Posted in
Elimu
No comments
Sunday, May 25, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
WAZIRI MKUU PINDA AHIMIZA MPANGO MAALUM KUMALIZA TATIZO LA MADAWATI RUKWA
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Rukwa uhakikishe
unamaliza tatizo la upungufu wa madawati ili watoto wa shule za msingi
wasiendelee kukaa chini.
Ametoa
agizo hilo jana usiku (Jumamosi, Mei 24, 2014) wakati akizungumza na
viongozi na watendaji wa mkoa wa Rukwa mara baada ya kupokea taarifa ya
Mkoa huo, Ikulu ndogo, mjini Sumbawanga.
Waziri
Mkuu amewasili mkoani Rukwa jana jioni akitokea Dodoma ambapo
atamwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu
Mteule Conrad Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa
itakayofanyika leo (Jumapili, Mei 25, 2014) kwenye Uwanja wa Nelson
Mandela, mjini Sumbawanga.
Akifafanua
kuhusu tatizo la madawati, Waziri Mkuu alisema: “Lazima mjipange kama
mkoa ili muweze kusaidia juhudi za Serikali kupunguza tatizo la madawati
kwa watoto wetu wa shule za msingi”.
“Lazima
mje na mpango maalum… mathalani kwenye Halmashauri zenu huko, angalieni
hizo mbao zinazokamatwa. Badala ya kuziuza, hizo mbao ziende
kutengeneza madawati na yakikamilika yaamuliwe kabisa haya yanakwenda
shule fulani, na utaratibu uendelee hadi shule zimalizike,” aliongeza.
Alisema
utaratibu huo unaweza kumaliza tatizo la upungufu wa madawati kwa
uhakika zaidi kwani hata Halmashauri zinapoamua kupiga mnada mbao
zilizokamatwa, fedha inayopatikana huwa haiendi kutengeneza madawati.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka idara za elimu za mkoa wa Rukwa, Halmashauri
tatu za wilaya za mkoa huo ambazo ni Nkasi, Kalambo na Sumbawanga
Vijijini zinakabiliwa na upungufu wa madawati 33,799, wakati mahitaji ya
madawati ni 62,118 na yaliyopo ni 28,319. Manispaa ya Sumbawanga
ilisema ina upungufu wa madawati 675 bila kutaja yaliyopo ni mangapi
wala mahitaji yake ni kiasi gani.
Akizindua
Wiki ya Elimu Kitaifa mjini Dodoma Mei 3, mwaka huu, Waziri Mkuu
aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI ambayo inasimamia sekta ya
elimu iandae utaratibu wa kuzibana Halmashauri ziwe za mjini au vijijini
kwani zote zina uwezo wa kupunguza tatizo hilo kulingana na fursa
zilizonazo. “Nasisitiza jambo hili liwe ni ajenda ya kudumu,” alisema
Waziri Mkuu.
Mei
14, 2014, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 30 wa Jumuiya ya Tawala za
Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Tanga, Waziri Mkuu aliwataka Mameya na
Wenyeviti wa Halmashauri kuhakikisha wanamaliza tatizo la madawati kwani
nyenzo wanazo kupitia Halmashauri wanazoziongoza.
Mapema,
akiwasilisha taarifa ya Mkoa wa Rukwa, Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi
Stella Manyanya alisema mkoa huo kupitia kamati za shule na uongozi wa
kata umeweka mkakati wa kutatua tatizo la madawati kama njia mojawapo ya
kuboresha taaluma katika mpango wa Matokeo Makubwa na ya Haraka (BRN).
Akizungumzia
kuhusu hali ya miundombinu katika Mkoa huo, Eng. Manyanya alisema kazi
za ujenzi wa barabara za mkoa huo kwa kiwango cha lami unaendelea sasa
baada ya msimu wa mvua kumalizika na baadhi ya wakandarasi kupatiwa
fedha na Serikali.
Kuhusu
usanifu wa Daraja la Mto Momba lililoko mpakani mwa mikoa ya Rukwa na
Mbeya, Eng. Manyanya alimweleza Waziri Mkuu kwamba kazi hiyo imesimama
kutokana na kina cha maji kupanda licha ya kuwa ilipaswa kukamilika
tangu Machi mwaka huu.
“Usanifu
ulitarajiwa kukamilika Machi 2014, lakini kutokana na kina cha maji
kupanda, uchunguzi wa matabaka ya udongo chini ya maji umeahirishwa
mpaka maji yatakapopungua,” alisema.
Hata
hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema wanatarajia kazi ya usanifu na uandaaji
wa nyaraka za zabuni utakamilika mwezi Mei mwishoni na baada ya hapo
zabuni kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo itatangazwa.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :