio na mandhari nzuri ya mji wa
Moshi na sehemu zenye mandhari ya mashamba ya kahawa na migomba jambo ambalo pia
litawavutia wananchi wengi kujitokeza kuwashangilia wanariadha.
“Njia zote zitakuwa na vituo vya maji vya kutosha ili
kuwafanya wanariadha wafurahie mbio bila kushikwa na kiu muda wote wa mbio.
Vilevile, njia nzima itakuwa na madaktari na wauguzi wa kutoa huduma ya kwanza
pamoja na magari ya kutosha ya wagonjwa huku mamlaka husika zikidhibiti usalama
wa wanariadha barabarani. Madaktari wengine na wauguzi wataukuwa uwanjani
ambapo kutakuwa na zahanati ya dharula kwa ajili ya huduma ya kwanza na kuchua
misuli.
Mbio ya walemavu ya Gapco Disabled 10km Marathon itaanzia
uwanja wa MUCCoBS na kufata barabara ya Kilimanjaro halafu mpaka Lema Road na
kugeuza.
Addison alisema mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run
zitaanzia kwenye mzunguko wa YMCA upande wa barabara ya Arusha na zitaenda hadi
kwenye mnara wa saa halafu kupita Boma Road
kuelekea mzunguko (roundabout) wa barabara ya Arusha na mzunguko wa YMCA
tena na watapita Uru Road na kuingia uwanjani kupitia geti la mashariki.
Executive Solutions ni waratibu wa mbio za Kilimanjaro
Marathon 2014 wakishirikiana na Riadha Tanzania, Chama cha Riadha Kilimanjaro
na Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
(wadhamini wakuu), Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement, and KK Security among
others, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB
Tanzania, UNFPA na Kilimanjaro Water.
Mwisho.
NB: Ramani zinapatikana kwenye tovuti ya www.kilimanjaromarathon.com
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :