UVCCM WAFANYA BARAZA LA WILAYA NA KUCHAGUA VIONGOZI WAPYA WA MAJIMBO, TEMEKE

Posted in ,
No comments
Sunday, February 16, 2014 By danielmjema.blogspot.com

Mbunge wa Kigamboni Ndugu Faustine Ndungulile (aliyevaa kovia na ameshika kipaza sauti) akiwa tayari meza kuu. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Vijana (W) Temeke Ndugu Oliver Mwambope, Katibu wa UVCCM (W) Temeke Ndugu Amour Onesha, Katibu Uhamasishaji na Chipukizi (W) Temeke Ndugu Sabuni. Kushoto kwa Mbunge Ndugu Ndungulile ni Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji (W) Temeke Fanny Abdul, Ernest Mwingira na Fikiri Mzome. Picha na Emmanuel Shilatu

Wajumbe wa Baraza la UVCCM (W) Temeke wakiwa wenye nyuso za furaha wakati wakimkaribisha Mgeni rasmi Mbunge wa jimbo la Kigamboni Ndugu Faustine Ndungulile.

Mgeni rasmi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kigamboni Ndugu Faustine Ndungulile akifungua rasmi Baraza la kazi la UVCCM (W) Temeke mbele ya Wajumbe (hawapo pichani) lililofanyika kwenye ukumbi wa Malaika uliopo Kata ya vijibweni, Jimbo la Kigamboni.

Wagombea wa nafasi za Uenyekiti na Ukatibu wa Majimbo ya Kigamboni na Temeke ya UVCCM.

 Mmojawapo wa wagombea ambaye alikuja kushinda nafasi ya Uenyekiti wa Jimbo la Kigamboni kupitia UVCCM akichukua karatasi ya kupigia kura.

 Mjumbe wa Baraza la UVCCM, Ndugu Emmanuel John akichukua karatasi ya kupigia kura.
 Mjumbe wa Baraza Ndugu Dude akipiga kura yake.

 Mjumbe wa Baraza Ndugu Yasin Kanyama akiikusanya kura yake aliyoipiga.
Mjumbe wa Baraza la Vijana UVCCM Ndugu Emmanuel John akiikusanya kura yake aliyoipiga. Picha zote na Emmanuel Shilatu
**********
Na Emmanuel  J. Shilatu
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi wilaya Temeke wamefanya Baraza la Wilaya kikatiba lililokuwa ni Baraza la kikazi zaidi ambapo pamoja na mambo mengineyo walifanya uchaguzi wa majimbo yaliyopo ndani ya Wilaya hiyo na kupata Wenyeviti na Makatibu wapya wa majimbo.

Baraza hilo la Vijana ambalo lilifunguliwa na Mgeni rasmi Mbunge wa Kigamboni, Ndugu Faustine Ndungulile ambaye wakati wa ufunguzi aliwaasa vijana kujiepusha na matumizi ya madawa ya kulevya na kujikinga zaidi na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwani hali iliyopo inatisha sana kwa vijana.
“Kati ya vijana wa kike watatu wanaotumia madawa ya kulevya, wawili kati yao ambao ni asilimia 67 wameathirika na virusi vya ukimwi. Halikadhalika kwa upande wa vijana wa kiume wawili wanaotumia madawa ya kulevya, mmojawao ambaye ni asilimia 50 ana maambukizi ya virusi vya ukimwi. Hali ni mbaya sana kwa vijana.” Alisema Mhe. Ndungulile.

Ndugu Ndungulile ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Temeke aliwaasa na kuwatia moyo vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za kiuongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa  na uchaguzi mkuu hapo mwakani naye kwa nguvu zake zote atapambana katika kuwatetea vijana wenye sifa stahiki kwani anaamini vijana ni nguvu kazi ya sasa ya Taifa.

Ndugu Ndugulile aliwaasa na kuwatakia uchaguzi mwema wajumbe wa Baraza hao wachague viongozi wenye sifa wanaowataka kwani yeye kama Ndugulile ameanika waziwazi kuwa hajashirika hata chembe katika kupanga safu za viongozi badala yake jukumu hilo limeangukia mikononi mwao wajumbe hao.
Kwenye baraza hilo la Vijana ambalo lilikuwa ni baraza la kazi waliwachagua viongozi wa majimbo ya kigamboni na Temeke yanayopatikana ndani ya Wilaya ya Temeke.

Kwa upande wa jimbo la Temeke waliojitokeza kuomba nafasi ya Uenyekiti ni  Arnord Sangawe aliyepata kura 48, Julius Mkada aliyepata kura 24 na Peter Sillo aliyepata kura 4. Mshindi wa nafasi ya Uenyekiti wa Jimbo la Temeke UVCCM ulinyakuliwa na Arnord Sangawe.

Halikadhalika waliojitokeza kwenye nafasi ya Ukatibu walikuwa ni Athumani Nyamlani aliyepata kura 6, Juma Ndwangila aliyepata kura 59 pamoja na Laurence Limwata aliyeapata kura 11. Hivyo nafasi ya Ukatibu wa jimbo ulichukuliwa na Ndugu Juma Ndwangila.

Kwa upande wa jimbo la Kigamboni wagombea wa nafasi ya  Uenyekiti wa jimbo walikuwa ni Ally Makwilo aliyepata kura 28, Shaaban Mbegu aliyepata kura 7 na Yasin Kanyama aliyepata kura 43. Hivyo Yasin Kanyama akatangazwa ndiye mshindi wa Uenyekiti wa jimbo la Kigamboni kupitia UVCCM.

Halikadhalika upande wa makatibu wagombea wa jimbo la Kigamboni walikuwa ni Kambarage Makongoro aliyepata kura 27, Mustaffa Pilla aliyepata kura 32 na Salum mpili aliyepata kura 16 na matokeo hayo yalimpa ushindi Ndugu Mustafa Pilla kuwa ndiye Katibu wa jimbo la Kigamboni kupitia UVCCM.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .