TANZANIA: RAIS MAGUFULI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA KATIBU MTENDAJI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI LEO JIJINI DAR ES SALAAM
Posted in
afrika mashariki
No comments
Wednesday, February 24, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Richard Sezibera
Ikulu Jijini Dar es salaam, ambapo pamoja na mambo mengine Rais Magufuli
amepokea taarifa ya maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 02 Machi, 2016 Katika Jiji la
Arusha, Nchini Tanzania.
Rais Magufuli ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
inayojumuisha nchi tano wanachama ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda,
Rwanda na Burundi.
Akizungumza mara baada ya mazungumzo hayo Katibu Mtendaji wa Jumuiya
hiyo Dkt. Richard Sezibera, amesema maandalizi kuhusiana na mkutano huo
yanakwenda vizuri.
Amesema pamoja na mambo mengine mkutano huo, utajadili masuala kadhaa
yakiwemo mpango wa kuanzisha viwanda vya magari ndani ya Jumuiya ili
kupunguza uingizaji wa magari kutoka nje ya nchi na Marais kuzindua pasi
ya kusafiria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kuhusu hali ya Jumuiya, Dkt. Sezibera amesema inaendelea vizuri na
ametaja baadhi ya mambo ambayo yamefanyika kuwa ni kutiwa saini kwa
mkataba wa umoja wa forodha, makubaliano ya soko la pamoja na
makubaliano ya sarafu moja.
Mengine ni kuwepo kwa mazungumzo kuhusu uimarishaji wa miundombinu
kama vile reli na umeme ndani ya Jumuiya, na mazungumzo kuhusu umoja wa
kisiasa.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dkt. Augustine Mahiga, amesema Tanzania
ikiwa ni mwenyeji wa kikao hicho ipo tayari kupokea ugeni na kwamba
pamoja na kufanyika kwa kikao hicho, marais wa Tanzania na Kenya
watafungua barabara inayounganisha Tanzania na Kenya katika Mpaka wa
Holili na kutakuwa na shughuli ya kuweka jiwe la msingi katika kituo cha
pamoja cha mpakani kwa ajili ya kuwezesha upitaji wa mizigo na watu
yaani "One Stop Boarder Post"
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es salaam
24 Februari, 2016
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :