WIKI NGUMU KWA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Posted in
Bunge
No comments
Monday, September 29, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
WIKI hii ni kati ya wiki ngumu zilizowahi kulikumba Bunge Maalum la Katiba lililoanza mwanzoni mwa Agosti mwaka huu.
Wakati Bunge linaanza mwanzoni mwa mwaka huu, wajumbe walitumia muda mwingi kujadili sura ya kwanza na ya sita inayohusu muundo wa Serikali na pia walivutana wakati walipokuwa wakijadili kanuni za 37 na 38 za Bunge hilo zinazohusu upigaji kura ya siri au ya wazi.
Leo wajumbe wa Bunge hilo wanaanza kupigia kura sura za rasimu ya Katiba inayopendekezwa iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge.
Chenge aliwasilisha rasimu hiyo baada ya wajumbe kufanya marekebisho na maboresho ya rasimu iliyowasilishwa mwanzoni mwa mwaka huu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Wakati wa kupiga kura hizo kuanzia leo hadi Oktoba 2 mwaka huu, kila mjumbe atakuwa akipiga kura kwa mara moja, ibara zote zilizoko katika kila sura.
Upigaji kura huo utatanguliwa na uwasilishaji wa rasimu nyingine mpya itakayokuwa imebeba maboresho yaliyotolewa na wajumbe wakati wa kuiboresha rasimu hiyo yaliyofanyika wiki iliyopita.
Ili kuhakikisha kila sura inapita, inatakiwa iungwe mkono na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania bara na idadi kama hiyo kwa wajumbe wanaotoka Zanzibar.
Pamoja na baadhi ya wajumbe akiwamo Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kukaririwa mara kwa mara, akisema rasimu mpya itathibitishwa na wajumbe wa Bunge hilo baada ya theluthi mbili kupatikana Tanzania Bara na Zanziba, baadhi ya wajumbe wanasema idadi hiyo haitapatikana.
Baadhi ya wajumbe wanaotilia shaka upatikanaji wa theluthi mbili ni waliojiondoa bungeni baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge hilo wanaoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Viongozi wakuu wa umoja huo, mara kadhaa wamekuwa wakisema uwezekano wa rasimu hiyo kupitishwa ni mdogo kwa kuwa theluthi mbili haipatikani kwa pande zote mbili.
Kwa mujibu wa Ukawa, uamuzi wao wa kujiondoa bungeni na kuwahusisha wabunge na wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kumeliathiri Bunge hilo katika upatikanaji wa theluthi mbili.
Kutokana na hali hiyo, Ukawa wamekuwa wakilalamikia uwepo wa Bunge hilo na kwamba kitendo cha Sitta kuruhusu wajumbe walioko nje ya nchi wapige kura kwa njia ya mtandao, kinaandaa mazingira ya kupatikana kwa theluthi mbili.
Ugumu wa theluthi mbili kupatikana unaweza pia kusababishwa na wajumbe wa Bunge hilo ambao ni Waislam, hasa kutokana na suala la Mahakama ya Kadhi kutoingizwa katika rasimu hiyo ya Katiba inayopendekezwa.
SOURCE: MTANZANIA
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :