SHILINGI BILIONI 321 ZA IPTL ZILITAFUNWA

Posted in
No comments
Monday, November 17, 2014 By danielmjema.blogspot.com


RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ukaguzi wa Akunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa Kampuni ya IPTL iliyowasilishwa bungeni mwishoni mwa wiki, imewaweka kitanzini vigogo wa serikali baada ya kubaini fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh bilioni 306 na zilitakiwa kurudishwa Tanesco.
Vyombo vya habari vilipoanza kuripoti uchotwaji wa fedha hizo Machi mwaka huu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, alisema fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh bilioni 195.2, zikiwamo Dola za Marekani milioni 22 na Sh bilioni 161.Siku chache baada kauli ya Profesa Ndulu, Mmiliki kwa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing iliyokuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL, James Rugemalira, alisema akaunti hiyo ya Escrow ilikuwa na Dola za Marekani milioni 120 (zikiwamo fedha za Tanzania), kauli iliyokinzana na ya Profesa Ndulu jambo lililoongeza utata wa kiasi sahihi cha fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo.
Katika ufafanuzi wake, Rugemalira alisema kati ya fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo, alilipwa Dola za Marekani 75 milioni (Sh120 bilioni) alizoziita ‘vijipesa vya ugoro’ sawa na asilimia 30.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata, katika ukaguzi wake, CAG alibaini kuwa akaunti hiyo ilikuwa na Sh bilioni 306 ambazo ni matokeo ya Tanesco kulipishwa capacity charges (tarifu) zaidi ya kiwango kilichotakiwa kulipwa.
Kutokana na hali hiyo, Tanesco walipaswa kurejeshewa Sh bilioni 321 zilizolipwa ziada kwa IPTL kati ya mwaka 2002 – 2012.
Akaunti ya Escrow ilifunguliwa mwaka 2006 wakati ambao tayari Tanesco ilikuwa imekwisha kuilipa IPTL Sh bilioni 15, kiasi ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na gharama ilizopaswa kulipa.
Inadaiwa pia kuwa kampuni ya PAP haikununua kwa halali asilimia 70 ya hisa za kampuni ya Mechmar ya Malaysia kwa sababu zilikuwa zimezuiwa na mahakama.
“Hawana hati halisi za hisa (share certificates) na PAP ilifanya udanganyifu katika malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za uongo kuwa ilinunua hisa kwa Sh milioni 6 badala ya dola za Marekani milioni 20.
Hali hiyo inadaiwa iliikosesha Serikali mapato ya Sh bilioni 8.7,” alisema mtoa taarifa wetu.
Inaelezwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alivunja sheria kwa kuelekeza kuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye capacity charges ilipwe na kusababisha Serikali kupoteza mapato ya Sh bilioni 21.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini alisaini na kuamuru fedha za Escrow zitolewe bila kuhakikisha fedha za Tanesco zinarudi hivyo kuipotezea Tanesco Sh bilioni 321.
MCHANGANUO
Chanzo chetu kinasema ripoti ya CAG inaonyesha fedha zilizozilipwa zaidi na Tanesco kwenda IPTL kati ya Januari 2002 mpaka Novemba 2006 ilipofunguliwa akaunti ya Escrow ni Sh152,359, 252,000.
Fedha zilizolipwa kwenda Escrow kati ya Desemba 2006, mpaka Machi 2012 ni Sh 84,780,308,00 huku riba ya kiasi kilichokuwa kimelipwa kabla ya kufunguliwa kwa akaunti ya Escrow ni 69,541,507,00 na riba ya Escrow ikiwa Sh 14,360,297,00.
“Kwa hiyo utaona kuwa fedha zote hizo ni Sh bilioni 321.04,” kilieleza chanzo chetu.
Pia sehemu ya ripoti ya CAG ambayo gazeti hili limefanikiwa kuiona, inasema hadi kufikia Machi 2008, Tanesco ilikuwa imekwisha kulipa tozo ya uwekezaji zaidi ya kiwango kilichotakiwa kulipwa IPTL Sh bilioni 157 ambazo zikichanganya na riba zinafikia Sh bilioni 195.7.
Inasema Aprili 2012, Tanesco iliwasilisha madai yake kwa mfilisi wa muda juu ya deni la Sh bilioni 321.04, dhidi ya IPTL kuhusiana na gharama za uwekezaji zilizotozwa zaidi (overstated capacity payments).
Madai ya Tanesco yalikuwa kwamba mtaji halisi wa IPTL ulikuwa ni Sh 50,000, Chanzo kingine kilisema kuwa ripoti hiyo ya CAG inasema kodi ya ongezeko la mtaji ililipwa kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asiliamia 20 kilichopaswa kulipwa.
Inasema kulipwa fedha hizo kidogo kulitokana na nyaraka zilizowasilishwa TRA ambazo hazikuwa na taarifa sahihi.
IPTL ILIULIZWA KUKIWA NA ZUIO LA MAHAKAMA.
Chanzo kingine kilidai kuwa ripoti hiyo inaonyesha Kampuni ya Piper Link Investment ilinunua hisa saba za za Mechmar iliyokuwa na asilimia 70 za hisa IPTL, Septemba 2010 kwa dola za Marekani 20,000,000 na katika kipindi hicho cha mauzo Mechmar haikuwa chini ya ufilisi.
Alisema kuwa mtu ambaye aliteuliwa kuwa msimamizi wa hisa za Standard Charted Hong Kong, za VIP na Mechmar katika IPTL Novemba 2010, alifungua shauri katika Mahakama Kuu ya British Virgin Island (BVI), na siku hiyohiyo hatua ya mahakama kuzuia uuzwaji wa hisa saba za Mechmar ilichukuliwa.
Kutokana na hali hiyo, Piper Link Investment iliingia makubaliano na PAP ya kuuza hisa hizo wakati kukiwa na zuio la mahakama.
VIGOGO WALIOJIWEKA KITAANZINI
1.Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Mara kadhaa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amekuwa akisema fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo siyo mali ya umma bali za kampuni binafsi.
Profesa Muhongo ameendelea na msimamo wake hadi wiki iliyopita alipowaeleza waandishi wa habari kwamba iwapo jamii itajikita katika kuyumbishwa na watu wachache na kuacha kuangalia uhalisia ni dhahiri kuwa itakuwa inajichelewesha kupiga hatua za maendeleo.
“Jamani napenda kusema kujadili suala hili la akaunti ya Tegete Escrow ni sawa na upuuzi kwani fedha hizi siyo za umma kama watu wanavyolazimisha iwe,” alisema.
2.Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Katika Bunge la Bajeti mwaka huu, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, alitaja baadhi ya viongozi wa serikali akisema wanahusika na kuchota fedha hizo.
Akihitimisha hotuba ya bajeti yake na kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alimwagiza CAG na Takukuru kuchunguza tuhuma hizo kubaini ukweli.
“Hoja iliyopo na inayoleta ubishani ni kuondoa fedha kutoka akaunti ya Escrow na kuzipeleka IPTL. Tunajiuliza kama ni ufisadi, ni ufisadi wa nini wakati fedha zile ni za IPTL?” alihoji Pinda.
Hata hivyo, hivi karibuni Pinda alionekana kubadili kauli yake alipozungumzia hatua ya wahisani kusimamisha misaada yao kusubiri ripoti ya CAG aliposema, “yawezekana kabisa kuwa kwenye suala la IPTL kuna uzembe uliofanywa na watu wachache.”
3.Gavana wa Benki Kuu
Machi mwaka huu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, alisema fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh bilioni 195.2, kati yake zikiwamo Dola za Marekani milioni 22 na Sh bilioni 161.
Ripoti ya CAG inaonyesha kuwa kwenye akaunti hiyo kulikuwa na zaidi ya Sh bilioni 300.
4.Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Akizungumza wakati wa Bunge la Bajeti, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema zimekuwapo taarifa potofu kuwa serikali imetoa fedha hizo kuilipa IPTL jambo ambalo si la kweli na ni upotoshaji mkubwa.
Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakisambaza vipeperushi hata ndani ya Bunge kuhusiana na upotoshaji huo ili kuendelea kuwapotosha wananchi.
“Mmoja wa watu wanaosambaza habari hizo ni huyo anayetoa maneno machafu. Kama ni tuhuma au kuna rushwa itakuja kujulikana… kama ni suala ya ESCROW kulikuwa na ugomvi wa familia.
“ESCROW si fedha ya serikali, fedha ya serikali haikai kwenye akaunti hiyo, kama unataka kuleta mambo ya nje nisubiri pale nje,” alifura Jaji Werema na kumfananisha Kafulila na tumbili baada ya kurushia vijembe huku Kafulila akimtuhumiwa kuwa yeye (Werema) ni mwizi tu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, naye amekuwa akitetea uhamishwaji wa fedha hizo huku akiwatuhumu wanaopinga suala hilo.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari Dar es Salaam Juni 27, Maswi alisema, “Juzi (Juni 24) AG alisema tatizo la nchi hii ni wanafiki na waongo… naungana naye kuwaita tumbili. Kama kuna mwanaume aje aseme barabarani hayo maneno yake nimshughulikie. Wanajionyesha wanaume kumbe washenzi tu. Mimi sichukui rushwa najiamini.
“Anakuja mshenzi mmoja anasema bungeni, kwa nini asije huku barabarani akanitambua mimi nani. Werema alisema tumbili na mimi nasema tumbili…. Watu wanalilia hela za IPTL tu.
“… Mwambie Kafulila nimesema wazi yeye ni mshenzi. Kafulila na mwenzake wamechukua hela na wamepewa hayo makaratasi na Mkono (Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono) wanafikiri sijui? Najua.. kwa sababu ya njaa njaa zao. Na nimemwambia kama mwanaume asema openly (wazi) hapa atanutambua mimi nani.. Kwa nini uende kusema bungeni na vipeperushi tu? Tusisemee kule ambapo tunajua ana kinga.”
Deo: Kila mtu atavuna alichopanda.
Wakizungumzia ripoti hiyo, Mbunge wa Ludewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ( PAC) Deo Filikunjombe (CCM), alisema wataifanyia kazi inavyopaswa na hakuna kuoneana haya.
“Ripoti tumeipata kesho(leo) tutakaa kama kamati na kuanza kuifanyia kazi, mimi kama mbunge wa CCM nasema tutaweka mambo bayana. Nisema tu kwamba CCM kwenye hili hatutatazamana usoni wala hatutaoneana haya, kila mtu atavuna alichopanda.
Tutaonyesha kuwa CCM siyo pango la wezi wala mafisadi, mimi kama mwana-CCM nitahakikisha nitaweka haya wazi kuthibitisha kwamba haya hayana baraka za Chama kwa sababu hii ripoti is very shocking (inatisha sana),” alisema.
5.Zitto
Mwenyekiti wa Kamati Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alisema bado wanaendelea kuisoma ripoti hiyo.
“Bado naisoma, ninamshukuru sana CAG kwa kumaliza kazi hii na kujibu hadidu rejea zote. Ni taarifa kubwa yenye majuzuu matatu na kila juzuu lina zaidi ya kurasa 300,” alisema Zitto kwa kifupi.
MWANZO WA MKANGANYIKO
IPTL ilikuwa inamilikiwa kwa ubia na Kampuni ya VIP Engineering and Management iliyokuwa na asilimia 30 za hisa na Mechmar ya Malaysia iliyokuwa na asilimia 70.
Inadaiwa kuwa Piper Link Investments Ltd ilinunua hisa asilimia 70 za Mechmar kwa Sh milioni 6 Septemba 2013 na wiki tatu baadaye iliziuza kwa PAP kwa dola za Marekani 300,000 (Sh milioni 500).
Asilimia 30 za hisa zilizosalia ambazo zilikuwa zikimilikiwa na VIP zilinunuliwa pia na PAP kwa dola zan Marekani milioni 75.
Suala la IPT lilibuliwa kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari kabla ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), kuliwasilisha bungeni.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .