EU, UN WAFAGILIA JUHUDI ZA KUBORESHA HALI ZA WANAWAKE TANZANIA
Posted in
Matukio
No comments
Tuesday, March 10, 2015
By
danielmjema.blogspot.com
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akitoa salamu za Umoja wa Mataifa kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Morogoro miwshoni mwa juma.
Na Modewjiblog team, Morogoro
SERIKALI ya Tanzania imepongezwa na Umoja wa mataifa kwa juhudi zake kubwa inazofanya katika kuhakikisha kuna usawa wa jinsia nchini humu.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez wakati alipopewa nafasi ya kuhutubia umati wa watu waliokusanyika kusherehekea siku ya wanawake duniani ambayo kitaifa ilifanyika Morogoro.
Alisema mbele ya Rais Jakaya Kikwete kwamba kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya awamu ya nne ya kutekeleza maazimio ya kimataifa kuhusu usawa wa jinsia umeifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa yanayostahili kupigiwa mfano.
Akitoa salamu za Umoja wa Mataifa kutoka kwa Katibu Mkuu Ban Ki Moon, mratibu huyo alisema kwamba katika bara la Afrika Tanzania imefanya makubwa katika kuhakikisha usawa wa jinsia na wanawake kuwezeshwa katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kisiasa na utawala.
Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini, Filiberto Ceriani Sebregondi akisoma risala wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Morogoro.
Alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika masuala ya usawa kijinsia na kutolea mfano wa kuwapo kwa asilimia 36 ya wanawake Bungeni.
Aidha amesema kuanzishwa kwa mifumo inayohakikisha kwamba wanawake wanapata nafasi sawa katika masuala ya uongozi, elimu na pia kupitishwa kwa sheria kali ya kukabiliana na masuala ya unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake.
Aidha alisema kwamba miaka 20 iliyopita hali haikuwa sawa lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa japo yanatakiwa mengi zaidi ili kukabiliana na changamoto zilizopo sasa.
Hata hivyo ameitaka serikali kufanya juhudi zaidi katika kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na kuhakikisha kwamba wanawake wanakuwa na sauti katika ngazi zote za utawala kuanzia katika kaya.
Msanii nguli wa muziki nchini, Starah Thomas akiimba wimbo maalum katika siku ya kimataifa ya wanawake duniani ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Morogoro.
Amesema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa bado yapo maeneo ambapo mwanamke amekuwa akidharauliwa na pia kulazimishwa kufanya mambo ambayo ni kinyume na uhuru wa mwanadamu na haki zake za msingi.
Mambo hayo ameyataja kama haki za urithi , umiliki wa ardhi, ndoa za utotoni na ukeketaji.
Aidha kuna utata katika utekelezaji wa mifumo ya sheria inayotakiwa kumlinda mwanamke.
Mratibu huyo alisema kwamba maadhimisho hayo yanatoa nafasi ya kuchambua mafanikio, kuangalia changamoto na kutazama fursa zilizopo katika kuleta mafanikio katika juhudi za kuleta usawa wa jinsia kwa kutekeleza maazimio ya Beijing.
Naye Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini Filiberto Ceriani Sebregondi amesema kwamba ameridhishwa sana na namna Tanzania inavyotekeleza mchakato wa kuelekea usawa wa wanawake na maendeleo kwa wote.
Msanii Peter Msechu akitoa burudani sambamba na baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari Morogoro kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Morogoro.
Amesema Jumuiya hiyo imefurahishwa na nafasi wanayopewa kusaidia Tanzania kufikia ustawi wa jamii kwa kuleta usawa kwa wanawake na wanaume.
Jumuya hiyo imesema kwamba inaamini mchango wake unasaidia kuweka hali bora zaidi kwa wanawake. Amesema jumuiya hiyo kwa bajeti ya sasa wamechangia zaidi ya shilingi bilioni 14 katika miradi ambayo inasaidia wanawake moja kwa moja katika masuala ya wanawake katika ardhi na kilimo,ufundi stadi, fursa za ajira na kuzuia ukatili kwa wanawake.
Alisema kwamba mwaka 2014, walifanikisha mafunzo kwa maofisa jamii 63, dawati la jinsia 150, waendesha mashtaka 200, kamati za shule 200, watu wanaojitolea 6000, pamoja na wazazi na waangalizi kutoka Tanzania na Zanzibar.
Aidha jumuiya hiyo iliwezesha wanawake 8000 wa Mtwara na Kigoma kupata mikopo, mafunzo ya biashara na kumiliki ardhi.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :