POLISI YAMSHIKILIA ALIYEMUUA HAWARA KIKATILI KILIMANJARO
No comments
Monday, February 10, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
Mwandishi wetu, Moshi.
Polisi mkoani Kilimanjaro inamshikilia mfanyabiashara mmoja wa mjini Moshi
baada kumuua kikatili mpenzi wa nje (hawara) kwa Rato baada ya mwanamke huyo
kukataa kumpa penzi.
Mwanamke huyo
alikataa kumpa penzi hawara yake huyo ambaye ni mume wa mtu, akitaka ampe
kwanza Sh10,000 kwani katika muda wa miaka miwili ya mahusiano yao hakuwahi
kumpa kitu.
Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz jana
alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa ambaye baada ya kumuua mpenzi wake,
Sekunda Mushi(42), alitupa maiti yake kwenye shimo la taka.
Mtuhumiwa huyo ni baba mwenye familia ya watoto wawili na
ana mke wake wa ndoa na wanaishi eneo la Kiborlon mjini Moshi na alikuwa na
uhusiano wa siri wa kimapenzi na marehemu.
Tukio hilo ambalo limekuwa gumzo katika mitaa mbalimbali ya
mji wa Moshi, lilitokea wiki iliyopita usiku wa manane katika eneo la Kosata
katika kijiji cha Longuo A nje kidogo ya mji wa Moshi.
“Huyo mtuhumiwa alimchukua mpenzi wake (marehemu)
wakaingia chumbani lakini wakahitilafiana … marehemu alikuwa anataka apewe pesa
lakini mwanamme akawa hataki”alisema Kamanda Boaz.
Habari zaidi zimedokeza marehemu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi
na mtuhumiwa kwa takribani miaka miwili mfululizo na katika kipindi chote,
alikuwa hajawahi kumpa pesa yoyote mpenzi wake huyo.
“Siku hiyo usiku walipoingia chumbani mwanamke akamwambia
kwa miaka yote hujawahi kunipa hata shilingi moja leo sikupi penzi mpaka unipe
Sh10,000”alidokeza polisi mmoja wa upelelezi.
Mara zote wakifanya mapenzi ndani ya chumba cha
mfanyakazi wa Grosari yake iliyopo Longuo A, mfanyakazi huyo alikuwa akilala
kitanda kimoja na wapenzi hao wawili akishuhudia mapenzi yao.
Akimkariri mfanyakazi Polisi huyo, alidai kitendo cha
kupewa sharti hilo la kutoa Sh10,000 angalau kwa siku hiyo ndani ya miaka
miwili ya mahusiano yao kilionekana kumuudhi mtuhumiwa.
“Yule jamaa akaanza kumpiga kipigo cha nguvu na kama
haitoshi akachukua Rato yenye meno matatu na kumpiga nayo kichwani ikaangia na
kutokea mdomoni kwa chini”alidokeza polisi huyo.
Inadaiwa kuwa, mtuhumiwa alimgeuza mwanamke huyo na
kuendelea kumpiga na rato mgongoni mithili ya mtu anayelima shamba na kisha
kumburuza na kumtupa kwenye shimo la taka.
“Wakati yote hayo yakiendelea Yule mfanyakazi wake
alikuwa akishuhudia na alipomtupa kwenye shimo la takataka akamtisha mfanyakazi
wake kuwa kama atamweleza mtu naye angemuua”alisema.
Kwa mujibu wa Polisi huyo, baadae mtuhumiwa alimwamuru
mfanyakazi wake huyo kwenda kuificha Rato iliyotumika katika mauaji hayo juu ya
dari ya chumba hicho ili kuficha uhalifu wake huo.
Baadae mtuhumiwa aliondoka kwenda kijijini kwao huko
Marangu Moshi Vijijini hadi alipokamatwa na wananchi na alipoulizwa kuhusu
mauaji hayo alikana na ndipo akapelekwa kituo kikuu cha Polisi.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Longuo A, Marcel Benard
Mushi, alisema waligundua kuwapo kwa mwanamke katika shimo la taka saa 11:00
alfajiri na wakati huo bado alikuwa yupo hai.
“Tulimkuta katika hali mbaya alikuwa na majeraha ambayo
kwa kweli huwezi kuamini yametokana na mwanadamu na aliomba maji ya kunywa
lakini kabla hatujampatia akakata roho”alisema Mushi.
Kaka wa marehemu, Goodluck Mushi alisema dada yao alikuwa
ameondoka nyumbani kwa siku mbili mfululizo na walikuwa wakimtafuta hadi
walipopewa taarifa saa 3:00 asubuhi kuwa ameuawa.
Ndugu huyo anasema wanavyofahamu wao, siku alipouawa ndio
ilikuwa mara ya kwanza kwenda kwenye Grosari inayomilikiwa na marehemu na ndio
siku ambayo walianza uhusiano na mtuhumiwa.
Mazishi ya mwanamke huyo yalifanyika juzi Jumapili baada
ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi na madaktari wa hospitali ya rufaa ya KCMC
ili kubaini nini hasa chanzo cha kifo chake.
Mwisho
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :