JERRY SILAA AGAWA DAWATI 300 KWA SHULE ZA SEKONDARI MANISPAA YA ILALA
No comments
Thursday, April 3, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala,
ambaye pia ni Diwani wa kata ya Gongo la Mboto Jerry Silaa akiwasili
kwenye shule ya sekondari Pugu kwa ajili ya kukabidhi madawati 300 kwa
shule tatu zilizopo manispaa ya Ilala na kulakiwa na Mwalimu Mkuu wa
Shule hiyo Jovinus Mutabuzi.(Picha zote na Zainul Mzige).
.Ni katika Mpango wa “Mayor’s Ball” “Dawati ni Elimu, Kalisha mmoja, boresha Elimu”.
Na Zainul Mzige
“Kiongozi hapaswi kutegemea nguvu za
Serikali kufanya shughuli za maendeleo” Hayo ni maneno ya Mstahiki Meya
wa Manispaa ya Ilala ambaye pia ni Diwani wa kata ya Gongo la Mboto,
Jerry Silaa katika hafla ya kukabidhi madawati kwa shule tatu za
sekondari zilizopo Manispaa ya Ilala iliyofanyika Shule ya sekondari
Pugu.
Katika hafla hii, jumla ya madawati 300
yenye thamani ya shilingi milioni 45 za kitanzania yaligawiwa kwa shule 3
zilizopo manispaa ya Ilala ambazo ni Shule ya sekondari Pugu (107),
Shule ya sekondari Ulongoni (93) na Shule ya sekondari Jangwani (100)
kupitia jitihada zake za kuanzisha mpango wa Mayor’s Ball 2013 ulioanza
mwaka jana kupitia kampeni ya “Dawati ni Elimu, Kalisha mmoja, boresha
Elimu”.
Bwana Silaa alitoa pongezi na shukrani za
dhati kwa wote waliotimiza ahadi zao katika kufanikisha zoezi zima la
ununuzi wa madawati mapya na kufanikisha kampeni yenye lengo la kuinua
viwango vya elimu ya sekondari na msingi Tanzania. Pia, alichukua nafasi
kuwaomba wadau waendelea kujitokeza kuchangia elimu kwani ni mara ya
kwanza kwa jambo hili la “Mayor’s Ball” kufanyika nchini.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala
Jerry Silaa, akisaini kitabu cha wageni katika shule ya sekondari Pugu
mara baada ya kuwasili shuleni hapo.
“naomba nitumie nafasi kuwapongeza wadau
wote walioitikia wito huu na naomba kutoa rai kwa wale wote walioahidi
kutimiza ahadi zao ili kufanikisha lengo la kampeni hii iliyobeba kauli
mbiu ya Dawati ni Elimu kalisha mmoja, boresha elimu”, alisema Mstahiki
meya Jerry Silaa.
Katika hotuba yake, amewaasa wanafunzi
kusoma kwa bidii hasa baada ya kuwaboreshea mazingira ya kusomea kwa
msaada wa madawati mapya na ya kisasa.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Gongo
la Mboto, Imelda Samjela, ameiomba serikali kuu kuiangalia shule ya
Sekondari Pugu kwa jicho la pili kutokana na hadhi yake ya kutoa
viongozi nchini na kuifanya iwe na hadhi ya kimataifa. Shule ya
sekondari Pugu inajivunia sifa ya kuwa shule iliyozaa viongozi
shupavuTanzania akiwemo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.
Bi. Imelda aliongeza kuwa kila mwaka
tunapoadhimisha Maisha ya Mwalimu Nyerere basi kufanyike jambo aidha
kupaka rangi na kusafisha mazingira ya shule hiyo iliyobeba historia ya
Taifa la Tanzania. Diwani pia alitoa wito wa kuweka fungu la fedha za
kukarabati majengo ya shule hiyo pamoja na kutokomeza kero ya Kunguni
shuleni.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya sekondari
Pugu, Jovinus Mutabuzi(mwenye suti nyeusi) akizungumzia changamoto
mbalimbali zinazoikabili shule hiyo mbele ya Mstahiki Meya wa Manispaa
ya Ilala Jerry Silaa. wengine pichani ni wakuu wa shule za sekondari
Ulongoni na Jangwani waliojuika katika hafla hiyo ya kukabidhiwa
madawati.
Kunguni wamekuwa ni kero kubwa kwa wanafunzi hasa wakati wakulala. Alitoa angalizo hili kwa mwenyekiti wa huduma za jamii.
Akitoa ufafanuzi wa suala la ukarabati wa
majengo ya shule hiyo, Mwenyekiti wa huduma za Jamii Manispaa ya Ilala,
Bi. Angelina Nalembeka amesema kuwa Manispaa ilishatoa shilingi Milioni
50 kwa ajili ya ukarabati na wanampango endelevu wa kufanya hivyo kila
mwaka. Mpango huu si tu kwa shule ya Pugu bali kwa shule nyingine pia
zinazoizunguka manispaa ya Ilala.
Mwenyekiti huyo pia alithibitisha
kufanyika kwa zoezi la awali la kutokomeza Kunguni shuleni kwa
kunyunyiza dawa na kuwepo kwa mpango endelevu wa kunyunyiza dawa ili
kuondoa kabisa kero hiyo ya Kunguni shuleni.
Mstahiki Meya Jerry Silaa akipitia moja ya mafaili ya taarifa za shule hiyo.
“Mheshimiwa Diwani amefuatilia suala lenu
la Pugu kwa umakini na taarifa zake tunazo katika Halmashauri. Mwalimu
mkuu atakuwa shahidi na tumeshakuja kupiga dawa na bado mwaka huu
tutakuja kupiga dawa tena kuondoa Kunguni” alisema Mwenyekiti, Huduma za
Jamii.
Aidha, Mwenyekiti wa huduma za Jamii
Manispaa ya Ilala aliongeza kuwa suala ya kero la Maji liko kwenye
utatuzi kamati yake ya manispaa yake ilishatembelea shuleni hapo na
kuona kero hiyo.
Amempongeza Mstahiki Meya kwa juhudi zake
za kutatua tatizo la madawati na ameomba wengine pia ambao ni viongozi
wakubwa serikalini waliosoma shuleni hapo wakumbuke walipotoka na
kusaidia kuiweka katika hali nzuri.
Meza kuu ikipokea heshima ya ukaribisho
kutoka kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Pugu (hawapo pichani).
Kutoka kushoto ni Kaimu Diwani wa Upanga Magharibi, Bi. Jokha Lemki,
Diwani wa Kata ya Pugu, Imelda Samjela, Mstahiki Meya, Mwalimu Mkuu wa
Shule ya Sekondari Pugu, Jovinus Mutabazi na Mwenyekiti wa Hudama za
Jamii Manispaa ya Ilala, Angelina Malembeka.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari
Pugu, Jovinus Mutabuzi akielezea furaha yake ya kupokea madawati 107
yaliyotolewa na mpango wa Mayor's Ball 2013 kupitia kampeni ya "Dawati
ni Elimu" chini ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa.
Diwani wa Kata ya Pugu, Imelda Samjela,
akiwasilisha kero ya shule ya Sekondari Pugu kwa Mstahiki Meya wa
Manispaa ya Ilala Jerry Silaa kuhusiana na wadudu aina ya Kunguni kwenye
mabweni ya wanafunzi shuleni hapo ambapo imekuwa kero kubwa wakati wa
kulala na kuwasababisha usumbufu.
Sehemu ya madawati kati ya 300
yaliyotolewa na mpango wa Mayor's Ball 2013 kupitia kampeni yake ya
"Dawati ni Elimu" inayolenga kutatua uhaba wa madawati kwa shule
zilizomo ndani ya Manispaa ya Ilala.
Mwenyekiti wa huduma za jamii manispaa
ya Ilala, Angelina Nyalembeka akitoa ufafanuzi kuhusiana na kero za
wadudu aina ya Kunguni katika shule hiyo ambapo amesema mwaka jana
walipulizia dawa kwenye mabweni yote ya wanafunzi na haraka iwezekanavyo
ataliwasilisha kero hiyo kwenye vikao vya Manispaa na kupatiwa ufumbuzi
na wanafunzi waweza kukaa kwa amani bila usumbufu.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala
ambaye pia ni Diwani wa kata ya Gongo la Mboto, Jerry Silaa, akizungumza
na waalimu pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari Pugu, kabla ya
kukabidhi madawati kwenye hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya
Sekondari Pugu wakifuatilia risala ya mgeni rasmi Mstahiki Meya wa
Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa.
Mstahiki Meya Jerry Silaa akiteta jambo
na mmoja wa wanafunzi wa kidato cha tatu ambaye ni mlemavu Voster Peter
wakati akikabidhi madawati shuleni hapo.
Baadhi ya viongozi wa Kata ya Pugu, Gongo la Mboto na Upanga Magharibi waliohdhuria hafla hiyo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala
Jerry Silaa akifurahi jambo na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu,
Jovinus Mutabuzi, wakati hafla fupi ya kukabidhi madawati 107 kwa shule
hiyo. Kushoto ni Mwenyekiti wa huduma za jamii manispaa ya Ilala, Angelina Nyalembeka akifuatiwa na Diwani wa Kata ya Pugu, Imelda Samjela.
Sasa mtajinafasi wakati wa masomo
darasani si ndio..? Mstahiki Meya Jerry Silaa akimuuliza mmoja wa
wanafunzi wa shule ya sekondari Pugu alipokuwa akikabidhi madawati.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari
Ulongoni, Bi. Sikitiko Salehe,( wa pili kulia) akipokea moja ya madawati
kati ya 93 kwa niaba ya shule yake kutoka kwa Mstahiki Meya Jerry Silaa
ikiwa ni zao la matunda ya Mayor's Ball 2013 iliyoweka kipaumbele
kwenye elimu kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa kwenye dawati katika
hafla fupi iliyofanyika kwenye shule ya sekondari Pugu jijini Dar.
Wanafunzi wa Shule ya sekondari Pugu
wakionyesha nyuso za furaha isiyo na kifani walipokabidhiwa madawati 107
na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa.
Mstahiki Meya Jerry Silaa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali Kata za Gongo la Mboto na Pugu.
Mstahiki Meya Jerry Silaa akiwa kwenye
picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa shule ya sekondari Pugu mara
baada ya kukabidhi madawati 107 kwa shule hiyo.
Kaka mkuu wa shule ya Sekondari Pugu,
Nicetas Ndekubali Ndeng'asso, akitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi
wenzake kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa.
Kaka mkuu wa shule ya Sekondari Pugu,
Nicetas Ndekubali Ndeng'asso akipeana mkono na Mstahiki Meya wa Manispaa
ya Ilala Jerry Silaa.
Mstahiki Meya Jerry Silaa akiondoka
shuleni hapa mara baada ya kumaliza zoezi la kukabidhi madawati kwa
shule hizo za sekondari za manispaa ya Ilala.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :