WANARIADHA WAKO TAYARI KWA KILIMANJARO MARATHON
Posted in
Michezo
No comments
Tuesday, February 18, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
Wanariadha mashuhuri wa Tanzania watapambana vikali ili kushinda medali na fedha katika mbio za Kilimanjaro Marathon 2014 zinazotarajiwa kufanyika tarehe 2 Machi, 2014 mjini Moshi.
Mkurugenzi wa Mashindano hayo John Bayo alisema jana kwamba
wanariadha maarufu wa Tanzania, Andrew Sambu, John Leonard na Daudi Joseph, ni
kati ya wanariadha Watanzania watakaoshiriki katika mbio za kilomita 42 kwa
wanaume.
Katika mbio za kilomita 42 kwa wanawake watakuwepo Banuelia
Brighton, Fabiola William na Flora Yuda ambao wanatarajia kutoa upinzani mkali kwa wanariadha wengine
Watanzania pamoja na wa kigeni.
Andrew Sambu ana rekodi ya kumaliza Korea Marathon kwa muda
wa dakika 2:09:52 mwaka 2004 na mshindi wa medali ya fedha kwenye Mashindano ya
Riadha barani Afrika na ameshiriki Olimpiki wakati Banuelia Brightonakiwa
ameshinda Kigali Peace Marathon mwaka 2009 na kumaliza wa pili Kampala Marathon
mwaka 2011.
Dickson Marwa – mshindi wa Ngorongoro Half Marathon 2013
ambapo alimaliza na 1:4:49 na Alphonce Felix pamoja na Ezekiel Jafari ni kati ya wanariadha ambao wataiwakilisha
Tanzania kwenye kwenye mbio za kilomita 21 kwa wanaume huku upande wa wanawake
ukitarajia kuwakilishwa na Mary Naali, Jacqueline Sakilu na Sarah Ramadhani.
Akiwa ametengeneza rekodi nyingi, Mary Naali ni kati ya
wanariadha bora nchini katika mbio za kilomita 21 maarufu kama Half Marathon. Alishinda
Vienna Marathon mwaka 2010 ambapo alimaliza katika muda wa 1:12:16 na baada ya
hapo akavunja rekodi kwenye mbio za kilomita 25 za Arusha VIP Race mwaka 2011
ambapo alishinda kwa 1 1:20:52 na kuvunja rekodi ya 1:22:18 iliyokuwa imewekwa
na Josephine Deemay mwaka 2006. Mei mwaka 2013 pia alishinda mbio ya Bucharest
International Marathonihuko Romania akimaliza katika muda wa 1:16:32.
Naali atashindana na Sarah Ramadhani ambaye ni bingwa
mtetezi kutokana na ushindi wake kwenye 2013 Kilimanjaro Marathon ambapo
alimaliza mbio akiwa na 1:13:05. Pia katika mpambano huo atakuwemo Jacqueline
Sakilu ambaye ni kati ya wanariadha wanaotarajiwa kufanya makubwa baada ya
kushinda mbio kadhaa za kilomita 21 ikiwemo Uhuru Marathon (1:15:25) na Ngorongoro
Run kwa 1:16:50.
“Tuna furaha kuwa na
kikosi madhubuti kwa wanaume na wanawake,” alisema John Bayo ambaye pia ni
kocha maarufu wa riadha. “Uwepo wa wanariadha hawa wazoefu naamini utaifanya
mbio hii iwe ya kuvutia.”
“Wanariadha wetu wana viwango vya kimataifa. Baadhi ya
wanairiadha wa kiume wameishakimbia chini ya muda wa masaa 2:15:00 huku upande
wa wanawake wakiwa wamekimbia chini ya 2:40:00.Hii ni mbio ya kimataifa ambapo
mshindi anaweza kuwa mtu yoyote kutoka taifa lolote lakini kinachotupa nguvu ni
hamasa tunayoipata kutoka kwa wananchi maana mbio inafanyika hapa nyumbani,
hivyo basi tuko tayari kwa changamoto hii,” alisema.
Nae Aggrey Marealle Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions,
waratibu wa mbio hizo amethibitisha kwamba timu ya wanariadha inayoandaliwa na Holili
Athletics Club imekuwa katika maandalizi kwa miezi 8 iliyopita na wako tayari
kupeperusha bendera. Timu hiyo imepunguzwa kutoka wanariadha 20 hadi 8 bora
ambao wako kwenye maandalizi ya mwisho. Wanariadha wa kambi hiyo wameonyesha
mafanikio baada ya kushinda Rock City Marathon na Dar Rotary Marathon.
John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji
wa mbio hizo amesema takribani washiriki 6,000 kutoka nchi zaidi ya 40 kutoka
mabara sita wanatarajiwa kushiriki kwenye mbio za 12 za Kilimanjaro Marathon.
Mbio
za Kilimanjaro Marathon 2014 zinaratibiwa na Executive Solutions kwa
ushirikiano na Riadha Tanzania, Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro na Kilimanjaro
Marathon Club. Mbio hizo zinadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager (wadhamini
wakuu), Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement,KK Security, Keys Hotel, TPC
Sugar, TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, UNFPA na
Kilimanjaro Water.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :