UNESCO YAWAFUA WATENDAJI WA REDIO JAMII
Posted in
Jukwaa la Habari
No comments
Thursday, September 25, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
Meneja wa Kituo cha Habari na Mawasiliano cha Redio Sengerema mkoani Mwanza Bw. Felician Ncheye, akiwakaribisha na kuwatambulisha wawezeshaji kwa washiriki wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo katika masuala ya masoko na Tehama kwa mameneja na waandishi wa habari takribani 60 kutoka Redio jamii mbalimbali nchini, yanayoendelea kwenye kituo cha habari na mawasiliano cha Redio Sengerema mkoani Mwanza.
Na Mwandishi wetu, Sengerema
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limesema litaendelea kusaidia kuimarika kwa redio za jamii nchini kwa kuwa ndio nyenzo muhimu za maendeleo ya wananchi kwa kuwapa sauti katika huduma na shughuli zao.Kauli hiyo imetolewa na Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa mameneja na watendaji takribani 60 kutoka Redio jamii mbalimbali nchini, mafunzo yanayofanyika kwenye kituo cha Redio Sengerema FM.
Katika mafunzo hayo watendaji hao watafunzwa masuala ya Tehama na utafutaji wa soko kwa lengo la kufanya redio hizo kuwa endelevu na kujiendesha zenyewe kwa kuweza kutekeleza miradi yake na kuendelea kushirikiana na wananchi. Mafunzo hayo ni utekelezaji wa mradi wa miaka mitatu wa kuwezesha redio za jamii nchini unaoendeshwa na UNESCO baada ya redio hizo nyingi kusaidiwa kuanzishwa katika miaka ya karibuni.
Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph akizungumza na Mameneja na waandishi wa habari kutoka redio tisa za jamii wanaohudhuria mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo katika masuala ya masoko na matumizi ya Tehama yanayofadhiliwa na mradi wa SIDA na kuratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Kushoto mgeni rasmi Ofisa mdhani kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar na Mjumbe wa bodi ya usimamizi Redio Jamii Micheweni, Ali Mohamed.
Kwa mujbu wa Yusuph mradi wa SIDA ambao umekuwa ukitekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu umeshughulika na uboreshaji wa redio hizo ili kuzipatia uwiano na pia kuziwezesha kutumia Tehama kuhabarisha wananchi pia kutokana na mafanikio yaliyopatikana mradi huo utaendelea kwa miaka mingine mitatu.
Ametaja mafanikio hayo kuwa yamepatikana kwa ushirikiano wa Redio za jamii pamoja na shirika hilo hali iliyofanya kuyavuta mataifa mengine kuchangia kwa ajili ya kuendelea kuzijengea uwezo redio za jamii kupitia shirika hilo.
Ameongeza kuwa kufanikiwa kwa redio za jamii nchini Tanzania katika mradi huu wa SIDA kumefanya mashirika mengi yanayotaka kufanyakazi na wananchi wa kawaida kukimbilia UNESCO kutambua redio za jamii ambazo zinaweza kufanyakazi nayo. Mradi huo wa Tehama unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) na kuratibiwa na UNESCO ni sehemu ya mradi wa UNESCO katika nchi saba za Afrika , Tanzania ikiwamo.
Baadhi ya Mameneja na waandishi wa habari kutoka redio mbalimbali za jamii wakimsikiliza Bw. Al Amin Yusuph kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendelea kwenye kituo cha habari na mawasiliano Sengerema Telecentre mkoani Mwanza.
Katika mafunzo hayo yanayofanyika mjini Sengerema, elimu inatolewa kwa wakuu wa vituo na waandishi wa habari kutoka redio Micheweni FM, Orkonerei FM, Pambazuko FM, Mtegani FM, Kahama FM, Redio FM, Kyela FM, Fadeco Radio na Pangani FM. "Kuna mambo mengi yamefanikiwa.. kikubwa zaidi kumpa nafasi mwananchi kujieleza na kueleza matumaini yake.." alisema Yusuph ambapo aliongeza kwamba kutokana na mradi huo kufanikiwa zipo nchi na mashirika ambayo yapo tayari kuchangia uimarishaji wa redio za jamii nchini. Hakuzitaja nchi hizo.
Alisema kutokana na mafanikio yaliyopo ya redio hizo kuwa karibu na jamii, SIDA kwa kushirikiana na UNESCO wametengeneza programu hiyo ili kuwezesha kuwepo kwa matumizi ya mtandao katika kukusanya habari, kuziboresha na kuzitumia kwa manufaa ya wananchi.
Ofisa mdhamini kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar na Mjumbe wa bodi ya usimamizi Redio Jamii Micheweni, Ali Mohamed, akitoa baraka zake tayari kuanza mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo katika masuala ya masoko na Tehama mameneja na waandishi wa habari takribani 60 kutoka redio za jamii mbalimbali nchini, yanayoendelea kwenye kituo cha habari na mawasiliano Sengerema Telecentre mkoani Mwanza.
Alisema kutekelezwa kwa mradi huo ni utekelezaji wa azimio la Windhoek la mwaka 1991 linalohimiza matumizi ya redio jamii katika kuboresha maisha ya wananchi kutokana na kuonekana dhahiri kwamba wananchi wanapokuwa na nafasi ya kujieleza wanaweza kufanya makubwa zaidi.
Akifungua mafunzo hayo Ofisa mdhamini kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar na Mjumbe wa bodi ya usimamizi redio jamii Micheweni, Ali Mohamed aliwataka mameneja na watendaji wa radio hizo kutekeleza ushauri wa UNESCO ikiwa na pamoja na kutekeleza maagizo ya utengenezaji wa vipindi vya vijana ili kupata nafasi ya kushindania nafasi moja ya upendeleo kwenda Paris , Ufaransa mwakani kwa tamasha la redio za jamii.
Aidha aliwataka watendaji kuwa makini katika kazi zao kutokana na serikali kuweka mazingira sahihi ya uendeshaji wa radio hizo kwa manufaa ya umma.
Mkufunzi wa darasa la mameneja wa redio mbalimbali za jamii Mkurugenzi Mtendaji wa ASMET, Bw. Ramadhan Ahungu akiendesha mafunzo ya siku tano ya namna ya kuingiza kipato pamoja na kutafuta masoko kwa ajili ya kuendeleza vituo vyao yanayofadhiliwa na mradi wa SIDA na kuratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) yanayoendelea kwenye kituo cha habari na mawasiliano Sengerema Telecentre mkoani Mwanza.
Baadhi ya mameneja wa redio mbalimbali za jamii wanaohudhuria mafunzo ya siku tano ya masoko na ujasiriamali yanayofadhiliwa na mradi wa SIDA na kuratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Meneja wa kituo cha redio Orkonerei FM, Bw. Lucas Kariongi akihoji swali kwa mkufunzi wakati wa mafunzo hayo.
Mhasibu wa kituo cha habari na mawasiliano Sengerema Telecentre, Bw. George Tumbo akiongaza washiriki wenzake katika kazi za vikundi wakati wa mafunzo hayo.
Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph akiendesha mafunzo ya matumizi ya Tehama kuwajengea uwezo wa kuweka kumbukumbu za vipindi na kukusanya vyanzo vya habari kwa kutumia "Tablet" kwa waandishi wa habari wa redio mbalimbali za jamii yanayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) na kuratibiwa na shirika la UNESCO yanayoendelea kwenye kituo cha Redio Sengerema mkoani Mwanza.
Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph akitoa maelekezo ya matumizi ya "TABLET" katika kuhifadhi na kuandaa habari kwa kutumia kifaa hicho.
Pichani juu na chini ni washiriki wa mafunzo hayo wakifanya mafunzo kwa vitendo kwa kutumia Teknolojia mpya ya "TABLET".
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :