PROF. MEGHEMBE: URAIS SI MASHINDANO YA UREMBO

Posted in
No comments
Tuesday, November 18, 2014 By danielmjema.blogspot.com

maghembe

Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe ameshangazwa na utitiri wa watu wanaotaka kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2015, akisema nafasi hiyo ya juu nchini haifanani na mashindano ya urembo ambayo mtu yeyote anaweza kujaribu.
 
Mbunge huyo wa Mwanga alisema watu hao wanaojitokeza kuwania urais hawaelezi wanataka kulifanyia nini Taifa na akashauri wasioweza kueleza hoja zao wasichaguliwe kushika nafasi hiyo.
 
“Urais unahitaji kuwa na sifa, dira na ajenda kwa Taifa,” alisema Profesa Maghembe wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili mjini hapa.
 
Kauli ya Profesa Maghembe imekuja wakati Taifa likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, 2015, huku chama chake, CCM kikikabiliwa na kazi ngumu ya kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake.

 
Hali kama hiyo iliikumba CCM wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 wakati takriban watu 20 walipojitokeza kutaka kuingia Ikulu na baadaye mwaka 2005 wakati wa uchaguzi uliomuweka madarakani Rais Kikwete.
 
Ndani ya CCM, mjadala huo sasa umekumbwa na hoja ya umri baada ya makada vijana kujitokeza kutangaza nia ya kumrithi Rais Kikwete kupambana na wanasiasa wakongwe, baadhi wakiwa ni wale waliojiandaa kwa muda mrefu.
 
Hata hivyo, Profesa Maghembe alipuuza mjadala huo wa umri wa mtu kugombea urais akisema kuwa hauna msingi na kwamba sifa kuu ya mgombea urais ni ajenda ya kuliletea Taifa maendeleo endelevu.
 
“Umri hauwezi kuleta tofauti katika uongozi wa nchi. Ni kama kusema jiwe liwe rais,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe, ambaye amefanya kazi wizara tofauti tangu Januari 2006 aliposhika uwaziri kwa mara ya kwanza.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka mgombea urais awe na umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea.
 
“Hivyo haisemi kuwa ukishakuwa na miaka 70 huwezi kuwa rais ama haisemi ukiwa na miaka 40 unafaa zaidi kuwa rais. Inategemea huyo mtu anayegombea anataka kuwafanyia nini Watanzania,” alisema.
 
Waziri huyo wa saba tangu Wizara ya Maji ianzishwe, alisema kugombea urais kunategemea ajenda aliyonayo mtu na hata watu wanapokwenda kumchagua, lazima waangalie ana ajenda gani. “Ikulu si mahali pa kukimbilia, mimi hata sijui wanakimbilia nini kwa sababu lazima mtu uwe na ajenda. Na kama mnasikia mtu anasema mimi nataka kuwa tu rais, huyo hafai kabisa,” alisema.
 
“Lazima mtu anayetaka kuwa rais atueleze uchumi sasa unakua kwa asilimia saba na umekuwa hivi kwa karibu miaka 10 lakini ni jambo linalofanya umaskini uwe mkali kabisa na usiishe ni kutokana na shughuli inayofanywa na watu wengi ya kilimo, kuwapatia kipato haikui kama sekta nyingine.
 
Alitoa mfano sekta ya usafirishaji ambayo inakua kwa zaidi ya asilimia 28 na sekta ya utalii kwa zaidi ya asilimia 18, lakini sekta ya kilimo inakuwa kwa asilimia 4.2 tu wakati ndiyo inabeba karibu asilimia 77 ya Watanzania.
 
“Lazima hali hii ibadilike huko tunakokwenda. Sasa huyu rais atuambie ataibadilishaje. Mtu anasema anataka aende Ikulu akae hata saa moja tu, sasa saa moja unafanya nini? Hata nusu saa wewe unataka kwenda hapo kufanya nini?” alihoji.
 
Alisema kwa kipindi hiki ni lazima mtu anayetaka urais awaeleze Watanzania atawezaje kuivusha nchi katika uchumi wa kati, vinginevyo haifai kushika nafasi hiyo.
 
“Naona watu wengi wanatangaza, mimi nataka kuwa rais, mimi nataka kuwa rais. Ehhh unatakuwa rais (anaitika ehh), Watanzania unawaondoaje hawa asilimia 77 waungane na wengine ili baada ya miaka yako 10 tuwe katika uchumi wa kati?” alisema.
 
Alisisitiza mtu ambaye anataka kuwa rais lazima awe na sifa na ajenda. “Lazima atueleze ajenda yake nini? Siyo kwamba si unaniona mimi hata wakipiga picha nafaa kuwa rais, hata kidogo,” alisema na kuongeza;
 
“Urais siyo kama mashindano ya Lundenga ya kupeleka warembo kwenda kuwashindanisha hata kidogo. Is Very important (ni muhimu sana), mimi nadhani ndiyo sifa ya msingi.”
 
WANAWAKE NA URAIS

Profesa Maghembe alisema haamini kwamba wanawake bado hawawezi kushika nafasi hiyo ya juu serikalini. Wapewe fursa washindwe wenyewe.
 
Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, wanawake wenye sifa ya kuwania urais na kushinda wapo na wakiweza wajitokeza ili wapigiwe kura.
 
“Unajua kuna wengine wanasema ni mapema. Lakini tangu lini saa hizi saa nane mchana unasema ni mapema, unataka wangoje usiku! Wamama wapo lakini na muda wa kutangaza nia bado upo,” alisema na kuongea:
 
“Pia tunaangalia hawa waliotangaza nia wataifanyia nini Tanzania. Kama wako ambao wanaweza kufanya hiyo kazi, mnaingia huko, siyo marathon.”
 
HATMA YA UBUNGE WAKE

Profesa Maghembe alisema kuwa kazi yake ya ubunge anaipenda sana na kwamba ni kazi inayohitaji nguvu, ubunifu na kuwa tayari kukabiliana na changamoto za maendeleo.
 
“Na ni kazi ambayo inahitaji nguvu, ubunifu na inahitaji kuwa tayari kukabiliana na changamoto za maendeleo. Kazi hiyo naipenda sana na bado nina nguvu na nia ya kuifanya. Kwa hiyo katika uchaguzi mkuu ujao nitagombea katika jimbo langu la Mwanga.
 
“Kwa hiyo mimi siwezi kusema kuwa nikipata upinzani ni kitu kama unfair (siyo cha haki) hivi, hata kidogo. Ni kitu ambacho ni sehemu ndani ya Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
 
Profesa Maghembe alisema ushindani ni kitu ambacho anafahamu kitakuwapo.
 
“Kila wakati ushindani unakuwa mkubwa zaidi, nimepita katika chaguzi tatu na kila wakati upinzani unakuwa mkali zaidi. Nategemea katika mwaka 2015 ushindani utakuwa ni mkubwa zaidi lakini nategemea nitashinda kwa kishindo zaidi,” alisema.
 
Alisema hakuna kosa kwa watu kushindana katika chaguzi na ni haki yao ya uanachama.
 
Alipoulizwa mambo matatu yanayomfanya kutegemea kushinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao, Profesa Maghembe alisema mojawapo ni utekelezaji wa ilani ya CCM na miradi ya maendeleo imetekelezwa.
 
“Wananchi matatizo yao yametatuliwa kwa kiwango kikubwa sana na tupo karibu nao, kuwasikiliza na kuona kuwa tunaelekea wapi,” alisema.
 
Alisema pia wananchi huangalia historia ya kipindi ambacho umeongoza na katika jimbo lako wamekuwa wakipiga hatua kila kipindi na kutokana na hayo utashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao.
 
NAFASI YA UPINZANI 

Profesa Maghembe alisema “Njaa ya wananchi wengi ni maendeleo, hivyo kile chama kinachowaahidi Watanzania kuwaletea maendeleo kitaendelea kushinda wakati wote,” alisema na kuongeza:
 
“Kile kinacholeta matumaini ya mkate wao wa kila siku, kuwapatia watoto shule kuendeleza vyuo vikuu, huduma nzuri za afya, maji na kuhakikisha mazao kuingia sokoni ili wapate bei nzuri kitaendelea kutawala Tanzania kwa muda mrefu.”
 
Alisema bado vyama vingi nchini vinaona kuwa kusimama majukwaani, kutoa sauti kubwa na ukali mwingi ndiyo kutawala nchi.
 
Alisema vyama vitakapofika kwa wananchi katika ngazi ya chini na kutoa mpango mbadala ya kuleta maendeleo nchini ndiyo vitaweza kuwa na ushindani. Alisema hivi sasa vyama vya upinzani havina ushindani na CCM. “Wakina Sangara, operesheni delete, kudelete haiboreshi shule,” alisema.
 
KATIBA

Katika hatua nyingine, Profesa Maghembe alibainisha kuwa Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaendelea vizuri, ila kinacholeta mgogoro ni kitendo cha Tanzania kuingia kwenye mchakato huo wakati bado Katika yake ya mwaka 1977 haijapoteza sifa.
 
Amesema Katiba hiyo iliyotuongoza kwa miaka 50 iliyopita bado ni nzuri, ndiyo maana kuna maoni tofauti juu ya mchakato wenyewe.
 
Alisema Katiba iliyopo imewatumikia vizuri lakini wakasema kuna fursa nzuri ya kutengeneza Katiba nzuri zaidi ya kuwatumikia vizuri zaidi kwa miaka zaidi ya 100.
 
“Watanzania tumekuwa kama wale watu ambao wana koti halijachakaa, zuri tu lakini wakapeleka kwa fundi liwekwe kiraka,” alisema.
 
“Hapo ndiyo tatizo, kwa sababu katika nchi, Katiba ni matokeo ya vita, wamepigana vita sasa wamechoka wanataka tuongee amani, tunaandika Katiba,” alisema na kuongeza:
 
“Sasa sisi tunaandika Katiba mpya tukiwa na amani. Hatuna tatizo kubwa kwamba watu wanapoongalia changamoto hawaliongelei hilo kama tatizo kwa sababu tunayo Katiba nzuri ambayo imetubeba kwa miaka 50.”

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .